Huwezi kuanza na kuimaliza siku yako nzima bila ya mtu kukukwaza kwa namna moja au nyingine, labda kama hutakutana au kuwasiliana na mtu kwenye siku yako.
Watu kukuangusha au kukukwamisha ni hali ya kawaida kwenye kila siku ya maisha yako.
Mtu atakuahidi kitu na hatatekeleza, mwingine atachelewa tofauti na matarajio na mwingine ataharibu kitu ambacho ulikuwa unakitegemea sana.
Njia pekee ya kuhakikisha yale ambayo watu wanafanya hayakusumbui, unapaswa kuwa mtu usiyevurugwa, yaani hata kitokee nini, wewe unakuwa tulivu kabisa.
Hufanyi hivi kwa kuigiza, bali kwa uelewa mkubwa ambao unakuwa nao kuhusu maisha na wewe mwenyewe.
Kwanza kabisa unaianza kila siku ukiwa unajua kuna mambo mengi yatakayotokea ambayo yako nje ya uwezo wako kabisa, hivyo lolote linapotokea, hushangazwi, ulitegemea na hapo unachukua hatua sahihi.
Pili unajua nini kipo ndani ya uwezo wako na nini kipo nje ya uwezo wako, kwa kilicho ndani ya uwezo wako unachukua hatua, kwa kilicho nje ya uwezo wako unaachana nacho.
Tatu unakuwa tayari kusamehe kila kitu, hakuna chochote ambacho unakiwekea kinyongo, unaelewa na kukubaliana na kila kitu na kisha unasamehe. Kwa sababu unajua kuweka vinyongo ni kuruhusu kuvurugwa.
Nne unajifunza kupotezea, kwa baadhi ya mambo ambayo watu wanafanya ili kukuvuruga, unayapotezea. Kama mtu amekutukana, unachukulia ni mtoto mdogo ambaye hajui kuongea, au kuchukulia ameongea lugha usiyoijua, au hujasikia.
Kutumia njia hizi kuepuka kuvurugwa haimaanishi kwamba unakubaliana na yote watu wanafanya, bali unayazuia yasivuruge utulivu wako wa ndani. Kama mtu amekosea na unapaswa kumpa adhabu kwa kosa hilo, lazima uitoe adhabu hiyo. Lakini unaitoa adhabu hiyo ukiwa na utulivu mkubwa ndani yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ahsante sana kocha, kwa mbinu hizi, kamwe hakuna mtu wa kunivuruga.
LikeLike
Vizuri Tumaini.
LikeLike