Mpendwa rafiki yangu,
Kila mmoja wetu anaingia katika ndoa akiwa tayari na matarajio yake binafsi. Na shida nyingi huwa zinaanza kuzaliwa ni pale mtu anapokuwa ameingia kwenye ndoa halafu huku akiwa na gia ya kukutana na kitu fulani katika ndoa yake halafu anakikosa na hapo ndipo changamoto zinapoibuka.
Hebu pata picha kidogo, enzi unasoma au hata sasa hivi kwenye baadhi ya taasisi huwa wanatoa chakula kwa wafanyakazi wake na mara nyingi huwa kuna kuwa na ratiba za chakula, kila siku ina siku yake.
Kwa mfano, mwanafunzi anayesoma shule ya bweni siku ya ratiba ya kula wali halafu ukaja kumwekea makande atakuelewa kweli? Yaani mtu anajua kabisa kila jumamosi ni siku ya wali na nyama au maharage halafu anaenda eneo la chakula anakutana na makande hebu pata picha kidogo atajisikiaje kisaikolojia? Na hivyo ndivyo ilivyo kwa wanandoa wengi wanazianza ndoa zao kwa shauku kubwa huku wakitarajia wanakwenda kukutana na kile wanachotaka mara wanapofika wanakutana na kile ambacho hawakutegemea kukikuta
Je unavumilia maisha ya ndoa au unayafurahia? Hili ni swali ambalo lilinisukuma kuandika kitabu cha Ijue Njaa Ya Wanandoa, usipojua ndoa yako ina njaa gani huwezi kuitatua njaa ya ndoa yako na uzuri ni kwamba kila mmoja anapoingia kwenye ndoa anakua na njaa yake na anategemea ashibishwe na mwenza wake na majibu sahihi juu ya ndoa yako yanapatikana kupitia kitabu hiko cha Ijue Njaa Ya Wanandoa.
Baada ya kupata utangulizi huo, turudi sasa katika shabaha ya makala yetu ya leo.
Hivi kwa akili ya kawaida tu unafikiri shetani anayeiharibu ndoa yako ni nani?
Watu wengi wamekuwa wanamsingizia shetani kila kitu, kila jambo ambalo anaona haliendi vizuri katika ndoa yake basi anakimbilia kusema ni shetani kumbe basi, muda mwingine ushetani huwa wanazalisha wanandoa wenyewe, usipotimiza majukumu yako ipasavyo lazima utaona kila matokeo hasi unayopata utaona ni shetani.
Lakini, yuko shetani wa karne 21 anayezitafuna ndoa nyingi ambaye siyo mwingine bali ni ubinafsi.
Asili ya ndoa ni umoja, hata mwasisi wa ndoa hakuwa na lengo la ubinafsi bali umoja na watu wanapokuwa katika ubinafsi ndani ya ndoa mambo mengi yanakua hayaendi.
Ndoa yeyote ambayo ina umoja lazima itafanikiwa na kubarikiwa na ninamini hilo bila shaka. Ukiishi kwa misingi sahihi ya ndoa yako lazima ndoa yako itastawi vizuri sana.
Nioneshe hata taasisi moja ya ndoa ambayo ina ubinafsi iliyofanikiwa na Mimi nitakuonesha taasisi yenye umoja iliyofanikiwa. Kwenye umoja ushindi lazima utapatikana kwa sababu fokasi yenu inakuwa ni moja na kipaumbele chenu kinakuwa kimoja kwanin sas kama mnashirikiana msifanikiwe?
Wako wanandoa hawajawahi kuonja ladha ya ndoa kwa sababu ya ubinafsi. Ziko ndoa ambazo zinashindwa kupiga hatua kwa sababu ya kutokua na umoja kila mmoja ni mbinafsi anajali maslahi yake binafsi.
Asili huwa inabariki sehemu yenye amani. Na upendo huwa unakaa sehemu ambayo ina amani. Kweli, sehemu ambayo haina amani, upendo hauwezi kupatikana wala kuishi hapo.
Acha maisha ya ubinafsi katika ndoa yako, shirikiana na mwenzako wa ndoa, mheshimu, pangeni pamoja na kila mmoja aonekane ni mwanandoa ana haki na siyo vinginevyo.
Ziko ndoa nyingine ukiwaona watu walivyo hutoweza kujua kama ni wanandoa, bali ni utajua ni kama kijakazi na bwana wake. Ikatae hali hii, mwinue mwenzako kwa umoja na kila mmoja atakua juu lakini ubinafsi utawaangusha chini.
Kumbuka, aibu ya mmoja katika ndoa ni aibu ya wote, ishi misingi sahihi ya ndoa na utaona ndoa ni nzuri. Usikimbilie kuishi imani za watu walioshindwa kwenye ndoa zao bali ishi na imani yako kwa kile unachoamini wewe ni sahihi kwa sababu siyo kila imani inaweza kuwa sahihi kwa wote.
Usifuatilie matatizo ya ndoa za watu bali kuwa kinara wa ndoa yako. Unapokuwa bize kufuatilia ya ndoa za watu yako inaanguka na pale akili yako inaposikia zaidi kero za doa inaathirika na pale inaposikia zaidi kuhusu mafanikio makubwa za ndoa zinaimarika.
Waoneshe watu uko sahihi kwa kuishi kile unachoamini na kikaleta mafanikio.
Siri zenu za ndoa zibaki katika kuta nne za chumba chenu, huna haja ya kuanika kwa w
atu, maana kila mtu ana matatizo yake na usione wako kimya ukajua wako salama bali kila mtu anapitia yake hivyo nawe yavumilie yako na beba msalaba wako na anayekuambia ukimbie msalaba wako mwepuke mara moja.
Hatua ya kuchukua leo; ishini kwa umoja kama asili ya ndoa inavyotaka, kumbuka hata mwasisi wa ndoa alizifanya ndoa ziwe za umoja ndiyo maana mko wawili, utengano na ubinafsi ndiyo unaleta shida
katika ndoa, unaweza kumtatuta shetani kumbe shetani wenu ni ubinafsi wenu.
Kwahiyo, maisha ya ndoa yanadai umoja na siyo ubinafsi. Kwenye umoja kila kitu kinakaa amani, furaha, upendo , bahati na nk.
Anza kushirikana na mwenzako wa ndoa utaona jinsi bahati zitakavyoanza kumiminika katika ndoa yenu, usifanye vitu kwa kumficha mwenzako kuwa muwazi na mambo mengi yataenda vizuri sana maana kuna watu huwa wanawashirikisha wenza wao mambo yao pale yanapoharibika na kuomba ushauri, unapoanza kumshirikisha mwenzako jambo lolote lile unalotaka kufanya utapata baraka kuliko kufanya kwa ubinafsi na ndiyo maana ubinafsi unawatafuna na kuwaangusha wengi kwenye ndoa zao.
Makala hii imeandikwa na
Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali.
Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa
http://www.mtaalamu.net/kessydeo , vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.
Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505/0767101504
deokessy.dk@gmail.com //
kessydeo@mtaalamu.net
Asante sana