Ni asili yetu binadamu kuyakimbia maumivu, huwa hatuyapendi, kwa sababu yanaumiza.
Lakini wote tuna ushahidi ni jinsi gani maumivu mbalimbali yalivyokuja na manufaa kwenye maisha yetu.
Maumivu uliyowahi kupata kwenye mahusiano yalikusaidia kupata watu walio sahihi.
Maumivu uliyopata kwenye ajira yalikusukuma kujiajiri.
Maumivu uliyoyapata kwa biashara kuwa ndogo yakakusukuma kuikuza biashara yako.
Kitu kingine ambacho sisi binadamu hatukipendi ni kubadilika, katika hali ya kawaida, huwa tunapenda kufanya kile ambacho tumezoea kufanya kuliko kujaribu kitu kipya.
Namna pekee tutakayosukumwa kufanya kitu kipya ni kama maumivu ya kile tulichozoea kufanya ni makubwa kuliko maumivu ya kile kipya cha kufanya.
Maamuzi yetu yote yanapima kiwango cha maumivu, na tunakimbia kile ambacho kina maumivu zaidi.
Kwa kujua manufaa haya ya maumivu, sasa anza kutumia maumivu yako kama mtaji. Kwa kila maumivu unayokutana nayo, badala ya kulalamika kama wengine wanavyokuwa wanafanya, wewe jiulize ni mtaji gani uko hapo, manufaa gani unayoweza kuyapata, namna gani unaweza kubadilika.
Usiyakimbie maumivu na usikubali maumivu yakuache kama ulivyokuwa awali. Tumia maumivu kuwa bora zaidi.
Hata kama maumivu hayana kitu cha kukupa, basi yafanye yakupe hekima zaidi, kwa kujifunza kwenye kile unachopitia ili uweze kuwa bora zaidi na kufanya maamuzi sahihi wakati mwingine.
Pia jua wakati ambapo unayakimbia maumivu na kabla hujayakimbia angalia manufaa yaliyopo kwenye maumivu hayo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,