“Walioshindwa wanajua kila kitu, waliofanikiwa hawajui chochote.” Hicho ndiyo kitu kikubwa ambacho nimeweza kujifunza katika miaka ambayo nimekuwa najifunza kuhusu mafanikio, kutoka kwa wale waliofanikiwa na walioshindwa.
Na hilo utaliona wazi kwenye kujifunza, kuna vitabu vingi mno vyenye maarifa mazuri ambayo yanaweza kumsaidia mtu kupiga hatua kwenye maisha, kutoka pale alipokwama na kutatua changamoto mbalimbali kwenye maisha yake.
Lakini wale walioshindwa siyo wasomaji wa vitabu, waambie wasome vitabu na watakuambia hakuna kipya cha kujifunza kwenye vitabu hivyo, mambo ni yale yale. Wanarudi kufanya yale ambayo wamezoa kufanya ambayo hayawapi mafanikio yoyote.
Wale waliofanikiwa wapo tayari kujifunza kila wakati, wakikutana na kitabu chochote wanakipata na kukisoma, hata mara moja hawajiambii tayari wanajua na hakuna cha kujifunza. Utayari huo wa kujifunza unawapa maarifa ya kupiga hatua zaidi.
Waliofanikiwa wana maktaba majumbani mwao, huku wakiwa na tv ndogo au hawana tv kabisa. Walioshindwa huwa hawana maktaba kabisa majumbani mwao, huku wakiwa na tv kubwa.
Waliofanikiwa huwa hawakosi muda wa kujifunza, wapo tayari kupunguza mambo mengine ila wapate muda wa kujifunza. Walioshindwa wana muda wa kufanya kila kitu ila siyo kujifunza. Wana muda wa kuperuzi mitandao, kufuatilia habari, kufuatilia maisha ya wengine, lakini kujifunza, hawana muda huo.
Haiwezi kufanya kazi kwangu.
Moja ya vitu vinavyowafanya walioshindwa wasiwe tayari kujifunza ni kukosa imani kwenye kujifunza.
Wengi wameshakata tamaa kiasi kwamba hawaamini kama kujifunza kunaweza kuwasaidia.
Wengi wanaposikia kitu kipya wamekuwa wanajiambia hiyo inaweza kufanya kazi kwa wengine, lakini haiwezi kufanya kazi kwangu.
Hata wakisikia hadithi za wale waliofanikiwa, watatafuta kitu cha kuwaaminisha kwamba watu hao wamepata bahati fulani ambayo wao hawawezi kuipata.
Wakishajiridhisha hivyo, wanaendelea na maisha yao ya kushindwa, huku wakiwa hawapigi hatua yoyote.
Hata wanapowaona wale waliofanikiwa wakijaribu vitu fulani, huamini kwamba vitu hivyo vinawezekana kwa watu hao, lakini haviwezekani kwao.
Hutoa kila aina ya sababu kwa nini ni vigumu kwao kufanya hivyo, wengine wapo tayari kulaumu hata mambo ambayo wazazi wao walifanya miaka mingi iliyopita.
Unafurahia matokeo unayoyapata?
Rafiki, moja ya vitu nilivyojifunza kwenye maisha ni hiki; kwenye mambo yanayonihusu nakuwa mhafidhina (conservative) ila mambo yanayowahusu wengine nakuwa huria (liberal).
Hivyo mtu anaponiambia kwamba kujifunza hakuwezi kufanya kazi kwake, au kanuni mbalimbali za mafanikio ninazoshirikisha haziwezi kufanya kazi kwake, huwa sibishani naye.
Anajua mengi kuhusu maisha yake kuliko ninavyojua mimi, hivyo siwezi kumkatalia mtu kile ambacho anaamini. Kila mtu yuko huru kuchagua aina gani ya maisha aishi, kama tu haingilii maisha ya wengine.
Lakini kuna swali ambalo nimekuwa nawauliza watu hao, je unafurahia matokeo unayoyapata sasa?
Labda ni kweli yale wanayofanya wengine wakafanikiwa kwako hayawezi kufanya kazi, lakini je unafurahia matokeo unayoyapata sasa? Je yale unayofanya wewe yanakupa matokeo sahihi?
Kama jibu ni sahihi, kwamba unafurahia matokeo unayoyapata, hulalamiki wala kuumizwa na chochote, basi nikutie moyo, endelea kufanya chochote unachofanya sasa, maana hicho ni sahihi kwako.
Lakini kama hufurahii matokeo unayoyapata, kama unalalamika au kuumia kwa namna maisha yako yanavyokwenda, hapo kuna tatizo. Na hapo siwezi kukubaliana na wewe.
Kwa nini usijaribu kitu kipya?
