Mwanahisabati Pythagoras aliwahi kusema nipe nyenzo ndefu na mahali pa kusimama na nitaweza kuisogeza dunia.

Hapa alionesha jinsi ambavyo nyenzo ina nguvu ya kufanya makubwa, yale ambayo kwa hali ya kawaida hayawezekani.

Chukua mfano wa nyenzo kwenye maisha yetu ya kila siku, kung’oa msumari mahali kwa mikono yako ni zoezi gumu, lakini kwa kutumia nyundo linakuwa zoezi rahisi. Kadhalika kufungua chupa ya soda kwa mikono yako ni vigumu mno, ila kwa kutumia kifaa cha kufungulia chupa, inakuwa rahisi.

Kwenye kila tunachofanya kwenye maisha, tunaweza kupunguza ugumu wake tukijua nyenzo sahihi.

Mfano kwenye biashara, nyenzo sahihi ni mtaji na watu. Unahitaji mtaji zaidi ili kukuza biashara yako na pia unahitaji watu wa kukusaidia ili biashara hiyo iweze kukua. Bila nyenzo hizo, itakuwa vigumu kwa biashara kukua.

Kwenye kuwabadilisha watu, unapotumia nguvu zako kuwataka watu wabadilike, wanakuwa wakali na watakupinga kuhakikisha hawabadiliki, hivyo zoezi hilo litakuwa gumu mno.

Lakini unapojua nyenzo sahihi ya kuwafanya watu wabadilike, na kisha kutumia nyenzo hiyo, utashangaa jinsi watu wanavyobadilika wenyewe, tena haraka.

Nyenzo ya kuwabadili watu ni motisha, kujua kile wanachokitaka sana, kisha kuwapatia pale wanapofanya kile unachotaka wafanye. Ukishajua kile ambacho mtu anakipenda kweli, kile ambacho hayuko tayari kuishi bila kuwa nacho, unaweza kukitumia kumbadilisha.

Unachofanya ni kumpa kitu hicho pale anapofanya unachotaka afanye au anapokuwa na tabia unayotaka awe nayo. Na yeye atalazimika kufanya au kuwa na tabia hiyo ili aendelee kupata kitu hicho.

Wale wanaosema hawawezi kubadilika ni kwamba tu hawajawa na motisha wa kutosha kuwasukuma kubadilika. Na wale wanaolalamika wameshindwa kuwabadili wengine, ni kwa sababu wanatumia nguvu zao binafsi kitu ambacho kinashindwa.

Nyenzo ni kanuni ya asili katika kutusaidia kupata matokeo makubwa kwa kuweka juhudi ndogo, itumie kwa kila unachofanya. Usihangaike na nguvu zako pekee, bali tumia nyenzo kupata matokeo makubwa kwa nguvu kidogo ulizonazo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha