Bilionea mwekezaji Warren Buffett huwa anashirikisha vigezo vyake vinne ambavyo huwa anavitumia kufanya maamuzi ya uwekezaji.

Vigezo hivyo ni kama ifuatavyo;

  1. Je ninauelewa uwekezaji huu? Kama hauelewi basi hawekezi, hata kama unaonekana kuwa na faida kubwa.
  2. Je uwekezaji huu una kitu cha kuutofautisha na wengine, kama ni biashara ina kitu kinachoitofautisha na biashara nyingine ambacho hakiwezi kuigwa? Uwepo wa kinachotofautisha ndiyo unafanya uwekezaji uwe bora.
  3. Je uwekezaji huo unaongozwa na watu wenye uwezo na ambao ni waaminifu? Kama watu hawana uwezo au siyo waaminifu, huo siyo uwekezaji mzuri.
  4. Je bei ni sahihi, yaani bei yake iko chini kuliko bei ya soko?

Buffett anasema kama uwekezaji utapita kwenye vigezo hivyo vinne basi anaweka fedha zake, kama hata kigezo kimoja kinakosekana hafanyi uwekezaji. Ni bora akae na fedha bila kuziwekeza kuliko kuwekeza kwenye biashara ambayo haikidhi vigezo hivyo, kwa sababu mwisho wa siku atapata hasara.

Hivi pia ndivyo unavyopaswa kufanya kwenye maisha yako, kwa maamuzi yoyote muhimu ambayo unapaswa kuyafanya, jiwekee vigezo kabla ya wakati wa kufanya maamuzi hayo.

Kwenye vigezo vyako weka vitu ambavyo lazima viwepo ndiyo ukubali, visipokuwepo usijidanganye.

Utaweza kutengeneza vigezo vyako kwa kuangalia jinsi wale waliofanikiwa kwenye eneo hilo wamekuwa wanafanya maamuzi yao, pia angalia makosa ambayo umekuwa unafanya huko nyuma na yatumie kuweka vigezo ambavyo wakati mwingine hutarudia makosa hayo.

Mfano kama umekuwa unashawishika kuingia kwenye fursa ambazo baadaye unagundua siyo sahihi, angalia ni namna gani umekuwa unafanya maamuzi hayo, kisha weka vigezo vitakavyozuia usirudie maamuzi yanayokuumiza.

Kuwa na vigezo mapema ni muhimu kwa sababu unapokuwa kwenye hali ya kufanya maamuzi, mara nyingi unakuwa umetawaliwa na hisia fulani, inaweza kuwa tamaa, hasira au furaha. Hisia hizo zitakuzuia usione uhalisia na hivyo kufanya maamuzi yasiyo sahihi. Hata wale wanaokusukuma ufanye maamuzi yatakayowanufaisha wao, huhakikisha wanachochea hisia ndani yako.

Kuwa na vigezo, vifuate na utafanya maamuzi sahihi mara zote.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha