Huwa najifunza vitu vingi nikiwa nasoma vitabu, insha na makala mbalimbali mtandaoni.
Na huwa ninanakili baadhi ya vitu ambavyo baadaye naweza kuvitumia kwenye makala mbalimbali ninazoziandika.
Lakini kasi ya kukusanya vitu vya kuandika imekuwa kubwa kuliko kasi ya kuviandika.
Nimebadili kifaa ninachotumia kutunza yale niliyoandika kwa ajili ya kujumuisha kwenye makala za baadaye, na hilo limepelekea nimepoteza vipande vya maarifa zaidi ya elfu moja nilivyokuwa nimehifadhi.
Bado nimebaki na vipande vingine, ili visipotee kabla sijapata nafasi ya kuviweka kwenye makala, nimeona mara moja moja niwe naandaa makala hizi za mseto kwenye kurasa, ambapo nitaweka maarifa mengi kwa pamoja na wewe utachagua namna ya kuyafanyia kazi.
Hili ni toleo la kwanza, karibu ujifunze na kuondoka na hatua za kuchukua.
- Ukiona watu wako wa karibu wanahoji au kukosoa tabia yako kitu ambacho hawajawahi kufanya huko nyuma, jua kuna mabadiliko umeyafanya, na huenda siyo mazuri. Usiwabishie, badala yake tafakari kile wanachohoji au kukosoa na utaona njia ya kuwa bora zaidi.
- Chagua vitu ambavyo utafanya kila siku kwenye maisha yako bila kuacha, iwe uko nyumbani, umesafiri au mazingira yamebadilika. Inaweza kuwa kusoma, kuandika, mazoezi, na mengine kulingana na wapi unataka kufika.
- Tengeneza mchakamchaka wa siku 90. Binadamu huwa tunaweza kukomaa na kitu kwa siku 90, baada ya hapo huwa tunazoea au kuchoka. Panga malengo unayofanyia kazi kwa siku 90, kimbizana nayo kwa siku hizo. Baada ya hapo fanya tathmini na tengeneza malengo mengine ya siku 90.
- Kumbuka watu wanahitaji kuambiwa kitu mara saba ndiyo wakisikie kwa mara ya kwanza. Hivyo kumwambia mtu kitu mara moja haitoshi, endelea kurudia mara kwa mara mpaka mtu asikie na kuelewa.
- Wakati wa kufanya maamuzi magumu, unahitaji kufanya maamuzi yaliyo sahihi na siyo yanayowafurahisha au kuwaridhisha watu. Kwa sababu kufanya maamuzi ya kuridhisha wengine, huwa yanaleta matokeo mabaya baadaye. Ni bora kufanya maamuzi magumu sasa na kukabiliana na madhara yake, kuliko kuyapeleka mbele, maana yanakuwa makubwa zaidi.
- Ni bora kufanya maamuzi mabovu kuliko kutokufanya maamuzi kabisa. Maana ukifanya maamuzi mabovu unajifunza na wakati mwingine utafanya maamuzi sahihi, lakini usipofanya maamuzi kabisa hakuna unachojifunza.
- Matatizo ni kama uyoga, kukiwa na giza na mvua huwa yanakua haraka, kukiwa na mwanga na jua yanapotea. Acha kuficha matatizo yako, unayapa nafasi ya kukua zaidi, yaweke wazi na utaweza kuyatatua, au yatatoweka yenyewe.
- Ushauri ambao wale waliofanikiwa sana wamekuwa wanatoa; kuwa mwaminifu, kuwa wewe, kuwa mnyenyekevu, kuwa mdadisi, jenga mtandao wako na weka kazi kila siku. Na nyongeza, usiwe mjuaji wa kila kitu, kuwa tayari kukubali usiyojua na kujifunza kwa wengine.
- Usikazane kuwa mwangalifu, bali kazana kufanya kile kilicho sahihi kwa yale unayokabiliana nayo sasa.
- Mtu akikuuliza swali kuhusu adui yako, mfano adui yako ni Amani, halafu mtu anakuuliza, unamzungumziaje Amani? Mjibu, Amani ndiyo nani? Usiongeze maelezo mengine yoyote, hivyo tu, hata akikutajia majina yake kamili, muulize ndiyo nani huyo. Mazungumzo yatabadilika.
- Mtu akija kwako na kukuambia kuna mtu alikuwa anakusema vibaya, mwambie hutaki hata kusikia mtu huyo alikuwa anasema nini, maana siyo kitu muhimu, kingekuwa muhimu mtu huyo angekufuata akuambie mwenyewe, siyo kuwaambia wengine.
- Kuna aina mbili za malengo, malengo ya chanya na malengo hasi. Malengo chanya ni yale ya kufanya kitu, mfano kuongeza kipato, huku malengo hasi yakiwa ya kuepuka kitu, mfano kuacha pombe. Kazana kuweka malengo chanya zaidi kuliko hasi, maana malengo hasi yanaleta hisia hasi kwako na kuwa vigumu kuyafikia.
- Unajua benki huwa zinapataje faida, wewe unaweka fedha zako kama akiba kwao na wao wanachukulia kwamba una fedha na huna cha kuzifanyia. Hivyo benki wanachofanya wanatafuta mtu ambaye ana cha kufanya ila hana fedha, na wanampa fedha zako afanyie kazi. Kinachotokea sasa, benki inamtoza yule iliyempa fedha zako riba ya asilimia 20 kwa mwaka, lakini wewe inakupa riba ya asilimia 1 mpaka 2 kwa mwaka. Hivyo benki inaingiza mara 10 ya kile inachokulipa.
- Kama umekuwa unashindwa kusema hapana na mwishowe kuishia kujikuta umekubali vitu vingi kuliko uwezo wako wa kufanya, kila mtu anapokuja kwako na kitu anachotaka ufanye, jiulize kama ingekubidi uache kila unachofanya wakati huo na ufanye kitu hicho, je ungesema ndiyo? Kama jibu ni hapana basi sema hapana, haijalishi kama umeambiwa unafanya wiki ijayo, mwezi ujao au mwaka ujao, kama huwezi kufanya sasa, hutaweza kufanya wakati huo.
- Kuna njia tatu zinazoweza kuponyesha magonjwa mengi ambayo mwili wako unahisi unayo bila hata ya kwenda kwa daktari; kunywa maji ya kutosha, kupata muda wa kutosha wa kupumzika na kufunga. Ukijisikia mwili wote unauma na ukaenda hospitali ukafanyiwa vipimo na kuambia vipimo havioneshi una ugonjwa wowote, fanya mambo hayo matatu, kwa sehemu kubwa utakaa sawa.
- Kama una tatizo, na tatizo hilo linaweza kutatuliwa na fedha, basi jua huna tatizo. Kama una tatizo ambalo fedha inaweza kutatua ila huna fedha za kulitatua, tatizo lako ni fedha.
- Tumia fedha ulizonazo kununua uhuru wako, kama kuna kitu unafanya na kinachukua muda wako, ila kuna mwingine anayeweza kukifanya na ukamlipa fedha ambayo ni ndogo kuliko unayopata kwa kufanyia kazi vitu vingine, fanya hivyo. Hiyo ndiyo kazi ya pesa.
- Njia bora ya kujitolea na kuwasaidia wengine ni kutoa fedha. Wengi wamekuwa wanafikiria muda ni njia bora ya kujitolea lakini siyo, labda kama ni muda wa kukaa na kuongea na wale unaotaka kuwasaidia. Lakini kama watu wana njaa, kujitolea kwenda kuwapikia ni kupoteza muda wako, huo muda utumie kufanya kazi au biashara zako, ingiza kipato na wasaidie fedha zitakazoweza kutatua tatizo lao.
- Unapojikuta njia panda na hujui ufanye nini, chagua kufanya chochote, utajifunza kwa kufanya chochote kuliko kutokufanya kabisa.
- Hakuna hisia nzuri au mbaya, ila kuna matumizi mazuri au mabaya ya hisia. Mfano ukiwa na hasira, unaweza kutumia hisia hizo kutambua kile ambacho hakipo sawa na kusaidia kikae sawa, au ukazitumia kuwaumiza wengine.
- Kutengwa au kuachwa huwa kunagusa sehemu ya ubongo inayohusu maumivu ya kawaida, hivyo mtu huumia kama vile mwili wake umeumizwa. Kutumia dawa ya maumivu katika hali kama hizo inasaidia.
- Idara za masoko kwenye makampuni makubwa huwa zinatumia vizuri hisia kuu mbili za watu, hofu na tamaa ya kuwa juu zaidi ya wengine. Angalia tangazo lolote, utaambiwa nafasi au bidhaa ni chache, utaona watu wanaovutia, vyote hivyo ni kugusa hisia zako.
- Kuna dhana ya Kijerumani inayoitwa Schadenfreude, ambayo inaeleza asili yetu sisi binadamu kujisikia vizuri pale tunapogundua wengine wana matatizo makubwa kuliko sisi. Hii ndiyo maana watu wanapenda kushindana kwa matatizo yao, lengo siyo kuona nani ana matatizo zaidi, bali kujilinganisha na kuona kama wewe ndiyo una matatizo zaidi au kuna wengine wana makubwa kuliko wewe. Hivyo ukijikuta kwenye hali ya watu kulinganisha matatizo, hakikisha ya kwako yanaonekana mabaya na makubwa zaidi.
- Ni rahisi kuhukumu mtu kwa kile ambacho umemuona au kusikia amefanya. Lakini jua kuna vitu vingi hujui kuhusu mtu huyo, ungepata nafasi ya kuwa ndani yake, usingetoa hukumu uliyoitoa.
- Kila mtu ana sababu nzuri ya kwa nini amefanya kitu fulani, hata kama kwa nje inaonekana ni mbaya, ndani yake ana maelezo mazuri. Jaribu kuwaelewa watu kabla hujawahukumu.
- Ni rahisi kuangalia yale yajayo, ambayo huyajui na kuyahofia, lakini unachopaswa kujua ni kwamba huishi kesho, bali unaishi leo, sasa. Hivyo ishi sasa kwa ukamilifu, yajayo yatakuja au yasije kwa mpango wake yenyewe.
- Ukipewa uhakika kwamba kesho unakufa, utatumia muda wako wa leo kubishana na watu mtandaoni, kuwajibu wanaokutukana, kuwachukia watu na mengine ya aina hiyo? Jibu ni hapana, hutofanya hivyo. Sasa swali ni je nani amekuhakikisha kesho utakuwepo? Kwa nini unapoteza muda wako wa thamani leo kwa mambo yasiyo na maana wakati hujui ni muda kiasi gani umebaki nao?
- Katika kila hali ya maisha, angalia kile ulichopata na siyo ulichokosa au kupoteza. Hakuna anayepata kila anachotaka kwenye maisha, hivyo usijiumize na hilo.
- Kamwe usijilinganishe na wengine kwenye mali au vitu vya nje, kwa sababu kuna mtu atakuwa amekuzidi, hata kama umepiga hatua kiasi gani. Ukishajilinganisha na wengine, unajidharau na kuona hujakamilika.
- Kuna njia nne za kukabiliana na tatizo au changamoto unayokutana nayo kwenye maisha; kuitathmini upya, kuiangalia kwa ukawaida, kuipangilia upya na kuigeuza kinyume. Kwa kufanya hivyo utaielewa changamoto kwa undani.
- Unaposema hapana, unakataa kitu kimoja, unaposema ndiyo unakubali kila kitu. Unaposema hapana unaokoa muda wako wa baadaye, unaposema ndiyo unagharimu muda wako wa baadaye. Hapana ni taji, ndiyo ni mkopo. (unafikiri kwa nini walisema ahadi ni deni). Sema HAPANA.
- Njia ya haraka ya kufanya kitu ambacho siyo muhimu ni KUTOKUKIFANYA. Njia ya haraka ya kuperuzi mtandao ili urudi kwenye kazi zako ni kutokuperuzi kabisa mtandao. Kama kitu siyo muhimu, haijalishi unakifanya haraka kiasi gani, kinabaki kuwa siyo muhimu, hivyo usikifanye.
- Kama kuna kitu unataka kukitatua lakini umekazana nacho na hupati jibu. Kiweke kitu hicho kama swali kwenye akili yako, kisha acha kabisa kukazana kupata jibu. Wewe endelea na mambo yako mengine, utashangaa siku jibu linakuja lenyewe, bila hata ya kuhangaika sana.
- Lengo la ubongo ni kupunguza matumizi ya nishati, kufikiri kunatumia nishati nyingi, ndiyo maana ni vigumu kufikiri, ubongo wako utakuzia kabisa usifikiri kwa kukupa majibu ya haraka. Hivyo unapofanya kazi inayokutaka kufikiri, hakikisha una nishati ya kutosha mwilini.
- Unaweza kuifanya kazi yako kwa viwango vya juu sana, au unaweza kucheza na simu yako siku nzima, huwezi kufanya vyote kwa pamoja.
- b) Muda ambao watu wangetumia kuja na mawazo ya kibunifu, ndiyo huo wanaupoteza kwa kutengeneza video za TikTok, kuweka picha instagram na kufuatilia maisha ya wengine mitandaoni.
- Kushindana ni mchezo wa walioshindwa, washindi hawashindani, bali wanajitofautisha.
- Charles Darwin, mwanabailojia aliyekuja na nadharia ya mageuzi kwenye asili ya mwanadamu, alioa binamu yake. Kuwa na maarifa sahihi kunaweza kuzidiwa nguvu na hisia.
- Watu wapumbavu ni rahisi kuajiri, na dunia imejaa wapumbavu wengi, wengi wanaonekana ni wema kabisa na wanaokutakia wema, lakini kitakachokugharimu ni upumbavu wao. Utaishia kukupa hasara kubwa, pamoja na kwamba wao wenyewe hawapendi. Hivyo epuka wapumbavu kama unavyoepuka ukoma.
- Kuwa tajiri ni kazi kama zilivyo kazi nyingine, unahitaji kuipa umakini na kujituma kweli ili kuikamilisha. Jiamini na fanya kilicho sahihi kufikia lengo hilo.
- b) Kazi ya kuwa tajiri ni rahisi ukilinganisha na kazi nyingine kama uchungu wa kuzaa mtoto, kulea watoto, kumwambia mzazi kwamba mtoto wake amekufa na hata kazi nyingine zinazotumia nguvu na zenye maumivu. Ukifanya kwa usahihi, kazi ya kufikia utajiri haitakuchosha na kukuumiza kama hizo nyingine.
- Kitendo tu cha wewe kuzaliwa ni bahati, kumbuka siku ya kutungwa kwa mimba yako, kulikuwa na mbegu zaidi ya milioni moja zilizokuwa zinashindana kuingia kwenye yai, mbegu wewe ukashinda. Usijidharau, wewe ni mshindi tangu unazaliwa, anza kuishi maisha yako ya ushindi.
- Mwandishi mmoja aliyeandika kitabu cha JINSI YA KUWA TAJIRI alisema maneno haya kwenye utangulizi; nafasi ya wewe kuwa tajiri baada ya kusoma kitabu hiki ni ndogo mno. Sababu kuu tatu; una roho nzuri sana, umeridhika mno na tayari umeshajipa hadhi fulani. Hivyo vitatu ndiyo adui yako kwenye mafanikio, haijalishi unajifunza mambo mazuri kiasi gani, bila kuvunja hivyo vitatu, hutapiga hatua.
- Zaidi siyo bora, bora ni bora. Huhitaji kupata zaidi, unahitaji kupata kilicho bora. Huhitaji kufanya zaidi, unahitaji kufanya kilicho bora. Dunia inatuhadaa na zaidi, wakati kinachohitajika ni bora.
- Hakuna kikwazo kikubwa kwa mtu kufikia utajiri kama mshahara mnono na wa uhakika kila mwezi.
- Usiwalazimishe watu wakuheshimu, bali anza kujiheshimu mwenyewe, jiwekee viwango na viishi kwenye maisha yako. Simamia viwango vyako kwa gharama yoyote ile na watu watakuheshimu wao wenyewe.
- Hakuna aliye tayari kulipa gharama kubwa kupata kitu feki wakati anaweza kupata kilicho halisi kwa gharama hiyo hiyo. Kama unataka kulipwa zaidi au kupata fedha zaidi, acha kuiga wengine na anza kuwa wewe. Kuwa wewe halisi, na watu watakuja kwako wakiwa tayari kukulipa zaidi, kwa sababu unawapa kile ambacho hawawezi kukipata pengine.
- Wale ambao wameshakata tamaa kwenye utajiri, watahakikisha na wewe unakata tamaa, hawatakuwa tayari kukuona ukifikia utajiri wakati wao wanaamini haiwezekani.
- Kama haupo bize kujifunza, upo bize kufa. Kwenye maisha hakuna kusimama, unakua au unakufa, unaenda mbele au unarudi nyuma, chagua ni mwendo upi unaoutaka.
- KUJITEGEMEA ndiyo ufunguo mkuu wa mafanikio kwenye maisha yako. Hakuna atakayekuja kukuokoa pale ulipo sasa, ni wewe upambane kutoka hapo. Mwanasiasa atakuambia amekuja kukuokoa, ila kumbuka utamuona kila baada ya miaka mitano. Jamii itakuambia iko kwa ajili yako, ila kumbuka haitakuruhusu uwe wewe. Hii ni vita yako, ipigane.
- Tafuta wateja bora zaidi. Kama wateja ulioa nao sasa wanakusumbua, weka vigezo vya wateja ambao unajua hawatakusumbua, jua unawapata wapi, jua utawashawishije, kisha watafute hao. Kuanzia hapo, usipokee tena wateja wasiokuwa na vigezo vipya ulivyojiwekea.
- Kwenye zama tunazoishi sasa, ambazo zina usumbufu usio na ukomo, una silaha mbili za kutumia, umakini (fokasi) na vipaumbele. Kuwa mkali kwenye matumizi ya muda na umakini wako kwa kuweka vipaumbele sahihi kwako. Kuna vitu havina mchango wowote kwako, usivifanye. Kuna watu ambao hawana mchango wa kukufikisha unakotaka kufika, waepuke. Weka macho yako kwenye kile unachotaka kufikia na hicho ndiyo kipaumbele chako na umakini wako unapopaswa kuwa.
Tutaishia hapo kwa leo, siku nyingine tutaendelea na mseto huu ili kuepuka kupoteza mawazo mazuri mengi ninayoyakusanya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kuna mengi ya kujifunza na kujikumbusha.ahsante sana kocha.
LikeLike
Karibu.
LikeLike
Habar kocha, namba 10 naomba ufafanuzi, mazungumzo yanabadilikaje kiongozi?
LikeLike
Lengo la zoezi hili ni kubadili mazungumzo, badala ya wewe kueleza kuhusu mtu uliyeulizwa, unajifanya kama humjui, na hapo kutakuwa hakuna tena cha kuzungumza kuhusu mtu huyo, maana humjui.
Hii inasaidia kuepuka kuwasema wengine kwa ubaya.
LikeLike