Kila mmoja wetu ana utofauti na upekee ndani yake,
Lakini ni wachache sana ambao wanaweza kubaki na utofauti waliozaliwa nao.
Wengi hupoteza upekee wao na kujikuta wakiendesha maisha ya kawaida ambayo hayawatofautishi na wengine.
Kitu ambacho kinachangia kuwazuia wasifanikiwe.
Kuna sumu kubwa mbili ambazo zimekuwa zinaua upekee na utofauti ulio ndani ya watu.
Sumu ya kwanza ni mashindano.
Unaposhindana na wengine, unaacha kuwa wewe na unachagua kuwa kama wao.
Hata kama ni watu waliopiga hatua kuliko wewe, kitendo cha kushindana nao, kinakutenga na wewe mwenyewe.
Na hata kama utakuwa umeshinda mashindano hayo, bado unakuwa umeshindwa kwa sababu umeacha kuwa wewe.
Kama ulivyo usemi kwamba hata ukishinda mbio za panya, unabaki kuwa panya, hakuna mashindano yoyote kwenye maisha yanakufanya uwe wewe. Kila mara utakuwa unajilinganisha na wengine.
Sumu ya pili ni ufahari.
Hapa ni pale unapofanya kitu ili uonekane, ili wengine wakusifie.
Hii nayo ni sumu kwa sababu hufanyi kile pekee na muhimu kwako,
Bali unafanya kile ambacho unadhani wengine wanataka ufanye au wakikuona umefanya basi watakusifia na kukukubali.
Huu ni mchezo mwingine ambao hata ukishinda, unakuwa umeshindwa.
Kwa sababu hata kama watu wataona unachofanya, hata kama watakusifia, hawajali.
Kila mtu anapambana na maisha yake, kila mtu anawaza zaidi mambo yake.
Kama usemi unavyoenda, unahangaika kufanya vitu ambavyo hutaki ili kuwaridhisha watu ambao hawajali.
Ushindi wa kweli kwenye maisha ni kukazana kuwa wewe,
Kufanyia kazi utofauti na upekee uliopo ndani yako.
Achana kabisa na mashindano,
Na usifanye chochote ili kuonekana au kusifiwa.
Kuwa wewe, maana wengine tayari wameshachukuliwa.
Kwa kuwa wewe utakuwa na ubunifu mkubwa kwa chochote unachofanya.
Hakuna atakayeweza kukushinda na kukuondoa pale ulipo kama utachagua kuwa wewe.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/07/01/2009
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani