Charlie Munger kwenye moja ya ushauri wake kwa vijana aliwaeleza mambo muhimu ya kuzingatia kwenye maisha ili waweze kufanikiwa.

Kwanza aliwaambia wanapaswa chochote kile kwa ubora wa hali ya juu sana, kadiri ya uwezo wao.

Pili aliwaambia wasidanganye, mara zote waseme ukweli hata kama unaumiza kiasi gani.

Tatu aliwaambia kutekeleza kile wanachoahidi, kufanya neno lao kuwa sheria, wakisema wanafanya kitu, basi watekeleze kama walivyoahidi.

Na nne ambalo ndiyo muhimu ninalotaka kukushirikisha na uondoke nalo hapa, omba samahani na usitoe visingizio. Ukimkosea mtu, muombe samahani na usijaribu kutoa visingizio kwa nini umekosea, kwa sababu visingizio yako havitaondoa kosa. Kama umekubaliana na mtu mkutane muda fulani, basi ondoka mapema ili uwahi muda huo, ikitokea umechelewa, omba samahani na usianze kutoa sababu kwa nini umechelewa, haitasaidia chochote.

Hii ya nne nimeona kuna funzo kubwa sana kwa kila mmoja wetu kujifunza, huwa tunakimbilia kutoa sababu na visingizio kwa ili kuhalalisha kosa tulilofanya au kufikiri tutapata huruma zaidi. lakini tunachopata kwa kufanya hivyo ni kuwaumiza zaidi wale ambao tumewakosea au kuwakwaza. Kitu sahihi kufanya ni kuomba samahani kweli kutoka ndani ya moyo wako na kufanya kilicho sahihi.

Uzuri wa kuomba samahani bila kutoa visingizio ni kwamba itakulazimu kufanya kilicho sahihi wakati wote. Kwa mfano umechelewa mkutano wa kwanza na mtu, ukafika na kumwambia umechelewa kwa sababu ya foleni. Sababu hiyo itakufanya siku nyingine tena uchelewe na usingizie foleni. Lakini kama umechelewa na kuomba samahani bila kutoa sababu, wakati mwingine itakubidi uwahi, maana ukichelewa tena itaonekana ni makusudi.

Unapokosea au kumwaza mtu, omba samahani kutoka ndani ya moyo wako na ishia hapo, usitoe sababu wala visingizio. Na hakikisha hurudii tena kile ulichofanya ukakosea au kumwaza mwingine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha