Hakuna kitu chenye thamani kwenye maisha ambacho hakihitaji kazi katika kukijenga na kukilinda.

Huwa tunafikiria kazi na biashara tunazofanya ndiyo zinahitaji kuweka kazi na juhudi, huku vitu vingine tukitegemea vitokee vyenyewe, bila sisi kuweka kazi.

Hapo ndipo wengi wanapokwama, kwa kutokuweka kazi kwenye maeneo mengine ya maisha yao, yanaanguka na hivyo kupelekea kuanguka kwenye yale wanayoweka kazi pia.

Moja ya maeneo ambayo huwa tunayasahau sana ni mahusiano, huwa tunaamini tukifanya kazi au biashara zetu na kuingiza kipato cha kutosha, basi mahusiano yetu yatakuwa bora.

Lakini huo siyo ukweli, mahusiano huwa hayawi bora yenyewe, bali mahusiano yanakuwa bora kama yanajengwa.

Na hapa ni mahusiano yote, kuanzia ya ndoa au mapenzi, familia, urafiki na mengineyo, kazi inahitajika katika kujenga mahusiano ambayo ni bora na imara.

Kila mahusiano yanahitaji muda, muda wa kuwa na wale ambao una mahusiano nao ni hitaji muhimu katika kujenga na kuimarisha mahusiano. Kadiri watu wanavyokosa muda wa kuwa pamoja, ndivyo mahusiano yanavyodhoofu.

Kila mahusiano yana migogoro na hali ya kupishana au kutokuelewana, inahitaji kazi kutatua migogoro hiyo, kuelewana na kwenda pamoja. Wengi wamekuwa wanakimbia mahusiano kwa sababu ya migogoro, wakiamini wanaweza kuwa na mahusiano mengine yasiyo na migogoro, kitu ambacho huwa hakitokei.

Mahusiano huwa yanatupima, yanatufundisha na pia kutupa fursa mbalimbali za kupiga hatua kwenye maisha. Tunachopaswa kufanya ni kuweka kazi ya kutosha ili kujenga na kuimarisha mahusiano muhimu kwetu.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha