Kila mtu ana maoni kwenye jambo lolote lile, hata lile ambalo mtu hana utaalamu nalo wala halijui kwa undani. Kwa kusikia tu kutoka kwa wengine, tayari na yeye anaweza kutengeneza maoni yake.

Wewe mwenyewe una maoni ya kila aina na kwa kila eneo, hata maeneo ambayo huna utaalamu wala uelewa kwa undani. Una maoni kwenye siasa, michezo, uchumi, dini, mahusiano, afya na maeneo mengine mengi.

Unapaswa kuwa makini sana na maoni, kwa sababu ni rahisi kukupotosha. Na hapa ni kwa pande zote, maoni yako na maoni ya wengine pia.

Maoni ni rahisi kuzalisha hivyo kila mtu ana maoni mengi na kuwa tayari kutoa maoni yake, hata kabla hajaombwa kuyatoa. Wengine wapo tayari kupigania maoni yao yasikilizwe.

Lakini kumbuka ni maoni, na maoni mengine siyo tu hayana msaada, bali ni sumu kabisa.

Unachohitaji wewe ni ukweli, kile ambacho ni sahihi kwa kila eneo, kila mtu na kila wakati. Ukweli haubadiliki, ukweli unasimama kwenye msingi. Kilicho kweli leo, kitakuwa kweli kesho, kilicho kweli Tanzania, kitakuwa kweli Marekani. Hiyo ndiyo sifa ya ukweli, haubadiliki. Lakini maoni yanabadilika kila wakati na kila eneo. Maoni ya kesho yanaweza kuwa tofauti kabisa na maoni ya leo.

Kuwa makini sana na maoni yako binafsi na maoni ya wengine pia, mengi ni sumu na yatakupoteza. Mara zote tafuta ukweli uko wapi na simama nao, na puuza sehemu kubwa ya maoni unayopata.

Na kama kweli unataka kupata maoni, basi yapate kwa mtu ambaye kweli ni mtaalamu au ana ujuzi wa kina kwenye eneo hilo. Mtu ambaye ameweza kufanya kitu chenye manufaa kwenye eneo hilo na hapo anaweza kuwa na maoni yenye mchango fulani.

Lakini mtu ambaye ana maoni, lakini yeye mwenyewe hajawahi kuyafanyia kazi, kuwa makini na maoni hayo, yatakupoteza.

Mara zote simama kwenye ukweli, na kama unataka maoni basi chukua ya wale ambao wanazalisha matokeo kwenye eneo unalotaka kupata maoni.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha