Kila mtu amekuwa anazungumzia umuhimu wa kuanzisha na kukuza biashara, wengi wamekuwa wakionesha ni kitu rahisi ukishakuwa na wazo bora na mtaji unahitaji. Lakini matokeo tunayoyaona ni tofauti, kati ya biashara nyingi mpya zinazoanzishwa, nyingi huishia kufa. Ni chache sana zinazofikia mafanikio makubwa.

Hiki ni kiashiria kwamba, kuanzisha na kukuza biashara siyo jambo rahisi kama wengi wanavyofikiri. Ni rahisi kuangalia biashara chache zilizofanikiwa na kuona ni rahisi, lakini huwezi kuona nyingi zilizokufa.

Ben Horowitz amefanikiwa kuanzia na kukuza makampuni ya teknolojia, katika safari yake amepitia magumu mengi ambayo amekuwa wazi kuyaeleza ili wengine waweze kujifunza. Ben ametushirikisha hayo kupitia kitabu chake kinachoitwa THE HARD THING ABOUT HARD THINGS; Building a Business When There Are No Easy Answers. Kwenye kitabu hiki, Ben ametuonesha ni jinsi gani ilivyo vigumu kuanzisha na kukuza  biashara, na kwa nini biashara nyingi huwa zinakufa. Kupitia yale aliyojifunza, Ben anatushauri yale ya kuzingatia na yale ya kuepuka ili biashara zetu zikue kama tunavyotaka.

the_hard_thing_about_hard_thing.jpg

Kwenye kitabu hiki, Ben anashirikisha uzoefu wake kwenye kuanzisha, kuendesha, kuuza, kununua na kusimamia biashara katika nyakati ngumu na kuifikisha kwenye mafanikio. Mafunzo ambayo Ben anatupa, hayapatikani kwenye shule za biashara, ni uzoefu wake binafsi katika kuanzisha na kukuza biashara.

Baadhi ya mambo magumu ambayo Ben anatushirikisha kwenye kitabu hiki ni;

  1. Kumfukuza kazi au kumshusha cheo rafiki yako ambaye umekuwa naye kwenye biashara kwa muda mrefu.
  2. Kuhusu kutengeneza na kutoa vyeo kwenye biashara yako.
  3. Kama ni sahihi kuajiri wafanyakazi kutoka kwenye biashara ya rafiki yako.
  4. Jinsi ya kujisimamia mwenyewe pale kampuni nzima inapokutegemea.
  5. Hatua za kuchukua pale unapokuwa na wafanyakazi wenye uwezo mkubwa, lakini hawana ushirikiano mzuri na wengine.
  6. Wakati gani wa kuuza biashara yako na jinsi ya kufanya hivyo.
  7. Jinsi ya kuajiri, kupandisha vyeo na kufukuza wafanyakazi.

Hayo na mengine magumu ambayo watu hukutana nayo kwenye biashara lakini hayafundishwi, Ben ametushirikisha kwa kina kutoka kwenye kitabu chake.

Kuhusu mwandishi.

Ben Horowitz ni mwanzilishi mwenza na mbia katika taasisi ya uwekezaji inayoitwa Andreessen Horowitz. Taasisi hii inawekeza kwenye makampuni machanga ya teknolojia.

Ben alikuwa mwanzilishi mwenza na mkurugenzi wa kampuni ya Opsware (zamani ilijulikana kama Loudcloud), ambayo aliweza kuikuza na kuivusha katika nyakati ngumu na hatimaye kununuliwa na kampuni ya HP mwaka 2007 kwa thamani ya dola bilioni 1.6.

Ben amefanya kazi kwenye makampuni makubwa ya teknolojia kama HP, AOL, na Netscape. Kupitia makampuni hayo makubwa na yale aliyoanzisha, Ben amejifunza mambo mengi kuhusu biashara kuliko alivyowahi kujifunza shuleni.

Ben ni mjumbe wa bodi kwenye makampuni ambayo taasisi yao ya uwekezaji ya Andreessen Horowitz imewekeza, baadhi ya makampuni hayo ni: Caffeine, Databricks, Foursquare, Genius, Magnet Systems, Medium, NationBuilder, Okta, Sisu, Tanium, TripActions, United Masters, na Usermind.

