“The less you speak, the more you will work.” – Leo Tolstoy

Kuna sheria moja ya siri ambayo wawekezaji wakubwa wamekuwa wanaitumia.
Sheria hiyo ni kwamba ukimuona mkurugenzi mkuu (CEO) au mwanzilishi (Founder) wa kampuni anaonekana akiongea sana kwenye vyombo vya habari, ni wakati wa kuondoa uwekezaji wako kwenye kampuni yake.
Kwa yeye kutumia muda mwingi kwenye kuongea, maana yake hatumii muda huo kwenye kufanya kazi, na hicho ni kiashiria kwamba kampuni ina matatizo au inakwenda kwenye matatizo.
Sheria hiyo inaweza isiwe sahihi mara zote, lakini kwa kuitumia imekuwa inawasaidia wasipoteze uwekezaji wao.

Kuna misemo mingi ya kiswahili ya kueleza hali hiyo;
👉🏼Debe tupu haliachi kuvuma,
👉🏼Ngoma ikilia sana ujue inapasuka.
Yote hii inaeleza kitu kimoja, yeyote anayeongea sana, hakuna kazi kubwa anayofanya.
Jiwekee sheria hii kwako na kwa wengine.
Kwako; Ongea kidogo, fanya zaidi,
Kwa wengine; ukikutana na anayeongea sana, jitahadhari.

Mwendelezo wa sheria hii ni kwenye matumizi ya mitandao ya kijamii.
Kadiri mtu alivyo bize kwenye mitandao ya kijamii, ndivyo ambavyo hafanyi kazi.
Kama mtu anapost kila muda kwenye mitandao hiyo, kama anabishana na kila mtu kwenye kitandao hiyo, jua kabisa mtu huyo hafanyi kazi kubwa.
Maana angekuwa na kazi inayomtinga kufanya, asingekuwa na muda wa kupost kila mara au kubishana na watu mitandaoni.
Hivyo sheria nyingine itakayokusaidia ni hii; kama mtu yupo bize sana mitandaoni, hakuna kazi kubwa anayoifanya.

Muda wetu una ukomo,
Nguvu zetu zinapungua haraka kwenye siku,
Na mambo ya kufanya ni mengi na yanahitaji umakini wako mkubwa.
Haiwezekani ukaweza kugawa muda na nguvu zako kwenye kufanya kazi yenye maana na wakati huo huo ukawa unaongea sana au kupost sana mitandaoni. Haiwezekani.
Hivyo chagua maneno kidogo na kazi zaidi au maneno zaidi na kazi kidogo, huwezi kufanya vyote viwili kwa pamoja.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu kilicho sahihi kwako kufanya, fungua; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/07/15/2023

Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani,