“The cucumber is bitter? Then throw it out.
There are brambles in the path? Then go around.
That’s all you need to know.” — MARCUS AURELIUS

Maisha ni magumu na yenye changamoto na vikwazo kwa kila mtu.
Ila kuna watu ambao huwa wanachagua kuyafanya maisha yao kuwa magumu zaidi ya yanavyopaswa kuwa.
Wanafanya hivyo kwa kulazimisha dunia iende kama wanavyotaka wao,
Kitu ambacho kipo nje kabisa ya uwezo wao.

Kuyafanya maisha yako kuwa rahisi, acha kulazimisha mambo kwenda kama unavyotaka wewe.
Badala yake nenda na mambo jinsi yanavyokuja kwako.

Kwa kila unachokabiliana nacho jiulize ni hatua zipi sahihi kwako kuchukua, kisha chukua hizo.
Kama kuna kitu hukipendi achana nacho.
Kama kuna watu ukiwa nao wanakufanya ujisikie vibaya acha kukaa nao.
Kama unakabiliana na ugumu wowote utatue, kama huwezi kuutatua achana nao.

Asili huwa inatupa matatizo ambayo tunaweza kuyatatua au kuyavumilia.
Hivyo kwa kila tatizo linalokukabili jiulize kama kuna kitu unaweza kufanya kulitatua.
Kama kipo, fanya kitu hicho.
Kama hakuna unachoweza kufanya basi achana na tatizo hilo na endelea na mambo mengine.
Lipuuze kabisa, chukulia kama ni kitu kisichokuwepo.
Kwa njia hiyo utapata nafasi nzuri ya kuendelea na mengine unayoweza kufanyia kazi.

Kusumbuka na kitu ambacho huwezi kutatua ni kupoteza muda ambao ungeweza kuutumia vizuri kwa yale unayoweza kutatua.

Maisha tayari ni magumu, usiyafanye kuwa magumu zaidi kwa kulazimisha dunia iende kama unavyotaka wewe.
Dunia inaenda kwa mipango yake yenyewe na huwa haichukui maoni ya mtu yeyote.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu kujidanganya kwenye muda, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/08/02/2041

Wako rafiki katika safari ya kuelekea kwenye mafanikio makubwa,
Kocha Dr Makirita Amani.