Mtoto mdogo akitaka kitu anakitaka kama anavyotaka yeye, hawezi kukubali kitu kingine isipokuwa kile anachotaka yeye.
Kupata kile anachotaka anaweza kufikiri ni uhuru, lakini huo siyo uhuru. Uhuru siyo kupata kile ambacho mtu anataka kwa namna anayotaka yeye. Huko ni kuendeshwa na hisia au mihemko na siyo kuwa huru.
Uhuru ni kujitambua, kujua siyo kila unachotamani kuwa nacho unapaswa kuwa nacho kweli. Kutambua kwamba hata kama kitu unakihitaji sana, siyo mara zote utakipata kitu hicho kama utakavyo.
Uhuru ni kutambua tabia za kitoto zilizo ndani yetu na kutoruhusu zikuendeshe. Tabia hizi huwa haziondoki kabisa ndani yetu, huwa zinaendelea kuja hasa nyakati ambazo mtu anakuwa na msongo.
Kadiri unavyojitambua ndivyo unavyozijua tabia hizo za kitoto zilizopo ndani yako na kuzizuia. Na kadiri unavyozuia tabia hizo, ndivyo unavyojijengea kujidhibiti na uhuru zaidi.
Kama ambavyo watoto wanapaswa kujengewa mazingira ya kukosa kile wanachotaka, ili wajue kwamba dunia haitoi kile mtu anataka kila wakati, ndivyo pia unavyopaswa kujinyima baadhi ya vitu unavyotaka sana ili uwe imara ndani yako.
Ukizoea kupata kila unachotaka, unaishia kuwa tegemezi kwenye vitu hivyo. Ukikosa kile unachotaka sana na maisha yakaweza kwenda kwa namna nyingine unatambua jinsi gani ulivyo huru.
Chukua mfano wa ajira, watu wengi wanapokuwa wanaanza ajira huwa wanakuwa huru kabisa. Lakini wanavyozidi kukaa kwenye ajira hizi, huku wakipokea mshahara kila mwezi, uhuru wao unapotea kidogo kidogo. Wanazoea mshahara kiasi kwamba anaweza kuchukua mkopo mkubwa na kuulipa kwa mshahara, kwa miaka mingi. Sasa katika kipindi kama hicho ambacho mtu ana deni kubwa linalotegemea mshahara, hawezi kuwa huru kwenye kazi yake. Atajikuta yeye mwenyewe anakosa uhuru, hata kama hakuna anayemwonesha hali hiyo.
Hata kwa vitu ambavyo umevizoea kwenye maisha, kama umeshajiambia huwezi kuishi bila ya vitu hivyo, maana yake haupo huru. Hata maisha yenyewe, kama haupo tayari kuyaacha maisha leo, haupo huru.
Kama ambavyo wanafalsafa wa Ustoa huwa wanasema, unakuwa huru pale unapoweza kukidharau kitu. Na ili uweze kukidharau kitu, lazima ujitambue kweli, lazima ujue nguvu kubwa ipo ndani yako, nguvu ambayo haiwezi kuingiliwa na chochote.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,