Moja ya faida ya uandishi na ualimu ni moja, unaweza kufanya kwa ajili ya wengine, lakini wewe mwenyewe ukanufaika sana na kile unachowafanyia wengine.

Unaandika kitu kwa ajili ya watu wengine, lakini katika uandishi wako, unapata njia za kukabiliana na hali fulani kwenye maisha yako mwenyewe.

Au unajiandaa kwa ajili ya kufundisha wengine, lakini katika mchakato wa kufanya hivyo, unajifunza zaidi wewe mwenyewe.

Uzuri ni kwamba, hilo haliishii tu kwenye kuandika na kufundisha, bali kwa kila kitu unachofanya kwa ajili ya wengine, kuna namna ya wewe kunufaika zaidi.

Unapowajali na kuwaheshimu wengine, hiyo inakufanya ujijali na kujiheshimu pia.

Unapowatia moyo wengine na kuwataka wasikate tamaa, hilo linakutia moyo na wewe pia.

Hivyo kuna mambo makuu mawili ya kuondoka nayo hapa;

Moja, unapojikuta kwenye hali fulani ambayo ungetamani aje mtu wa kukutoa hapo, angalia mtu mwingine ambaye amekwama na kazana kumsaidia kujikwamua. Kwa kumsaidia mtu mwingine, moja kwa moja unakuta umejisaidia na wewe pia. Huu ni msingi mzuri sana kwa chochote unachofanya, kwa tatizo lolote ulilonalo, angalia mwingine mwenye tatizo kama hilo na msaidie, kwa kufanya hivyo utajikuta unatatua matatizo yako kwa urahisi kabisa.

Mbili, kwa kila unachofanya kwa ajili ya wengine, pata muda wa kutafakari ni namna gani kinakunufaisha na wewe pia. Kwa kila ambacho unamshauri mtu mwingine, angalia ushauri wako unawezaje kukusaidia wewe mwenyewe. Nimekuwa nasema kama sisi wenyewe tungekuwa tunafuata ushauri tunaowapa watu wengine, tungepiga hatua sana. Hebu sasa anza wewe mwenyewe kufanyia kazi ushauri unaowapa watu wengine.

Faida kubwa ya kuwatumia wengine kutatua mambo yako ni kuondoa hisia ambazo mara nyingi huwa ni kikwazo. Unapokuwa kwenye matatizo, unayaangalia matatizo ambayo yanateka hisia zako na hivyo huwezi kufikiri. Lakini unapoangalia matatizo ya wengine, hayateki hisia zako, hivyo unaweza kufikiri kwa usahihi. Hapo utamsaidia kwa namna bora. Hivyo ukisahau yako kwa muda na kuangalia ya wengine, utapata njia sahihi ya kutatua yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha