Wakati tunasoma, somo la hisabati lilikuwa linaonekana ni somo gumu kwa wanafunzi walio wengi. Hivyo wale ambao walikuwa wanaliweza somo hilo walionekana kuwa na kipaji. Kulikuwa na kauli kabisa kwamba ‘hesabu ni kipaji’
Kwenye mafanikio pia, wapo wengi wanaoamini kwamba mafanikio yanahitaji mtu uwe na kipaji fulani. Na hapo wanatumia mifano ya wale waliofanikiwa kwa vipaji vyao.
Japo ni kweli kwamba kipaji kinamsaidia mtu kufanikiwa, una nafasi kubwa ya kufanikiwa hata kama huna kipaji.
Lakini ukweli mwingine ni kwamba, kila mtu ana kipaji, kama unajiona huna kipaji ni kwa sababu umetelekeza kipaji chako mpaka umefikia hatua ya kukisahau kabisa.
Leo nataka nikuoneshe kwamba tatizo siyo kipaji, bali tatizo ni maamuzi na kujitoa. Kama hujafikia mafanikio unayotaka, kinachokuzuia siyo kipaji, bali zile hatua unazochukia.
Kuna mambo mengi ambayo ukiyafanya utajiweka kwenye nafasi ya kufanikiwa sana, na mambo hayo hayahitaji uwe na kipaji chochote kile. Hapa nitayaorodhesha kumi ambayo ukiyazingatia utafanikiwa, hata kama unajiambia huna kipaji.
- Usomaji. Huhitaji kipaji ili uweze kusoma na kujifunza vitu vipya. Lakini tabia hii ya kusoma itakufundisha mengi, utaweza kuziona fursa nyingi na kufanikiwa sana.
- Kuwa mwema kwa wengine, hakuna anayezaliwa na kipaji cha wema. Lakini kuwa mwema kwa watu wengine kunaimarisha mahusiano yako na hilo linakusaidia kufanikiwa.
- Kutuliza akili yako na kutafakari kwa kina.
- Kujaribu vitu vipya kila wakati.
- Kupata muda wa kutosha kupumzika.
- Kufanya mazoezi ya mwili.
- Kula kwa afya.
- Kwenda hatua ya ziada kwenye kile unachofanya.
- Kuwa na nidhamu ya hali ya juu.
- Kuwa na uadilifu.
Mambo hayo 10, hayahitaji uwe na kipaji, bali yanakutana ufanye maamuzi ya kuyafanya na kisha uwe na msimamo kwenye kuyafanya. Kwa njia hiyo, utapata matokeo ambayo ni makubwa.
Acha kusingizia kipaji na anza kufanya mambo hayo kila siku.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,