Tunaweza kusema maendeleo ya binadamu yamekuwa yanazaliwa kutokana na uchoshi (boredom). Pale ambapo mtu anakuwa kwenye hali ya kuboreka, akiwa hana cha kufanya ndipo akili yake inakwenda hatua ya ziada na kumwonesha njia za kukabiliana na chochote anachopitia.
Na uchoshi huo ni ule ambapo mtu anakuwa mpweke, mawazo yake yanakuwa yenyewe na anapata nafasi ya kuota zile ndoto watu wanaita za alinacha. Kuona vitu ambavyo havionekani na kufikiria vitu ambavyo wengi wanaamini haviwezekani.
Hivyo ndivyo watu walivyopata mawazo ya kila aina ya uvumbuzi ambao umetokea duniani.
Lakini sasa tunaishi kwenye zama ambazo hatupati tena nafasi ya kuwa na uchoshi. Muda wote tunatembea na kifaa ambacho kipo tayari kutuondoa kwenye uchoshi.
Simu zetu za mkononi, tunazoziita simu janja (smartphone) zimekuwa kitu kinachotuondoa kwenye kila aina ya uchoshi. Ukijisikia vibaya tu au ukiwa huna cha kufanya, unakimbilia kushika simu yako, kuingia mitandaoni, kuangalia nini kinaendelea.
Unaweza kuona simu ni kifaa kizuri, kifaa kinachokuondoa kwenye uchoshi na kinachokuzuia usijisikie vibaya, lakini ni kifaa chenye madhara. Kwa sababu unapokosa uchoshi, unaondoa ile nguvu ya ubunifu iliyo ndani yako.
Akili yako inapokuwa imetingwa kila mara, hasa na mambo yanayoendelea, haiwezi kupata nafasi ya kuona yale yasiyoonekana na kuweza kuja na ubunifu.
Watu pekee wanaobaki na ubunifu zama hizi, ni wale wanaotafuta njia za kubaki kwenye uchoshi, wale wanaokataa kuchochea akili zao kila mara.
Unapaswa kuwa mmoja wa watu hao, kila siku tenga muda wa kukaa na uchoshi badala ya kuukimbia. Pale unapojikuta una upweke na hujisikii vizuri au huna cha kufanya, usikimbilie kwenye simu au watu wengine. Kaa hapo ulipo, kaa na hali hiyo kwa muda.
Ruhusu mawazo yako yazurure yatakavyo, jipe ruhusa ya kufikiria kila kitu bila ya kujipinga mwenyewe na pata nafasi ya kuangalia matatizo mbalimbali unayopitia.
Ni katika nyakati kama hizo ndipo unapata ubunifu mkubwa, ndiyo unakuja na ugunduzi mpya, ndipo unapata suluhisho la matatizo mbalimbali yaliyokusumbua muda mrefu.
Acha sasa kupoteza nyakati hizo nzuri kwa kusisimua akili yako kwa mambo yasiyo na tija. Tenga muda wa kukaa na uchoshi na utapata manufaa yake.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Dah! Kweli kocha. Nimekuwa naona hili kwenye maisha yangu, pale ninapofika mwisho, pale ninapoona kila nilicuotegemea kimeshindwa kuniletea matokeo mazuri, ndiyo kipindi ambacho nimekuwa napata njia za tofauti za kutatua changamoto zangu. Asante sana kocha kwa hili umeniongezea kitu katika kufanya zoezi hili.
LikeLike
Vizuri.
LikeLike