Kitu kimoja ambacho sisi binadamu tunakipenda sana ni uhakika. Huwa tunafanya kile ambacho tuna uhakika nacho, tunajua matokeo tunayokwenda kupata, hata kama siyo matokeo tunayoyapenda.

Ukitaka kumtawala mtu, mpe uhakika, hapo atakuwa tayari kukubaliana na wewe. Hivyo ndivyo ajira zinavyowashikilia wengi, kwa kuwa mshahara ni wa uhakika, hata kama ni mdogo, basi mtu atakuwa tayari kufanya kazi.

Hata kama juhudi hizo hizo anazoweka kwenye kazi zingeweza kumpa kipato zaidi kwa kufanya biashara au kujiajiri mwenyewe, hafanyi hivyo kwa sababu huko hakuna uhakika ambao anapenda kuutegemea.

Kubadilika maana yake ni kuacha kufanya kile chenye uhakika na kujaribu kile ambacho mtu huna uhakika nacho. Hilo ni gumu na ndiyo linalopelekea mabadiliko kuwa magumu kwa walio wengi.

Kwa kujua hili, litakusaidia kwenye kutengeneza mabadiliko kwa namna ambayo itakuwa rahisi kwako. Kwa kuanza kujijengea uhakika ambao hautakuteteresha kwenye kile unachotaka kujaribu.

Moja ya maandalizi unayoweza kufanya ni kuhakikisha hata kama mabadiliko unayokwenda kufanya yatashindikana, basi huanguki kabisa.

Pia kujiandaa kwa maumivu makali yanayoletwa na mabadiliko inasaidia. Wengi wamekuwa wanadanganywa kwamba mabadiliko ni rahisi, hivyo wanapofanya mabadiliko na kukutana na ugumu wanaona hawajafanya kwa usahihi na hivyo kuacha. Lakini unapoanza ukijua mabadiliko ni magumu, yana changamoto na maumivu, unapokutana na vitu hivyo haikushangazi wala kukutisha, unajua uko kwenye njia sahihi.

Mabadiliko ni magumu zaidi kwa sababu wale wanaokuzunguka hawatakuachia kirahisi ubadilike. Watakuwa kikwazo kwako kubadilika, kwa sababu mabadiliko yako yatawaathiri na wao pia. Hivyo lazima uwe tayari kukabiliana nao na kuhakikisha hawakurudishi nyuma.

Wale ambao mabadiliko yako yanalenga kwasaidia pia hawatayakubali kirahisi, wengi wameshazoea maisha yao ya awali, kile kipya unachowaletea hawawezi kukielewa haraka. Hivyo unahitaji uvumilivu mkubwa unapokuja na kitu kipya, watu hawatakikubali haraka, itachukua muda kwa watu kukipokea, kwa kuanza na wachache walio tayari kujaribu, kisha wengine kuona hao wachache wakinufaika na wao kuwa tayari kubadilika ili wanufaike.

Unapofanya kitu cha tofauti, lazima ujiandae kwa haya; maumivu kwako binafsi, kuzuiwa na wale wanaokuzunguka na kutokueleweka na wale unaowalenga. Kwa kuelewa uhalisia wa ugumu wa mabadiliko, kutakufanya ujiandae vyema na pia uwe na uvumilivu unaohitajika ili kukamilisha mabadiliko hayo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha