Kila mtu anajua ni nini anataka kwenye maisha yake, hata kama hana uhakika sana.
Kila mtu ana picha ya jinsi angependa maisha yake yawe, nini angefanya na maisha yake yangeendaje kama angekuwa na uhuru wa kuchagua kuyaishi maisha hayo.
Lakini wengi hawana maisha wanayoyataka, siyo kwa sababu hawawezi kuwa nayo, bali kwa sababu wanaponzwa na wale wanaowazunguka.
Ili wakubalike na wale wanaowazunguka, wanalazimika kufanya kile kinachowapendeza wengi na siyo kilicho sahihi kwao.
Kinachotokea ni kunakuwa na jamii yenye watu wengi ambao hawana maisha yao, bali wanaishi maisha ya kuwafurahisha wengine, huku nao wakiwazuia wengine wasiishi maisha yao.
Kitu kimoja unapaswa kujua ni kwamba jamii haitaki uwe huru, haitaki uchague kuishi maisha yako kama unavyopanga. Kwa sababu inajua ukiwa huru hutatawalika, hutatishika na hivyo jamii haiwezi kukutumia itakavyo.
Hivyo inakazana kujenga kile inaita maisha ya kawaida, na kukuambia watu kama wewe wanapaswa kuishije. Watu wenye elimu kama yako, kazi kama yako na biashara yako wanapaswa kuishije, wanapaswa kuishi kwenye nyumba za aina gani, kuwa na starehe za aina gani na kadhalika.
Kama unataka kuwa huru, hatua ya kwanza unapaswa kuachana kabisa na jamii, kupuuza kabisa kila ambacho mtu anakuambia unapaswa kuwa au kufanya. Kuchagua yale maisha yenye maana kwako, yaliyo sahihi kwako na kuyaishi.
Kufanya hivyo haitawafurahisha wengi, lakini itakuridhisha wewe, na hilo linatosha. Uzuri pia ni kwamba ukionesha msimamo kwenye kuyaishi maisha yako, utapata matokeo bora na makubwa kuliko ya wengine na mwisho utageuka kuwa shujaa kwa kila mtu.
Hakuna shujaa yeyote ambaye alikubali kuishi kama jamii ilivyomtaka aishi, hakuna aliyewahi kupata mafanikio makubwa kwa kumsikiza kila mtu. Watu hao walimsikiliza mtu mmoja tu, wao wenyewe, walisikiliza nafsi zao na hilo liliwapa utofauti mkubwa kwenye jamii.
Unachopaswa kujua ni kwamba huwezi kuwaridhisha watu wote, hata ungefanya maamuzi gani, kuna ambao wataona ni mazuri na wengine wataona ni mabaya. Hivyo kama jiridhishe wewe mwenyewe, fanya kile ambacho baadaye hutajutia na hilo linakutosha wewe.
Epuka maoni ya wengi kama sumu, kila mtu huwa ana maoni na kila mtu anaamini maoni yake ni sahihi. Unachohitaji ni kujifunza misingi sahihi na siyo kubeba kila aina ya maoni. Kama unataka kujifunza kwa wengine, basi angalau angalia wale waliofanya na siyo wanaosema tu. Epuka pia ushauri wa wengi, hasa ule ambao hujaomba, wengi wanaokushauri kwa kuangalia juu juu hawajui hasa unakabiliana na nini.
Mafanikio makubwa wanayapata wachache kwa sababu hao ndiyo wenye uthubutu wa kuipuuza jamii na kufanya yao, wasioogopa maneno makali ya wengine na wasioangalia kundi linafanya nini. Watu hao wako tayari kushindwa wakipambana wenyewe hata kama watachekwa, kuliko kujificha ndani ya kundi.
Fanya kile kilicho sahihi kwako, na siyo kitakachowafurahisha wengi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,