Najua kila mtu ana matatizo mengi kwenye maisha yake, ambayo anakabiliana nayo kila siku. Lakini sehemu kubwa ya matatizo hayo huwa ni ya kutengeneza. Ndiyo umesoma vizuri hapo, kuna matatizo mengi umekuwa unayatengeneza wewe mwenyewe.
Iko hivi rafiki, sisi binadamu tumeumbwa kwa asili kuangalia nini hakipo sawa. Hivyo hata tukiwa kwenye chumba ambacho ni tulivu na kina usalama wa kutosha, bado tutakuwa tunajiuliza hivi moto ukitokea hapa nitatokea wapi au kufikiria mambo mengine yanayoendelea kwenye maisha yako.
Ndivyo tulivyo, hatuwezi kukaa na kuangalia mazuri muda wote, mara kwa mara tutajikuta tukisumbuka na yale ambayo ni mabaya, hata kama bado hayajatokea.
Hivyo basi, kwa kuwa hakuna wakati utakuwa bila ya matatizo, chagua kitu kikubwa utakachokifanyia kazi. Chagua kitu kitakachokupa matatizo ya kweli badala ya matatizo ya kutengeneza.
Unaweza kufanya hivyo kwa kujiwekea malengo makubwa, ambayo yanakusukuma kuyafikiria na kuyafanyia kazi muda wote. Kwa malengo hayo makubwa, hupati muda wa kuhangaika na matatizo ya kutengeneza, maana una matatizo halisi yanayoendelea kwenye maisha yako ambayo yanahitaji umakini wako.
Mikasa (drama) ya maisha huwa haiishi, ukimaliza moja linakuja jingine, na kama huna matatizo makubwa, basi matatizo madogo madogo ndiyo yatakayokusumbua zaidi.
Ni wakati sasa wa kuwekeza nguvu zako kwa usahihi, kutokuruhusu zipotee kwa matatizo ya kutengeneza na kuzipeleka kwenye matatizo halisi ambayo yana manufaa kwako.
Badala ya kuamka na kuimaliza siku yako ukihofia habari unazosikia au kuonea wivu maisha ya wengine kwa jinsi wanavyoonekana mitandaoni (yote hayo ni matatizo ya kutengeneza), amka ukiwa na hamasa ya kwenda kupiga hatua kubwa kufikia lengo ulilojiwekea.
Upo usemi kwamba ukuu wa mtu unapimwa kwa matatizo yaliyomtinga. Hebu anza kupima ukuu wako kwa kuorodhesha ni matatizo gani yanayokusonga sasa. Kama matatizo yanayokusumbua ni vitu vidogo vidogo basi tambua hutafikia ukuu kwenye maisha yako. Na hapo chukua hatua ya kujiwekea malengo makubwa ambayo yatazalisha matatizo makubwa yatakayokutinga na kukuondoa kwenye mambo hayo madogo madogo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Shukrani kocha kwa ukurasa huu umenena ukweli.
Mungu ukubariki zaidi kwa maarifa unayotupa yameweza kunifikisha hatua nyingine
LikeLike
Vizuri Mwijage.
LikeLike