“One has to kill a few of one’s natural selves to let the rest grow — a very painful slaughter of innocents.” – Henry Sidwick

Kila mkulima anajua jambo hili muhimu sana,
Kama amepanda mazao yake, kisha yanapoota anakuja kukuta shina moja lina miche mingi,
Hafurahii kwamba shins hilo litazaa sana, badala yake anapunguza miche iliyopo kwenye shina hilo,
Yaani kuna baadhi anaiua kwa makusudi.
Anaondoa miche mingi na kubakiza mmoja au miwili.
Hafanyi hivyo kwa sababu hataki mavuno mengi, ila kwa kufanya hivyo ndiyo atapata mavuno mengi na bora.
Ukiacha miche mingi iote kwenye shina moja, yote haitazaa vizuri, kwa sababu itanyang’anyana virutubisho na mbolea iliyopo.
Lakini ukipunguza na kuacha mmoja au miwili, itakua vizuri kwa sababu hakuna ushindani.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwako,
Hupigi hatua kubwa kwa sababu una miche mingi imeota ndani yako,
Na miche yote inanyang’anyana muda na nguvu ulizonazo.
Hivyo badala ya kuweka rasilimali hizo adimu kwenye kitu kimoja au vichache na upate matokeo makubwa, unazitawanya kwenye vitu vingi na kupata matokeo ya hovyo.

Unahitaji kufanya jambo ambalo linaweza kuonekana ni la kikatili, lakini lenye manufaa.
Jambo hilo ni kuua baadhi ya nafsi zako, kung’oa mashina ya ziada yaliyoota ndani yako.
Unaweza kufanya mengi, unaziona fursa nyingi kubwa na nzuri,
Lakini nguvu na muda vina uhaba kwako.
Hivyo kwa makusudi kabisa jiambie naachana na haya mazuri ninayoweza kufanya, ili nipeleke nguvu na muda wangu kwenye haya machache yatakayoniwezesha kuwa bora zaidi.

Asili haina nafasi ya vitu vingi kukua vizuri kwenye eneo moja.
Kadhalika wewe huna nafasi ya nafsi nyingi kukua vizuri ndani yako.
Ua baadhi ya nafsi ili utoe nafasi kwa nafsi chache kukua vizuri.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,
http://www.t.me/somavitabutanzania