Ipo kauli maarufu kwamba ujinga ni kufanya jambo lile lile, kwa namna ile ile halafu kutegemea kupata matokeo ya tofauti. Sisemi wewe ni mjinga, lakini kama umefanya kazi au biashara kwa zaidi ya miaka 10 na hakuna hatua unapiga, unafikiri nini kitabadilika kama unaendelea hivyo?
Kama kile unachofanya sasa hakikupi matokeo yanayoridhisha, kama hufurahii matokeo unayopata sasa, kwa nini usijaribu kitu kipya?
Kwa nini usiweke ujuaji wako pembeni na kujaribu yale ambayo waliofanikiwa wamefanya na wakafanikiwa?
Hata kama umekuwa unaamini kwamba hayawezi kufanya kazi kwako, kwa nini usiweke imani hiyo pembeni kwa muda tu na ukachagua vitu vipya vya kufanyia kazi na kujipa muda wa kujifanyia tathmini?
Kwa miaka mingi umekuwa unaenda unavyoenda na umefika hapo ulipo sasa, kuna ubaya gani ukatenga mwaka mmoja na kwenda tofauti kidogo, kisha kufanya tathmini?
Kama baada ya mwaka mmoja utakuwa huna tofauti na ulivyokuwa awali, basi unaweza kurudi kwenye maisha uliyokuwa unafanya awali. Lakini kama utakuwa na matokeo mazuri, basi uendelee na maisha bora.
Kwa uzoefu ambao nimekuwa nao kwenye eneo hili, ukifanya jaribio hilo la mwaka mmoja, hata kama hutapiga hatua kubwa, hutakuwa tayari kurudi kwenye maisha ya awali, maana utaona jinsi yalivyokuwa yanakukwamisha.
Jaribio la mwaka mmoja.
Kwa mwaka mmoja kuanzia sasa, napendekeza ufanye jaribio hili, fanya kila ninachopendekeza hapa bila ya kuacha hata kimoja, kisha baada ya mwaka fanya tathmini. Iwapo matokeo yatakuwa mazuri endelea, kama siyo mazuri rudi kwenye ulichozoea awali.
Mambo ya kufanya kwenye jaribio hili;
- Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kama bado hujawa mwanachama. Kwa kuwa ndani ya KISIMA CHA MAARIFA unapata mafunzo na miongozo sahihi ya kukuwezesha kupiga hatua. Kwa kulipa ada ya mwaka, una uhakika wa kujifunza kwa mwaka mzima. Kujiunga na KISIMA tuma ujumbe kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253.
- Anza kuamka mapema zaidi ya ulivyozoea kuamka, amka saa moja mapema zaidi ya ulivyozoea. Saa hiyo moja unayoamka mapema itenge na kuilinda kuwa saa yako ya nguvu, saa moja kwa ajili ya maendeleo yako binafsi.
- Kwenye saa yako moja kila siku, fanya vitu hivi vitatu, soma, tahajudi/tafakari na fanya mazoezi. Tenda dakika 20 kwa kila jambo hapo, soma kitabu kwa dakika 20 na ondoka na kitu cha kufanyia kazi. Fanya tahajudi au tafakari ya maisha yako kwa dakika 20, pamoja na kupangilia na kupitia siku yako kwenye muda huo. Na fanya mazoezi ya mwili kwa dakika 20, iwe utaruka kamba, utakimbia, pushup au mengineyo. Hii ni njia bora sana ya kuianza siku yako.
- Unapofanya kazi, weka umakini wako wote kwenye kazi yako, tenga muda ambao hukubali usumbufu kabisa. Kwenye kufanya kazi zako, mara zote jaribu vitu vipya na kuwa mbunifu, huku pia ukienda hatua ya ziada, ukifanya zaidi ya ulivyozoea kufanya. Weka moyo wako wote na akili zako zote kwenye chochote unachofanya, na utaweza kukifanya kwa ubora wa hali ya juu.
- Kwa kila fedha inayopita kwenye mikono yako, haijalishi ni kiasi gani, asilimia 10 ya fedha hiyo iweke pembeni. Hiyo umejilipa wewe mwenyewe na hutaitumia kwa matumizi ya aina yoyote. Kuwa na akaunti maalumu ya benki, ambayo unaweza kuweka fedha lakini huwezi kutoa. Kisha asilimia hizo 10 ziweke kwenye akaunti hiyo, kwa mwaka mzima bila kuzitoa.
- Jiondoe kwenye mitandao yote ya kijamii ambayo haina manufaa kwako. Na manufaa ya kuzingatia ni fedha, kama hulipwi kwa kutumia mitandao hiyo, achana nayo mara moja. Kwa mitandao itakayokuwa na manufaa kwako, yaani inayokuingizia kipato moja kwa moja, tengeneza ratiba yako ya siku ni muda gani utaitembelea. Usikubali kila wakati ukawa unasumbuliwa na mitandao hiyo.
- Acha kufuatilia habari ya aina yoyote ile. Kwa mwaka huo mmoja achana na habari zote kabisa, kila muda wa ziada unaoupata kwa kuondoka kwenye mitandao na kuachana na habari uwekeze kwenye kusoma zaidi vitabu. Jiwekee lengo la kusoma angalau kitabu kimoja kila mwezi na uchambuzi mmoja wa kitabu kila wiki. Kupata vitabu na chambuzi jiunge na SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua; www.t.me/somavitabutanzania
- Acha kukimbizana na fursa mpya kila wakati. Kwa miaka yote ambayo umekuwa unahangaika na kila fursa mpya unayosikia imeingia umefika wapi? Katika mwaka huu mmoja wa majaribio acha kabisa kukimbizana na fursa mpya. Chagua vitu vichache utakavyofanya na fanya hivyo. Kama unafanya biashara basi kwa mwaka huu mmoja utaweka juhudi kwenye biashara hiyo tu, kuikuza zaidi kwa kuwafikia wateja wengi zaidi na kutoa bidhaa huduma zaidi ya unazotoa sasa. Kama umeajiriwa, chagua biashara moja utakayoifanya katika kipindi hiki, kisha fanya hiyo tu. Ukishaamua hivyo, usiyumbishwe na fursa yoyote mpya inayokuja mbele yako. Fanya kile ulichopanga na fursa zinazohusiana nacho.
- Fanya usafi wa maisha yako. Kuna mazingira mengi umeyatengeneza kwenye maisha yako katika kipindi chote ambacho umekuwa unaishi kwa mazoea. Na hayo yamekuwa kikwazo kwako, usipofanya usafi muhimu, mazingira hayo yatakuzuia kufanya jaribio hili la mwaka mmoja. Moja anza usafi kwenye mahusiano, kuna ndugu, jamaa na marafiki ambao ukiendelea kuwa nao watakukatisha tamaa na kukurudisha nyuma, hawa achana nao kwa muda. Eneo jingine la kufanya usafi ni anasa ambazo umezoea kufanya, kama umekuwa mnywaji wa pombe au mfuatiliaji wa michezo mbalimbali, chagua kuachana na vitu hivyo kwenye mwaka huu wa majaribio. Kila muda ulionao unahitaji kuuwekeza kwenye kujifunza na kufanya vitu vipya, hivyo hupaswi kupoteza kwa namna yoyote ile.
- Soma vitabu hivi viwili; ELIMU YA MSINGI YA FEDHA na TANO ZA MAJUMA 50 YA MWAKA. Kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA kitakupa msingi muhimu sana wa kujijenga kifedha katika kipindi hiki cha jaribio la mwaka mmoja. Utaweza kuondoka kwenye madeni, kuweka akiba na kuwekeza. Kitabu cha TANO ZA MAJUMA 50 YA MWAKA ndiyo biblia ya mafanikio kwako, ni kitabu kikubwa kilichosheheni maarifa ya kila aina kuhusu mafanikio. Kina siri 50 za mafanikio, uchambuzi wa vitabu 50 na mengine mengi. Ni kitabu ambacho utakisoma kwa mwaka mzima. Kupata vitabu hivyo wasiliana na namba hizi; 0752 977 170 au 0678 977 007, utaletewa au kutumiwa popote ulipo Tanzania.
- Kuwa na msimamo. Jaribio hili halitakuwa rahisi, mengi hapo ni mambo mapya kwako, hivyo unahitaji kujisukuma ili kuyafanya. Wanaokuzunguka watakuambia umebadilika, unawatenga, usipokuwa na msimamo hutaweza kufanya mambo hayo hata kwa wiki moja. Jiambie una mwaka mmoja tu wa kufanya jaribio hilo, siyo kwamba maisha yako yataenda milele hivyo, kama hutafurahia hali hiyo, utabadili baada ya muda. Kama unaona mwaka ni kitu kirefu, hesabu kwa kupunguza kila siku, siku ya kwanza jiambie una siku 365 zimebaki, siku ya pili, 365 na kuendelea. Kadiri siku zinavyopungua ndivyo unakuwa na matumaini kwamba jaribio halidumu milele.
Rafiki yangu mpendwa, hilo ndiyo jaribio napendekeza ulifanye. Kama kuna mambo umesoma hapo na kujiambia hayawezi kufanya kazi kwako, nirudie kukuuliza, je matokeo unayopata sasa unayafurahia? Kama ndiyo usingesoma mpaka hapa, kusoma mpaka hapa ni kiashiria kwamba matokeo unayopata hayakuridhishi. Sasa kwa nini usiweke ubishi wako pembeni na kujaribu hili kwa mwaka mmoja?
Kama umechagua kufanya jaribio hili, karibu twende pamoja kwenye KISIMA CHA MAARIFA, na utakwenda kuwa mwaka wa kipekee sana kwako. Kama bado hujawa mwanachama, tuma ujumbe sasa kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA na utapata maelekezo ya kujiunga.
Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania