Kisichokuwa na msingi huwa hakidumu, hilo liko wazi.

Watu wengi wamekuwa wanaingia kwenye biashara bila ya kuwa na misingi sahihi, misingi ambayo wataisimamia katika kipindi chote cha biashara na ambayo itawafikisha kwenye mafanikio.

Hivyo kinachotokea ni watu kujikuta wanahangaika na mambo mengi yasiyokuwa na mchango kwenye biashara zao. Yanaweza kuwa mambo ya kuonekana ambayo wengine wanafanya, lakini kwa biashara husika yanakuwa hayana mchango.

Ndiyo maana ni muhimu sana unapoanza biashara, basi uweke wazi misingi sahihi ya biashara hiyo.

Na msingi mkuu unatokana na majibu ya maswali haya matatu;

Ninauza nini?

Ninamuuzia nani?

Ninamuuzia kwa njia gani?

Unauza nini ni bidhaa au huduma unayotoa ambayo inatatua tatizo au hitaji ambalo mteja analo. Lazima ujue wazi ni bidhaa au huduma ipi unayoitoa na jinsi gani inavyoongeza thamani kwa watu wengine.

Unamuuzia nani ni kujua mteja mkuu unayemlenga sifa zake, anakopatikana, uwezo wake, maumivu yake na mengine yote yanayomhusu mteja wa biashara hiyo. Kadiri unavyojua kuhusu mteja, ndivyo unavyoweza kuiweka biashara yako kwa namna itakavyomsaidia zaidi mteja.

Unamuuzia kwa njia gani haya ni yale yote ambayo yanafanyika kwenye biashara, kuanzia kuandaa na kupatikana kwa bidhaa au huduma mpaka inamfikia mteja. Hapa utajua wazi unahitaji kushirikiana na watu wa aina gani, utapata wapi malighafi, unatengenezaje bidhaa au kuandaa huduma na unamfikishiaje mteja. Pia unapaswa kujua njia bora ya kufanya hivyo ili mwisho uweze kubaki na faida.

Majibu hayo lazima yawe rahisi, ambayo unaweza kumweleza bibi yako wa miaka 80 na ambaye hakuenda shule akaelewa. Kama hawezi kuelewa basi hujayaelewa maswali na hivyo huna msingi sahihi.

Ukishapata majibu hayo ndiyo unayatumia kwenye maamuzi yote kwenye biashara yako, huo ndiyo msingi unaoufuata. Katika kuboresha na kukuza biashara, katika kuajiri na mengine.

Vipi kama umeshaanza biashara na hukuwa na msingi huo?

Safi, Thoreau anatuambia ukigundua umejenga kasri kwenye hewa, usikubali kupoteza kazi yako, maana hapo ndipo inapopaswa kuwa, sasa jenga misingi chini yake.

Una nafasi ya kujenga misingi sahihi sasa, ambayo itaizuia biashara yako isianguke siku zijazo. Ijenge na kuanza kuiishi ili biashara iweze kukua zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha