Tofauti ya mjasiriamali na mfanyabiashara ni mjasiriamali yuko tayari kuchukua hatua za hatari ambazo hana uhakika na matokeo yake. Huku mfanyabiashara akichukua hatua ambazo zina uhakika na akiangalia zaidi faida kuliko kitu kingine. Mjasiriamali anaitaka faida, lakini kuna kitu kingine kikubwa zaidi kinachomsukuma ukiacha faida. Anakuwa na maono makubwa, kusudi kubwa analotaka kulitimiza, na hicho ndiyo kinamsukuma kuchukua hatua za hatari, ambazo watu wengine hawawezi kuzichukua.
Hakuna ubaya utukufu kuwa mjasiriamali au ubaya kuwa mfanyabiashara, muhimu ni kujua msukumo ulioko ndani yako na kuiishi huo kwa uhalisia badala ya kuishi maisha ya maigizo.
Sifa nyingine za mjasiriamali;
Kutokujitambulisha kwa kile anachofanya, ndiyo maana wengi huwa wanaleta mapinduzi kwenye maeneo mbalimbali. Kwa sababu hawajichukulii wao kama kile wanachofanya, bali wanajichukulia kama wakala wa kukamilisha kitu hicho.
Kuwa tayari kupoteza kidogo ili kupata kikubwa, hapa siyo uwezekano, bali inakuwa ni uhakika kwamba wanapoteza, lakini kwa kuangalia picha kubwa, wanakuwa tayari kupoteza.
Kutokuona aibu pale anaposhindwa, wengi wamekuwa wanakaribisha kushindwa haraka ili wajifunze na kusonga mbele. Hawaogopi au kuona aibu pale wanaposhindwa, kwa sababu wanajua hawajashindwa wao, bali kile wanachofanya ndiyo kimeshindwa, na hapo wanakifanya kwa utofauti.
Hawakai nje ya mchezo kwa muda mrefu. Kila mtu kuna wakati analazimika kukaa nje ya mchezo, kama wachezaji wanavyoumia na kulazimika kutokucheza kwa muda. Kwa mjasiriamali, huwa anavuka nyakati hizo haraka na kurudi kwenye mchezo, bila ya kujali ni nini amekabiliana nacho.
Kujua kitu pekee chenye uhakika ni mambo kwenda vibaya, na hivyo kujiandaa mapema. Huwa hawafikiwi na majanga kwa mshangao, kabla hawajachukua hatua wanajua kabisa matokeo mazuri na mabaya ya hatua husika na hivyo matokeo yoyote wanayoyapata hayawashangazi.
Wanalijua kusudi, wana misingi wanayoisimamia kila siku na wana nidhamu ya hali ya juu katika kutekeleza yale waliyopanga. Siyo watu wa kuahirisha mambo au kusubiri mpaka wajisikie kufanya, wanapanga na kufanya.
Hawatafuti umaarufu, japo umaarufu huja kwao baadaye. Wanafanya kwa sababu ni kitu muhimu kwao kufanya, wanafanya kwa sababu haijawahi kuwatokea kwenye fikra zao kwamba wanaweza kuendesha maisha yao bila kufanya walichochagua kufanya. Wanafanya kwa sababu hawatajisamehe pake wanapoona mambo yanaenda hovyo wakati wangeweza kuyafanya kuwa bora. Sifa na umaarufu ni vitu ambavyo hawajisumbui navyo, lakini huwa vinawafuata kutokana na matokeo mazuri wanayozalisha.
Kama unaziona sifa hizi ndani yako, usizizuie, badala yake ziishi. Jisikilize mwenyewe, tayari unajua nini unapaswa kufanya, ila kelele nyingi unazohangaika nazo zinakuzuia usione kilicho sahihi kufanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,