Kutoka kwa Ben.

Ujumbe mfupi kutoka kwa Ben ni huu;

“Kila mara ninaposoma vitabu vya biashara na mafanikio huwa najiambia, ni vizuri, lakini hicho siyo kilicho kigumu zaidi.

Ni rahisi kuwa na malengo makubwa, lakini siyo rahisi kupunguza watu kazi pale unaposhindwa kufikia lengo.

Ni rahisi kuajiri watu bora, lakini ugumu unakuja pale watu hao wanapoona bila wao huwezi na kutaka uwape kile wanachotaka, hata kama huwezi.

Ni rahisi kutengeneza chati ya usimamizi kwenye biashara, lakini siyo rahisi kuwawezesha watu kuwasiliana ndani ya chati hiyo kama ulivyopanga.

Ni rahisi kuwa na ndoto kubwa, lakini ugumu unakuja pale unaposhtuka usiku na kuona ndoto hiyo ni kama jinamizi.

“Changamoto ya vitabu vingi vya biashara na mafanikio ni kutoa majibu mepesi kwa changamoto ambazo hazina majibu. Hakuna kanuni ya kutatua changamoto ambazo zinabadilika. Hakuna kanuni ya kuanzisha na kukuza biashara au kufikia mafanikio ambayo inaweza kufanya kazi kwa watu wote na kwa nyakati zote. Na hilo ndiyo jambo gumu kuhusu mambo magumu, hakuna kanuni ya kukabiliana nayo.

“Kuna ushauri na uzoefu ambao unaweza kuwasaidia watu kukabiliana na mambo magumu. Kwenye kitabu hiki siendi kukupa kanuni ya kufanikiwa, bali nakushirikisha hadithi yangu, kwa yale niliyopitia kama mjasiriamali, mkurugenzi na mwekezaji. Nimejifunza mambo haya kwa uzoefu na ninayaona kwa wengine, hali zinaweza kutofautiana, lakini mambo huwa hayatofautiani sana.”

Karibu kwenye uchambuzi.

Uchambuzi wa kitabu hiki utakuwa na sehemu sita kulingana na sura zilizopo kwenye kitabu. Sura fupi na zinazoendana zimewekwa pamoja kama sura ya kwanza mpaka ya tatu, kisha sura nyingine ambazo zinajitegemea na ni ndefu, zimefanywa kuwa sehemu inayojitegemea.

Sehemu ya kwanza tutaona historia ya Ben kwa ufupi, ambapo tutaona alivyotoka kwenye ukomunisti mpaka ubepari.

Sehemu ya pili tutajifunza hatua za kuchukua pale mambo yanapokwenda mrama, hapa ni pale mambo yanapokuwa magumu.

Sehemu ya tatu tunajifunza kipaumbele sahihi cha watu, bidhaa na faida katika kukuza kampuni yako. Hicho ndiyo kipaumbele sahihi unachopaswa kufuata.

Sehemu ya nne tunajifunza hatua za kuchukua kuhusu mambo yanayoendelea kwenye biashara, haya ni mambo yanayotokana na shughuli za kila siku kwenye biashara.

Sehemu ya tano tutajifunza jinsi ya kuongoza hata kama hujui unakoenda, kama mkurugenzi mtendaji wa kampuni yako, hupaswi kuonesha wasiwasi kwa wafanyakazi wako hata kama hujui unakokwenda.

Sehemu ya sita tutajifunza sheria ya kwanza ya ujasiriamali ambayo ni hakuna sheria, hapa tutajua hatua muhimu za kuchukua mfano kama uuze kampuni yako au la.

Karibu kwenye uchambuzi tujifunze, siyo kanuni za mafanikio, bali uzoefu ambao utatuonesha kipi cha kuzingatia na kipi cha kuepuka katika kuanzisha na kujenga kampuni yenye mafanikio makubwa.

Kupata uchambuzi kamili wa kitabu hiki pamoja na vitabu vingine vizuri karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania kisha bonyeza JOIN CHANNEL.

Usikubali kuendelea kuwa kwenye hatari ya biashara yako kushindwa, njoo tujifunze hatua sahihi za kuchukua ili kuweza kuvuka nyakati ngumu kwenye biashara yako.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.