Watu huwa wana hitaji kubwa la kuamini kwenye kitu chochote kile. Na hivyo watatafuta chochote wanachoweza kukiamini na kwenda nacho.

Maisha yetu wanadamu ni magumu sana bila ya kuwa na imani kwenye kitu fulani. Pale mambo yanapokuwa magumu na changamoto kuwakabili watu, kinachowawezesha kuvuka ni kile wanachoamini.

Hii ndiyo maana kwenye kila jamii kuna dini, falsafa na hata ushirikina ambao watu wanaamini.

Kabla ya kuja kwa dini, watu waliamini vitu mbalimbali kulingana na mazingira yao. Wale waliokaa karibu na miti mikubwa waliiamini hiyo, waliokaa karibu na mlima waliamini kwenye mlima.

Chochote ambacho kilionekana kuwa kikubwa kuliko watu, na ambacho hawawezi kukielezea basi ilikuwa ndiyo kitu wanachopeleka imani yao.

Kwa maneno mengine, sisi binadamu tumekuwa tunatengeneza miungu mbalimbali kulingana na kile tunachopitia au mazingira tuliyopo. Hatuwezi kwenda bila ya kuwa na kitu cha kuamini.

Hili lina manufaa matatu kwako;

Moja, weka imani kuu kwako mwenyewe, jiamini mwenyewe na amini kwenye ndoto kubwa unayoifanyia kazi kwenye maisha yako. Usijiruhusu kuwa na mashaka ya aina yoyote ile.

Mbili, unapotaka kuwashawishi wengine, jua ni nini hasa wanachoamini, jua imani zao kuu zilipo na hapo utajua jinsi gani ya kuweza kuwashawishi kupitia kile wanachoamini.

Tatu, wale wanaotaka kukushawishi, wamekuwa kwanza wanakufanya ujenge imani kwao, hata tapeli, haji moja kwa moja na kukutapeli, bali anajenga kwanza imani, na ukishamwamini basi anatekeleza utapeli wake kwa urahisi. Hivyo kuwa makini na wale wanaokuteka uwaamini kwa namna yoyote ile, hakikisha hufanyi kitu kwa sababu tu umeweka imani kwa mtu, badala yake hakikisha unafanya kile ambacho ni sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha