Tunaishi kwenye zama za taarifa, ambapo kila mtu ana uwezo wa kupata habari mara inapotokea popote pale duniani. Japokuwa tunaona ni maendeleo mazuri, kujua kila kinachoendelea duniani, lakini hilo linakuja na madhara makubwa kwetu.

Makampuni yanayoendesha vyombo vya habari huwa yanapata faida pale watu wengi wanapofuatilia habari zao. Kisaikolojia, sisi binadamu huwa tunapenda kufuatilia zaidi habari ambazo ni hasi kuliko chanya. Hivyo ili makampuni hayo yapate faida, yamekuwa yanatoa habari nyingi hasi ili wengi wayafuatilie.

Upo usemi kwamba mbwa akimng’ata mtu hiyo siyo habari, lakini mtu akimng’ata mbwa, hiyo ni habari ya kusisimua. Hivyo makampuni hayo yamekuwa yakiangalia matukio machache yasiyo ya kawaida na kuyapa uzito zaidi ili kuteka umakini wa watu wengi.

Isingekuwa na shida sana kama ukipata habari hizo unaendelea na maisha yako. Lakini madhara ya habari nyingi unazozipata ni makubwa kwenye maisha yako. Ufuatiliaji wa habari imekuwa chanzo cha wengi kupata msongo, kukosa utulivu, kukosa furaha na hata hekima. Zaidi ya yote kadiri mtu anavyofuatilia habari, ndiyo anakuwa mjinga zaidi kuhusu uhalisia wa mambo.

stop reading news.jpg

Mwandishi Rolf Dobelli alilitambua hilo kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, baada ya kuona kadiri anavyofuatilia habari ndivyo kazi zake za uandishi zinakosa ubora aliotaka. Alijaribu njia nyingi za kudhibiti habari, mfano kuchagua vyombo vichache vya kufuatilia, kusoma habari muda fulani kwenye siku, lakini njia zote hizo zilishindwa.

Hivyo aliamua kuchukua hatua moja ngumu na inayohitaji kujitoa kweli kweli, aliamua kuachana na habari moja kwa moja. Yaani aliamua hatofuatilia tena habari kwenye maisha yake. Alifanya hivyo miaka zaidi ya 10 iliyopita na japo mwanzo ulikuwa mgumu, baadaye alizoea na maisha yake yakaenda vizuri kabisa kuliko alivyokuwa anafuatilia habari.

Mwaka 2013 Rolf alikuwa anahojiwa na gazeti la The Guardian la nchini Uingereza kuhusu kitabu chake kingine kinachoitwa The Art Of Thinking Clearly. Rolf alikuwa amezungukwa na wanahabari zaidi ya 50 na amejiandaa kuelezea kitabu chake, lakini mhariri alimuuliza swali tofauti, kwamba amesoma kwenye tovuti yake huwa hafuatilii habari, anaweza kufafanua hilo. Rolf anasema hakutegemea swali la aina hiyo, tena kutoka kwa wanahabari, lakini aliamua kuwa mkweli na kuwaeleza kwamba wanachofanya siyo kupasha habari, bali kuburudisha tu. Aliwapa hoja zake kwa nini habari nyingi hazina manufaa kwa wengi. Mwisho wa mahojiano mhariri alisema hoja za Rolf zichapwe kwenye gazeti. Na hapo ndipo ulipoibuka mjadala mkubwa, uliopelekea Rolf kuandika kitabu hiki cha Stop Reading the News ili kueleza kwa kina hoja zake na kuwasaidia wengine kuchukua hatua kama zake.

Jinsi ya kuacha kufuatilia habari.

Rolf anatushirikisha jinsi yeye alivyokuwa mfuatiliaji wa karibu wa habari tangu alipokuwa mdogo. Ulikuwa utaratibu wa familia yao kila siku asubuhi kusikiliza taarifa ya habari, baada ya hapo mchana baba yake angenunua gazeti ambalo lilisomwa na familia nzima. Na usiku walikaa wote pamoja kuangalia habari za siku nzima.

Kwa kufanya hivi aliamini kwamba alikuwa ana taarifa sahihi za kila kinachoendelea duniani na hata kwenye jamii yake pia. Alikuwa akishika gazeti anasoma kila habari kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Wakati marafiki zake walikuwa wakicheza na kufanya mambo mengine ya kuwaburudisha na kuwapumzisha, yeye alitumia muda mwingi kusoma na kufuatilia habari.

Anaendelea kueleza ujio wa intanteni kwenye miaka ya 1990 ilimfanya azidi kufuatilia habari nyingi kutoka kila kona ya dunia. Kila wakati alikuwa akifuatilia habari mpasuko zinazoendelea dunia nzima. Na kadiri alivyokazana kusoma habari zote mpya, ndivyo habari nyingine mpya zilikuwa zinaingia. Hili lilimchosha sana.

Baada ya kuwa mfuatiliaji wa habari kwa muda mrefu, huku akiwa anachoshwa sana na hilo, Rolf alikaa chini na kutafakari kipi amenufaika nacho kwenye kufuatilia habari. Katika tafakari hiyo alijiuliza maswali mawili; je ninaielewa dunia vizuri sasa? Na je ninaweza kufanya maamuzi bora? Anasema majibu ya maswali yote mawili yalikuwa HAPANA. Yaani licha ya kuweka maisha yake yote kufuatilia habari, hakuwa ameielewa dunia vizuri na hakuweza kufanya maamuzi bora.

Na hapo ndipo alipochukua hatua ya kuanza kupunguza kufuatilia habari. Alianza kwa kujitoa kwenye vyombo vya habari alivyojiandikisha ili kuwa wa kwanza kupata habari, akapunguza vyombo vya habari alivyokuwa anafuatilia na kupunguza muda wa kuvifuatilia kwa siku. Lakini hayo yote hayakusaidia, alikuwa ameshakuwa mteja wa habari kiasi kwamba hata kwenye chombo kimoja alijikuta akihangaika na habari nyingi.

Ndipo siku moja akaamua imetosha, akajiambia kuanzia siku hiyo hatafuatilia tena habari ya aina yoyote ile. Yalikuwa maamuzi magumu na ya haraka, lakini yalimsaidia sana. Anaeleza hayakuwa maamuzi rahisi, kwa sababu marafiki zake wengi ni waandishi wa habari na hivyo ilikuwa vigumu kujadiliana nao wanapokutana.

Lakini alisimamia maamuzi yake hayo na tangu mwaka 2010 mpaka sasa hajarudi tena kwenye habari. Ameweza kuachana na habari kabisa na hilo limempa uhuru mkubwa, limeboresha maisha yake, ameweza kufikiri kwa usahihi na amekuwa na muda mwingi wa kufanya yale muhimu. Alianza hilo kama jaribio lakini baadaye ikawa ndiyo falsafa yake ya maisha.

Hivyo anapotuambia sisi tuachane na habari, ni kwa uzoefu wake binafsi na anajua manufaa ambayo mtu atayapata kwa kuacha habari. Na zaidi, hakuna ambacho mtu utakosa au kupitwa nacho kwa sababu umeachana na habari.

Habari ni sukari ya akili.

Rolf anatuambia pale mtu unapotumia sukari kwa wingi, mwili wako huwa unazoea sukari hiyo na pia inakuletea madhara kama uzito uliopitiliza na magonjwa mbalimbali.

Hivyo pia ndivyo habari zilivyo, madhara yake ni kwenye akili yako, ambayo inazoea habari hizo na kukuletea madhara kama msongo wa mawazo na magonjwa mengine ya akili.

Habari nyingi unazofuatilia hazigusi maisha yako moja kwa moja, nyingi ni za mambo yanayoendelea huko duniani, ambazo hata ukizijua hazibadili chochote kwenye maisha yako binafsi.

Vyombo vya habari pia vimekuwa vinaremba habari zake kwa kuziita habari mpasuko (breaking news), ili kukuonesha kwamba habari ni ya moto na muhimu zaidi kwako. Lakini ukweli ni kwamba, kadiri habari inavyokuwa ya mpasuko, ndivyo inavyokosa umuhimu kwenye maisha yako binafsi.

Njia pekee ya vyombo vya habari kuingiza fedha ni kupitia matangazo. Ili watu watangaze kwenye chombo husika, lazima kiwe na wafuatiliaji wengi. Sasa kwa kuwa huwa tunapenda kufuatilia habari chanya na zinazosisimua, vyombo vya habari vinalazimika kutoa habari za aina hiyo kwa wingi, ili viwe na wafuatiliaji wengi na hivyo kupata matangazo mengi na kuingiza faida.

Ujio wa mitandao ya kijamii na simu janja umeongeza sumu kwenye kusambaa kwa habari. Sasa hivi vyombo vingi vya habari vinalazimika kuzalisha habari kwa wingi zaidi, kwa wasomaji ambao wanazipata bure, kwa lengo la kuuza matangazo. Hali imezidi kuwa mbaya katika zama hizi kuliko kipindi cha nyuma ambapo watu walipata habari kwa kulipia, kama kununua magazeti.

Ili unaswe kwenye habari, zimegeuzwa kuwa kama sukari kwenye akili yako, zinavutia, ni rahisi kumeng’enya na uharibifu wake ni mkubwa kwenye akili yako. Mtu anaweza kufuatilia habari nyingi kwa haraka, na mwisho ukamuuliza amejifunza nini asiwe na cha kukujibu. Hapo ndipo habari zimetufikisha kwa sasa.

Achana na habari mara moja.

Kama kile ulichojifunza mpaka sasa kinaleta maana kwako, kwa kuona jinsi habari zimekuwa zinakuweka roho juu juu kwa mambo ambayo yanapita na kusahaulisha, Rolf ana ujumbe mfupi kwako; amua leo kuachana na habari kabisa. Futa kabisa kila urahisi ulionao wa kupata habari, jiondoe kwenye vyombo vya habari ulivyojiandikisha, futa programu za habari kwenye simu yako, uza tv yako, acha kusikiliza redio, usinunue magazeti na acha mara moja kutembelea tovuti yoyote ile ya habari. Fanya hivyo mara moja bila ya kufikiria mara mbili.

Unapokuwa unasafiri, beba vitabu vya kukutosha na muda unaoupata, wakati wengine wanasoma magazeti na kufuatilia habari, wewe soma vitabu. Hata unapokuwa unapita karibu na habari, mfano eneo lenye magazeti, angalia mbali kabisa usije kushawishika kuangalia vichwa vya habari kwenye magazeti hayo. Ukienda eneo ambalo watu wanaangalia habari tafuta njia ya kuondoka mara moja kabla na wewe hujaanza kufuatilia.

Kama bado unataka kujua nini kinaendelea duniani, unaweza kuchagua chombo kimoja cha habari cha kimataifa na kuwa unaangalia tu vicha vya habari, mara moja kwa wiki. Mfano jarida la The Economist wana kipengele cha habari za wiki nzima, ambapo utaweza kujua nini kinaendelea duniani. Lakini hakikisha unaishia kupitia kwa juu juu tu, usipoteze muda wako kuzama ndani.

Unaweza pia kuchagua kusoma majarida ambayo yanachambua habari zake kwa kina, maana hapo yanakuwa yanakupa kitu cha kujifunza. Lakini hizi habari fupi fupi, hazina cha kukufunza zaidi tu ya kushika umakini wako ili uoneshwe matangazo mbalimbali.

Weka muda wako mwingi kwenye kusoma vitabu, na unapokutana na kitabu kizuri ambacho umejifunza mambo mzuri, kisome mwanzo mpaka mwisho na kisha rudia tena kukisoma. Unaposoma kitabu mara mbili unajifunza kwa kina zaidi. Vitabu vinakupa nafasi ya kujifunza kwa kina huku kikikuba utulivu tofauti na ilivyo kwenye habari.

Kama unafanya utafiti mtandaoni na umeandika kitu kwenye mtandao wa Google ili kupata taarifa zaidi, unaweza kujikuta kwenye tovuti ya habari. Hakikisha unasoma kile kilichokupeleka pale tu, usishawishike kufungua habari nyingine.

Mpango wa siku 30.

Kama unaona kuacha habari zote mara moja haiwezekani, Rolf anakushirikisha mpango wa siku 30. Hili ni jaribio la kuacha kufuatilia habari zote kabisa kwa siku 30. Unajipa siku 30 tu ambapo unaachana kabisa na habari, kwa ahadi kwamba kama siku 30 zitaisha na bado ukaona ni muhimu uendelee kufuatilia habari, bado utafanya hivyo. Ila kwa sasa ni siku 30 bila habari.

Wiki ya kwanza ya mpango huu itakuwa ngumu kwako. Inahitaji nidhamu kubwa kuacha kufuatilia habari, utaona kama unapitwa na mambo yanayoendelea, kama vile kuna hatari itakuwa inatokea na wewe pekee ndiye usiyejua. Utajiona kama umetengwa na dunia. Yote haya yasikushawishi urudi kwenye habari, badala yake endelea na mpango wako wa siku 30, huku ukijiambia ni siku 30 tu, zikiisha unaweza kurudi kwenye habari.

Katika mpango huu wa siku 30, utaanza kuona una muda mwingi kuliko ilivyokuwa awali. Utajikuta huna cha kufanya na muda huo, na hapo ndipo unapopaswa kuutumia vizuri. Chagua vitabu vizuri utakavyokuwa unavisoma, au majarida yanayochambua mada mbalimbali kwa kina. Unaweza pia kujiunga na kozi mbalimbali zinazotolewa mtandaoni. Chagua kitu utakachojifunza kwenye muda wa ziada unaoupata unapoachana na habari, kitu ambacho kitakupa ubobezi ambao wengine hawana.

Hakuna mtu amewahi kuwa mbobezi kwenye habari, kwa sababu habari ikishatoka, kila mtu anaijua. Hivyo kama unataka ubobezi, chagua kitu ambacho wengine hawakijui kwa urahisi, wewe weka muda kujifunza kitu hicho na ukibobea, utakuwa tofauti na wengine huku ukijiongezea fursa za kupiga hatua zaidi.

Mwanzo ni mgumu, kila wakati utapata matamanio ya kufuatilia habari jambo kwa kidogo. Yashinde matamanio hayo kwa kusimama kwenye maamuzi yako. Kadiri siku zinavyokwenda utaona matamanio hayo yakipungua na inakuwa rahisi kwako kukataa kufuatilia habari. Hapo unakuwa umefika hatua ya pili ya kuachana na habari.

Kwenye wiki ya mwisho ya siku zako 30 za majaribio, utagundua mabadiliko makubwa sana ndani yako. Utajikuta wewe mwenyewe unazikataa habari, yaani hutaki hata kuzifuatilia tena. Hapo ni kwa sababu unakuwa umeshaona jinsi umepata muda wa kujifunza mengi, lakini pia unagundua hakuna chochote cha maana kilichokupita kwa kutokufuatilia habari. Hapa unakuwa umefika hatua ya tatu na unakuwa huru kabisa kwenye utumwa wa habari.

Njia nyepesi ya kuacha habari.

Kama mpango huo wa kuacha habari mara moja unaonekana mgumu kwako, kuna njia nyingine rahisi za kuachana na habari. Kwa njia hii, unachagua kuachana na habari za kila siku, yaani hununui wala kutembelea tovuti za magazeti, wala husikilizi au kuangalia habari. Badala yake unachagua gazeti au jarida linalotoka kila wiki na kisha unasoma jarida hilo, kwa nakala iliyochapwa na siyo mtandaoni. Jarida lililochapwa halina usumbufu kwenye kusoma kama unaposoma mtandaoni, ambapo unaletewa habari nyingine zinazohamisha umakini wako.

Kusoma habari mtandaoni kunahitaji nguvu na kunavuruga umakini wako kuliko kusoma kwenye nakala iliyochapwa. Hii ni kwa sababu ukiwa mtandaoni unasoma habari mtandaoni, unaletewa habari nyingine zinazofanana na hiyo. Hivyo kila wakati utakuwa unajiuliza au nisome na hii, vipi hii nyingine. Maswali kama hayo yanaondoa umakini wako kwenye kile unachosoma. Ukisoma kwenye nakala iliyochapwa, hakuna usumbufu wa aina hiyo.

Unaposoma habari hizo za wiki, soma mara moja tu, usiweke kiporo na kujiambia utasoma siku nyingine ukiwa na nafasi. Kama huna nafasi sasa jua hutakuwa na nafasi baadaye, hivyo chagua kusoma zile habari muhimu tu.

Hatua za kuchukua unapoanguka.

Rolf anatuambia kuna wakati mtu unaanguka na kurudi tena kwenye habari, hiyo siyo dhambi, bali unapaswa kutambua hilo na kuchukua hatua sahihi.

Rolf anatushirikisha wakati ambao yeye alianguka kwa kurudi kwenye habari. Ilikuwa mwaka 2016 wakati wa uchaguzi mkuu wa nchini Marekani ambapo Donald Trump alishinda uchaguzi huo. Anasema alijikuta akiwa na shauku ya kufuatilia kinachoendelea na hapo alijikuta amesharudi kwenye kufuatilia habari. Alijikuta akirudi kwenye hofu, wasiwasi, kushindwa kufikiri kwa umakini na kupoteza muda.

Alipotambua hili aliamua kurudi kwenye msimamo wake kwa kuanza upya kuachana na kila aina ya habari na kuzuia tamaa ya kutaka kufuatilia ili kujua nini kinaendelea.

Rolf anatuambia kama hapa kwenye kusoma kitabu chake, na ukafanyia kazi ushauri mmoja tu aliotoa wa kuachana na habari moja kwa moja bila ya kuwa na huruma. Hilo litakuwa na manufaa makubwa kwako. Lakini kama unataka sababu kwa nini uachane na habari au kama unataka kuwashawishi wengine nao waache habari, basi endelea kusoma ili upate hoja sahihi.

Kwa nini nimechagua kitabu hiki.

Kwa mara ya kwanza nilijifunza kuachana na habari mwaka 2012 na mwaka 2013 nilifanya jaribio la siku 10 kuachana na habari kabisa. Mwanzo ilikuwa vigumu kwa kuwa nilikuwa nimezoea sana habari. Lakini baada ya jaribio hilo niliona ni kitu kinachowezekana na chenye manufaa. Hivyo tangu mwaka huo 2013 sijawa mfuatiliaji wa habari.

Japo kuna kipindi nimekuwa naanguka na kurudi kwenye habari imekuwa mara chache na kwa kipindi kifupi. Lakini mwaka huu 2020 umekuwa mwaka wa tofauti. Nimejikuta napata anguko kubwa la kurudi kufuatilia habari. Na hili lilianza baada ya kusambaa kwa kasi kwa mlipuko wa virusi vya Corona. Katika kufuatilia kujua nini kinaendelea kutokana na virusi hivyo, nikajikuta nimerudi kwenye habari bila kujua. Kila mara kufungua tovuti mbalimbali za habari kujua maambukizi yanaendaje, vifo vingapi na kadhalika.

Mwanzo sikujua haraka kwamba nimerudi kwenye habari, niliona ni sehemu ya kupata taarifa sahihi kuhusu ugonjwa ambao umeisimamisha dunia nzima. Ni mpaka nilipojikuta nikiwa nafuatilia habari hizo mara kwa mara kwa siku, na huku nyingi zikibadilika kwa kasi ndipo niligundua nimeanguka tena kwenye habari.

Ni kawaida yangu ninapokutana na changamoto kwenye maisha kutafuta kitabu kitakachonisaidia kuondoka kwenye changamoto hiyo. Baada ya anguko langu kwenye habari, niliamua kutafuta kitabu cha kunisaidia kuondoa kwenye anguko hilo na kutokurudi tena, ndipo nikakipata hiki cha STOP READING THE NEWS, ni kitabu kizuri mno na nimejifunza mengi.

Katika muongo huu wa 2020 mpaka 2030 ambao nimeutenga kwa kwenda kufanya makubwa sana, sitakwenda kufuatilia habari ya aina yoyote ile, hata kama utakuwa ni mwisho wa dunia, mimi nitaweka muda wangu na nguvu zangu zote kwenye kile nilichochagua kufanya. Najua kama kuna habari muhimu, nitasikia wengine wakizungumzia, na hiyo inatosha.

Mwaka kama huu ambao ni wa uchaguzi, ni rahisi sana kuanguka na kurudi kwenye habari kwa kutaka kujua nini kinaendelea. Lakini sitafanya hivyo. Na kwa kuwa pia situmii mitandao ya kijamii, nitakuwa mbali zaidi na habari kuliko hata kipindi cha nyuma.

Kama umechagua muongo huu uwe wa kufanya makubwa kwako, achana na habari na peleka muda na nguvu zako zote kwenye kile unachotaka kubobea na kufanikiwa sana.

Karibu usome uchambuzi kamili wa kitabu hiki STOP READING THE NEWS ambapo utajifunza sababu 22 kwa nini habari ni mbaya kwako na hatua sahihi za kuachana na habari bila ya kujisikia vibaya.

Kupata uchambuzi kamili wa kitabu hicho pamoja na kitabu chenyewe, karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania kisha bonyeza JOIN CHANNEL.

Usikubali kuendelea kutumiwa na watu wa habari kuwaingizia faida huku maisha yako yakizidi kuwa magumu. Chagua leo kuachana na habari ili uwe na maisha tulivu, yenye furaha na hekima. Karibu usome kitabu cha STOP READING THE NEWS upate maarifa na hatua sahihi za kuchukua.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.