“Nimepata hii kazi ambayo siyo kitu ninachopenda, nitaifanya kwa miaka mitano, nikusanye mtaji kisha niiache na kwenda kuanzisha biashara ninayoipenda.”

Haya ndiyo mawazo ya wengi wakati wanaingia kwenye ajira. Lakini kati ya wengi wanaopanga hivyo, ni wachache wanaotekeleza kweli, maana wengi miaka mitano inapoisha wanajikuta kwenye madeni na mtaji waliokusanya hakuna.

“Nimeshakusanya mtaji wa kutosha, hii kazi inanibana sana, naiacha ili nikaanzishe biashara na niwe huru na muda wangu.”

Hayo ndiyo mawazo ya wale ambao walikuwa wamepanga kutumia ajira kukusanya mtaji na kufanikiwa kufanya hivyo. Lakini katika wale wanaochukua hatua hiyo, muda mfupi baadaye wengi wanakuwa wameshindwa kwenye biashara hizo na wanarudi kutafuta ajira.

Ninachokuambia mimi rafiki yako ni hiki, kama upo kwenye ajira, usiache ajira hiyo na kwenda kuanzisha biashara, usijaribu kabisa kufanya hivyo.

makirita cover 3-01

Zipo sababu nyingi kwa nini nakuambia hivyo, lakini hapa nitakushirikisha mbili za msingi kabisa, moja hasi na moja chanya, nitaanza na hasi.

MOJA; BIASHARA UNAYOKWENDA KUANZISHA ITAKUFA.

Kama hujawahi kufanya biashara kabisa kwenye maisha yako, biashara ya kwanza unayokwenda kuanza itakufa.

Sikuelezi hivi kukutisha au kukukatisha tamaa, bali kukupa ukweli ambao hutauona ukishajawa na hisia za kuanzisha biashara yako.

Kwenye nchi zilizoendelea, ambapo mazingira ya kibiashara ni mazuri kabisa, tafiti zimekuwa zinafanywa na matokeo yamekuwa ni ya kusikitisha na kuumiza.

Asilimia 80 ya biashara mpya zinazoanzishwa zinakuwa zimekufa ndani ya miaka mitano tangu kuanzishwa. Yaani kama mwaka huu kuna biashara mpya 10 zinaanzishwa, miaka mitano baadaye 8 zitakuwa zimekufa na 2 tu ndiyo zinazoendelea.

Sasa hapo ni kwa nchi zilizoendelea, ambapo wanaweza kufanya tafiti na mazingira yao ya biashara ni mazuri. Vipi kwa nchi ambazo zinaendelea na tafiti hakuna?

Huhitaji hata tafiti, wewe angalia eneo unaloishi, angalia biashara mpya ambazo zimekuwa zinaanzishwa kila wakati, mwaka baadaye biashara hiyo haipo. Yaani kunaweza kuwa na eneo la kufanyia biashara linalokodishwa na kila baada ya miezi sita ya pango kulipwa unakuta kuna biashara mpya imeanzishwa pale.

Ni kama mtu anaona eneo zuri la biashara, anajiambia atalikodi na kuanza biashara, anafanya hivyo, kodi ya miezi sita inaisha, anafunga biashara, eneo linabaki wazi, mwingine anakuja kukodi tena na mchezo unaenda hivyo.

Kuna changamoto nyingi sana kwenye biashara, ambazo huwezi kuzijua mpaka uingie, sasa unapoacha ajira na kuanza biashara ukiwa huna nguvu ya kukabiliana na changamoto hizo, unajiweka kwenye hatari ambayo huna namna ya kuivuka.

Hiyo ni sababu hasi, ambayo inaumiza kidogo, sasa twende kwenye sababu chanya ya kutokuacha ajira, ambayo itakufanya ujisikie vizuri.

MBILI; UNAPATA PESA ZA BURE.

Kama umeajiriwa na kila mwezi unalipwa mshahara, ni sawa na unapewa pesa za bure. Hebu fikiria, haijalishi mwezi umeendaje, haijalishi kiwango cha kazi, mwisho wa mwezi umefika na mshahara wako umeingia.

Rafiki, nakuambia hizo ni pesa za bure kabisa, kwenye biashara hakuna anasa ya aina hiyo, hakuna uhakika wowote, kuna mwezi utaweka kazi kweli kweli, lakini hutapata faida. Miezi haifanani.

Unaniambia hilo siyo kweli, siyo pesa za bure, natumikishwa, nafanya kazi sana. Na mimi nitakujibu unajidanganya tu, sehemu kubwa ya siku yako ya kazi huitumii kufanya kazi ambayo inaumiza na kuchosha kweli, bali unaitumia kwa mambo ya kawaida yasiyokuwa kazi.

Nimekuwa nasema kwa kazi nyingi za ofisini, ukifanya tathmini hasa ya muda ambao kweli mtu anafanya kazi, ile kazi ya maana hasa, haizidi masaa mawili kwa siku. Muda mwingine mtu anakuwa anajiandaa kwenda kwenye kikao, anafanya vikao, anakwenda mapumziko ya chai au chakula cha mchana anapiga soga za hapa na pale mpaka siku ya kazi inaisha.

Hata kwa zile kazi ambazo mtu anafanya kwa masaa, bado kuna muda mwingi ambao kunakuwa hakuna kazi, ni ile tu unapaswa kuwa unaonekana eneo la kazi kwa muda wa kazi.

Ndiyo maana nakuambia unapata pesa za bure, hivyo maamuzi ya kuacha kazi ili ukaanzishe biashara ni kuamua kuachana na pesa za bure huku ukienda kuanzisha kitu ambacho kutakufa. Je unafikiri hayo ni maamuzi sahihi?

Unanichanganya Kocha, wewe ndiye umekuwa unashauri kila mtu awe na biashara ambayo itampa nafasi ya kufanya kile anachopenda na kumpa uhuru wa muda na kipato pia. Sasa iweje utuambie tena tusiache kazi na kwenda kuanzisha biashara?

Ni kweli nimekuwa nasisitiza kila mtu awe na biashara, inayohusisha kile ambacho mtu anapenda kukifanya na anayoifanyia kazi na kuikuza ili baadaye iweze kumpa uhuru.

Lakini huwa sishauri mtu AACHE ajira na kwenda KUANZA biashara mpya.

Badala yake nimekuwa nashauri mtu…

UFANYE VYOTE KWA PAMOJA.

Ndiyo, endelea na ajira yako, huku ukianzisha biashara kwenye lile eneo unalolipenda. Pambana na vyote kwa pamoja na hili litakuwa na manufaa mengi, machache ni haya;

  1. Utakuwa na uhakika wa kipato cha kuendelea kuendesha maisha yako kutoka kwenye mshahara wako, hivyo hutaanza kuitegemea biashara mapema.
  2. Utaweza kuanza na mtaji kidogo huku ukiendelea kuukuza kadiri unavyokwenda.
  3. Una dirisha la kujaribu mawazo mbalimbali ya biashara mwanzoni mpaka kupata lile unalolipenda na sokoni linalipa.

Lakini kazi yangu inanibana, sina muda kabisa wa kuweza kuanzisha biashara wakati niko kwenye ajira ndiyo maana inabidi nikusanye mtaji ili niache kazi hii na kuingia kwenye biashara moja kwa moja.

Hiyo ni sababu unayojipa na utakayoniambia, ukiamini ni sababu sahihi. Inaweza kuwa kweli, lakini siyo sahihi. Inaweza kuwa kweli kwamba kazi yako inakubana, lakini siyo sahihi kwamba huwezi kuanzisha biashara ukiwa bado upo kwenye ajira.

Kwenye kitabu nilichoandika kinachoitwa BIASHARA NDANI YA AJIRA, nimekushirikisha njia sahihi kwako kuweza kuanzisha biashara ukiwa kwenye ajira yako, jinsi unavyoweza kuikuza na hatimaye kufika hatua ya wewe kuondoka kwenye ajira ukiwa umeshatengeneza uhakika kwenye biashara yako.

Hiki ni kitabu ambacho kila mtu aliyeajiriwa anapaswa kukisoma, iwe ana biashara au la, iwe anapanga kuingia kwenye biashara au la. Kwa sababu kina mengi yatakayokufungua na kukusaidia kufikia uhuru wako kwenye maisha, hata kama ajira imekubana kiasi gani.

Kitabu kina michanganuo ya biashara zaidi ya kumi unazoweza kuanza, zote ukiweza kuzifanya huku ukiendelea na ajira yako. Pia kinakupa mbinu za kukabiliana na changamoto mbalimbali kama ukosefu wa muda, mtaji na kupata wasaidizi bora kwenye biashara yako.

Rafiki, lengo la makala hii siyo kukutisha, bali kukupa tahadhari, kukuonesha kile ambacho hujakiona kabla hujafanya maamuzi hayo. Nimebahatika kuwakochi wengi na nimeona wengi wa walioondoka kwenye ajira na kwenda kuanza biashara mpya karibu wote walirudi kwenye ajira.

Ndiyo maana sitaki wewe ufanye makosa hayo, na kama ulishayafanya usiyarudie, anza biashara yako ukiwa kwenye ajira na ikishakua utakuwa huru kuachana na ajira hiyo.

Mwongozo sahihi kwako kufanya hivyo upo, ni kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA, kupata kitabu hiki, wasiliana na namba 0678 977 007 au 0752 977 170 na utatumiwa au kuletewa kitabu ulipo.

Na kama utapenda kupata nafasi ya kuwa karibu na mimi kwa ajili ya kupata ukocha wa karibu, basi hakikisha umejiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kama bado hujawa mwanachama, karibu ujiunge. Tuma ujumbe kwenda wasap namba 0717396253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA na utapata maelekezo ya kujiunga.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania