Ipo njia rahisi na ya uhakika ya kushinda mabishano ya aina yoyote ile. Njia hiyo ni kuepuka kuingia kwenye mabishano ya aina yoyote ile. Unaweza kuona ni hoja isiyo na msingi lakini wacha nikueleze kwa kina zaidi ili uweze kuelewa na uokoe muda wako.
Chanzo kikuu cha mabishano ambayo watu huingia, ni kwenye imani na misingi ambayo tayari ipo ndani yao. Watu huwa wanabisha pale wanapokutana na kitu kinachokwenda tofauti na vile wanavyoamini wao.
Hivyo basi, hata ukabishana nao kiasi gani, hakuna atakayebadili imani yake kwa sababu ya hoja ambazo amezipata kwenye mabishano aliyofanya na wengine. Unaweza kumpa mtu hoja zilizo wazi kabisa, lakini hatazisikia wala kuzielewa, kwa sababu imani yake itampa upofu.
Hivyo epuka mabishano, elewa watu wanasimama kwenye upande upi wa kile ambacho wanabishana, kisha taka kujua kwa nini wako upande waliopo.
Jipe muda kusikiliza kwa makini na mtake mtu ajieleze zaidi kutetea upande wake, bila hata ya kumpinga au kueleza upande wako. Kadiri unapompa mtu nafasi ya kujieleza mwenyewe, ndivyo anavyogundua jinsi gani hoja anazotoa hazina mashiko. Lakini wewe usimwoneshe hilo.
Kama unataka watu wabadilike, wape muda na wape nafasi, watabadilika wenyewe kwa kuona kilicho sahihi. Lakini kadiri utakavyokuwa unawalazimisha wabadilike, ndivyo watakavyoendelea kushikilia kile wanachoamini.
Kama kuna kitu watu unataka wakione ambacho kitawasaidia kuona ukweli ni upi, wape nafasi ya kukiona wao wenyewe, kupitia kujieleza kwao, watafika mahali na kuona hoja zao hazitoshelezi, na hapo unaweza kuona nafasi nzuri ya kupendekeza njia mbadala kwa wao.
Epuka mabishano, kuwa msikilizaji na jiweke kwenye viatu vya yule ambaye anaamini tofauti na wewe. Utaona kwa nini ni vigumu kwake kubadilika na hapo utampa nafasi ili aweze kubadilika.
Kumbuka hakuna atakayesikia hoja zako na kusema kuanzia leo nimebadilika, hata kama atashindwa kutetea hoja zake, ataondoka akiwa anashikilia zaidi upande wake kuliko alivyokuwa awali.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana kwa hekima hii
LikeLike
Karibu.
LikeLike