“There should be a science of discontent. People need hard times and oppression to develop psychic muscles.” — Frank Herbert
Moja ya nadharia za mageuzi inasema kiungo cha mwili kinachotumika sana huwa kinakuwa imara huku kile kisichotumika kikiwa dhaifu na hata kupotea kabisa.
Na njia rahisi ya kupima hilo ni mikoni yako, angalia nguvu ya mkono ambao umekuwa unautumia sana na ule ambao hauutumii sana, je mikono hiyo ina nguvu sawa?
Kama huwa unatumia zaidi mkono wa kulia kuliko wa kushoto, mkono huo utakuwa na nguvu zaidi.
Kadhalika kama unatumia zaidi mkono wa kushoto.
Kwenye afya, mtu imara kiafya siyo yule ambaye hajawahi kuumwa kabisa.
Yule ambaye hajawahi kuumwa kabisa ndiye dhaifu zaidi kiafya, na siku akiumwa, hali yake itakuwa mbaya kuliko wale ambao walishaumwa.
Hii ni kwa sababu mwili huwa unatengeneza kinga pale mtu anapoumwa.
Hivyo mtu ambaye amewahi kuumwa, mwili wake umeshajaribiwa na kutengeneza kinga, hivyo akiumwa tena, mwili una nguvu kubwa zaidi ya kupambana.
Mtu ambaye hajawahi kuumwa kabisa mwili wake haujajaribiwa, hivyo haujatengeneza kinga, akija kuumwa, mwili hauwezi kupambana na ndiyo maana hali yake inakuwa mbaya zaidi.
Ukitaka kukuza na kuimarisha misuli ya mwili, unapaswa kufanya mazoezi.
Ukitaka kukuza na kuimarisha misuli ya akili, unapaswa kujifunza vitu vipya.
Je vipi ukitaka kukuza na kuimarisha misuli ya roho/imani, unapaswa kufanya nini?
Siyo kwa maombi wala tahajudi,
Bali kwa kupitia magumu.
Imani zetu zinapimwa pale tunapopitia nyakati ngumu.
Hizo ndizo nyakati zinazotikisa imani zetu hasa na kuondoa kabisa kila aina ya maigizo.
Kile kinachobaki na wewe baada ya kupitia magumu kwenye maisha yako, ndicho unachoamini kweli.
Tumekuwa tunaona hili kwa wengi,
Wakati mambo ni mazuri kwao wanaonekana watu wenye imani ya dini fulani, wakihudhuria ibada, kufanya maombi na kutoa sadaka.
Lakini wakati mambo yanapokuwa magumu kweli kweli, wanaenda kwenye imani za kishirikina.
Watu hao imani yao ya kweli ipo kwenye ushirikina, dini ni maigizo tu.
Lengo kuu la imani ni kukuwezesha kukabiliana na magumu na changamoto unazokutana nazo.
Lakini imani hiyo inajengwa na magumu hayo pia.
Hivyo usiyakimbie wala kuyaogopa,
Jua yanakufanya kuwa imara kiimani, kwa kuijenga misuli ya kiroho.
Chagua kile unachosimamia na kisimamie katika nyakati zote,
Kwenye shida na raha, urahisi na ugumu.
Utavuna matunda yake kupitia maisha tulivu utakayoweza kuwa nayo, bila ya kujali kitu gani unapitia.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu watu wenye hofu, fungua hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/07/10/2018
Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani.