Upo usemi kwamba tatizo la mbio za panya ni kwamba hata ukishinda, unabaki kuwa panya. Ni usemi unaohusu zaidi eneo la fedha, hasa pale unapoishi maisha ya mashindano, kwamba hata ukiwashinda wengine, bado unaishia kuwa kama wao.
Leo nataka tupeleke usemi huo kwenye eneo jingine la maisha yetu, eneo ambalo tumekuwa tunapoteza nguvu na muda, halafu mwisho wa siku hakuna unachonufaika nacho.
Eneo tunalokwenda kuliangalia leo ni ubishani kuhusu watu wengine.
Mara kwa mara huwa unajikuta kwenye hali ya kutokukubaliana na wengine kuhusu watu wengine. Na hili huwa linahusu watu ambao wana umaarufu fulani. Wanaweza kuwa viongozi, wanasiasa, wasanii, wanamichezo, wafanyabiashara na kadhalika.
Hawa ni watu ambao sehemu kubwa ya maisha yao inajulikana hadharani, na hivyo kila mtu kuwa na maoni yake kuhusu watu hao. Wewe pia unakuwa na maoni yako. Sasa unapokutana na mtu mwingine ambaye ana maoni ya tofauti kuhusu mtu huyo, unakuwa tayari kubishana na kupinga maoni ya mwingine.
Chukua mfano kuna kiongozi A, ambaye kwa mtazamo wako ni kiongozi mbovu kabisa na aliyeharibu mambo mengi, lakini kuna wengine wanaona ni kiongozi bora kabisa kuwahi kutokea. Unapokutana na watu wa aina hiyo utabishana nao, utawapa ushahidi kwa nini huyo ni kiongozi mbovu kabisa.
Sasa unajua hao wengine watafanya nini? Unajua kabisa hawatakubaliana na wewe, wataendelea kushikilia msimamo wao kwamba huyo ni kiongozi bora kuwahi kutokea na watakuoa kila aina ya ushahidi kuthibitisha kile wanachosimamia.
Mwisho wa siku mtachoka kwa kubishana na kila mtu ataondoka akiwa na msimamo ule ule aliokuwa nao mwanzo. Pamoja na kuweka nguvu na muda, hakuna chochote ulichofanikisha, umeendelea kubaki na msimamo wako na upande mwingine umebaki na msimamo wake.
Ninachotaka ujifunze hapa ni kuepuka kubishana vitu ambavyo havitaleta matokeo yoyote ya tofauti. Na karibu kila aina ya ubishani, huwa haileti matokeo yoyote ya tofauti. Kama kuna kitu unataka kujifunza, chagua ni kupitia nani unaweza kujifunza kitu hicho, kisha nenda kwake kajifunze na siyo kuleta ubishi.
Kama wengine wana maoni yanayotofautiana na yako kwenye jambo lolote, kwanza jiulize kama ni jambo muhimu na lenye manufaa kwako, kama ndiyo basi chunguza maoni yapi ni sahihi, ya kwako au yao na ukishajua ukweli basi nenda na ukweli huo. Kama jambo siyo muhimu achana nalo, usipoteze muda wako kutafuta ukweli. Na kama umetafuta ukweli na ukajua wewe ndiyo uko sahihi na wengine wamekosea, kaa na ukweli wako, usiwalazimishe waone ukweli unaoona wewe labda kama watakuja kwako kutaka kujua ukweli, wakiwa tayari kujifunza na siyo kutetea kile wanachoamini wao.
Watu wengi wamekuwa wanapoteza muda na nguvu nyingi kubishana kuhusu maisha ya watu wengine, kitu ambacho hakina matokeo yoyote yenye tija kwao.
Ushauri wangu kwako ni kila muda unaotaka kubishana, acha mara moja na chukua kitabu usome au tafuta kitu ujifunze, au tafuta mteja mpya wa biashara yako, au kamilisha kazi ambayo bado hujakamilisha. Kuna mengi yako mbele yako ambayo umekuwa unajiambia huna muda wa kuyafanya, halafu unaenda kupoteza muda huo kubishana!
Anza sasa kujiwekea vipaumbele sahihi na mambo yasiyo na tija kama hayo ya kubishana yatakimbia yenyewe kwenye maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,