Hakuna majibu rahisi kwenye maisha, hakuna njia za mkato za kufanikiwa na hakuna kitu kimoja ambacho kikifanywa na kila mtu basi atapata mafanikio makubwa.

Tunatofautiana kwa mambo mengi, kuanzia yale tunayopendelea, mazingira, uwezo, kiwango cha hamasa, kiasi cha kuridhika na mengine mengi.

Lakini kuna namna ya kuyakabili maisha, ambayo kila mtu akiifanyia kazi ataweza kutatua changamoto nyingi anazokabiliana nazo kwenye maisha na kufikia mafanikio makubwa.

Njia hiyo ni kuweka kipaumbele kwenye kazi na upendo.

Fanya kazi, wapende watu. Ukisimamia hili kila wakati, utapata jawabu la karibu changamoto zote unazopitia kwenye maisha.

Changamoto ambayo haitaweza kutatuliwa kwa kazi na upendo, basi itatatuliwa kwa muda, ipe muda na itapotea yenyewe. Lakini wakati wote wewe pambana na kazi na upendo.

Kazi inakupa heshima, kazi inakutambulisha na kazi ndiyo inayokupa kila unachotaka kwenye maisha yako. Heshima unayoipata kutokana na kazi yako ni heshima inayodumu. Heshima nyingine isiyotokana na kazi haiwezi kudumu, kwani wale wanaokupa heshima hiyo wanaweza kukunyang’anya, ila heshima ya kazi yako, hakuna mwenye uwezo wa kukunyang’anya.

Upendo ndiyo dawa na silaha ya mambo mengi unayokabiliana nayo. Wapo watakaochagua kukuchukia kwa wewe kuchagua kuyaishi maisha yako, wapende. Wapo watakaokuonea wivu kwa hatua fulani unazopiga, wapende.

Upendo siyo tu unawasaidia wale unaowalenga, bali unakusaidia wewe mwenyewe pia. Kwa kuwa na upendo kwa wengine, hupati muda wa kuwa na chuki au wivu kwa wengine, hivyo hupotezi nguvu zako kwa mambo yasiyo na tija.

Jijengee nidhamu thabiti ya kazi, kwa kuweka vipaumbele vyako vizuri na kuwa king’ang’anizi kwenye kile unachofanyia kazi. Usikubali kubughudhiwa na kelele zinazoendelea na wala usiwe rahisi kuahirisha yale uliyopanga kufanya. Usiache kufanya mpaka umepata kile unachotaka kupata.

Mafanikio makubwa ni matokeo ya kuchagua eneo moja na kuweka kila ulichonacho, kuweka kazi hasa, huku ukipenda kile unachofanya na kuwapenda wale unaoshirikiana nao katika kukifanya. Kazi na upendo, hakuna namna unaweza kuvitenganisha kama unataka mafanikio makubwa.

Ukiwa tayari kuweka kazi, huku ukisambaza upendo, hakuna chochote chenye nguvu ya kukuzuia, utawaka kama moto kwenye majani makavu, hata walio mbali watakuja kushangaa moto huo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha