Ukiona watu wanakuna kwako na fursa, wanakuonesha fursa inayokufaa sana na kukushawishi ujiunge na fursa hiyo la sivyo utaikosa basi kuwa na uhakika kwenye jambo hili, wewe ni fursa kwa watu hao.
Kama wanachokuambia ni fursa kweli, unafikiri ingekaa muda wote ikusubiri wewe? Unafikiri hao wanaokusisitiza ni fursa wangepoteza muda wao kuja kukushawishi wewe kuhusu fursa hiyo badala ya kujinufaisha na fursa hiyo kwanza?
Kama kuna fursa kweli, kiasi cha watu kuja kukuambia, basi haiwezi kuwa inakusubiri wewe, wengi watakuwa wameshaiona na kuifanyia kazi, hivyo wakati wewe unapata taarifa, unakuwa umeshachelewa.
Fursa ya kweli kwako, ni ile unayoiona mwenyewe, ila unayoona unaweza kufanyia kazi kulingana na uwezo wako na kile unachotaka kwenye maisha yako.
Kwa kifupi fursa sahihi inaanza na wewe mwenyewe, kwa kile unachoona tofauti na wanavyoona watu wengine. Hakuna anayeweza kukusaidia kuona fursa sahihi kwako.
Wengine wanaweza kupendekeza mambo mazuri unayoweza kufanya, wanaweza kukuonesha vitu vinavyoendelea, ila ni wewe pekee unayeweza kuunganisha alama hizo na ukaja na fursa sahihi kwako, ambayo ukiifanyia kazi utafanikiwa.
Na ukishaipata fursa, ifanyie kazi, usipoteze muda wako kuanza kuipigia kelele, maana haitamsaidia mtu mwingine ila wewe, kwa sababu hakuna anayeweza kuona fursa hiyo kwa namna unavyoiona wewe.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,