Enzi hizi tumekuwa na mashujaa wetu wapya, mashujaa ambao tumewageuza miungu na kuwasujudu. Mashujaa ambao hakuna walichofanya ambacho tunaweza kujifunza kwao, lakini tunawakubali na kuwaangalia kama mfano.
Mashujaa wa sasa wanapimwa na wingi wa wafuasi kwenye mitandao ya kijamii. Umaarufu unapimwa kwa namna mtu anavyoongelewa na wengine kwenye mitandao na vyombo vingine vya habari.
Umepata ‘likes’ na ‘comments’ ngapi baada ya kuweka picha yako mtandaoni? Hicho ndiyo kipimo kipya cha mafanikio na ushujaa kwenye zama hizi.
Tabia yetu wanadamu ni kutafuta njia ya mkato wa kufikia chochote kinachotukuzwa. Na katika ushujaa huu mpya, watu wameshajifunza njia ya mkato, ambayo ni kufanya mambo ya kijinga yatakayowafanya watu watake kuwafuatilia.
Kwa kuwa binadamu tunapenda umbea na udaku, kwa kuwa tunafuatilia maisha ya wengine kuliko yetu, basi wale wenye lengo la kupata ushujaa wa sasa, wanafanya mambo hayo ya kijinga. Wanaweka picha za uchi mitandaoni, wanawashambulia na kuwatukana watu wengine na mengine ya aina hiyo.
Kwa kuwa watu wanapenda umbeya, wanaanza kuwafuatilia kwa wingi, na muda siyo mrefu mtu anakuwa shujaa.
Wengine wanatafuta ushujaa huu kwa kuigiza maisha, kuweka aina ya maisha ambayo mtu hana. Kuagiza magari ya wengine na kupiga nayo picha kisha kuweka mitandaoni. Kwenda kwenye hoteli za kifahari na kupiga picha kisha kuweka mtandaoni na maigizo mengine ya aina hiyo ya kuwafanya watu waamini wana mafanikio makubwa, kumbe hawana.
Usipoteze muwa wako kwa mashujaa hawa wa kisasa na wala usipoteze muda wako kutafuta ushujaa huo. Huo ni mchezo ambao hupaswi hata kuushiriki, kwa sababu huwezi kushinda. Hata yule aliye shujaa leo, hatakaa kwa muda mrefu, atatokea mwingine aliye tayari kufanya mambo ya kijinga zaidi na kuteka mashabiki wa yule aliyekuwepo.
Wewe chagua eneo lako la kuhudumu, kama nilivyokuambia kwenye ukurasa uliopita hapa, peleka nguvu zako zote kwenye eneo hilo, weka kila ulichonacho kwenye eneo lako hilo. Kama kitu hakina mchango kwenye eneo hilo, achana nacho.
Jinsi unavyogusa maisha ya wengine kwa kuongeza thamani zaidi, ndivyo unavyokuwa shujaa wa kweli, shujaa ambaye atadumu. Hata kama watu hawatakutangaza na hutakuwa maarufu, lengo lako siyo kuwa maarufu, lengo lako ni kuhudumu. Kwa sababu kupitia kuhudumu kwako unaridhika wewe binafsi, wengine wananufaika na unapata fursa nzuri zaidi za kupiga hatua na kufanikiwa.
Tusijichanganye na mambo yanayoonekana yana manufaa ya muda mfupi lakini hayana mchango kwenye kile tulichochagua kufanya. Wacha wengine wahangaike na mambo hayo, wewe hudumu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,