Ukichukua mahindi na kuyaweka kwenye mashine ya kukoboa, yanatoka makande.

Ukichukua mahindi hayo hayo na kuyaweka kwenye mashine ya kusaga, unapata unga.

Umeanza na kitu kimoja lakini matokeo ni tofauti kwa sababu ya utofauti wa mashine.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye maisha yetu,

Kesho yako inategemea zaidi jinsi ulivyo leo.

Fikra na imani ulizonazo pamoja na hatua unazochukua leo ndiyo zinazotengeneza kesho yako.

Zamani watu walikuwa wanaamini kwamba hatima ya mtu imeshapangwa kabla hata hajazaliwa. Kwamba unapozaliwa tayari maisha yako yote yamepangwa, huwezi kwenda nje ya maisha hayo.

Lakini sasa tunaona wazi kabisa watu waliobadili maisha waliyotegemewa kuwa nayo kwa kubadilika wao wenyewe.

Kilichofanya watu waamini kwenye hatima ni ukosefu wa maarifa. Mtoto aliyezaliwa kwenye familia ya wakulima aliishia kuwa mkulima, kwa sababu ndiyo kitu pekee alichokuwa anakijua maishani mwake.

Mtoto aliyezaliwa kwenye familia masikini na yeye aliishi maisha ya umasikini akiwa mtu mzima, kwa sababu kila anachojifunza ni kuhusu umasikini.

Kadhalika mtoto wa mfalme alikuwa mfalme kwa sababu mazingira yalimwandaa hivyo.

Kwa kujua kwamba hatima ya mtu haijapangwa, bali anaitengeneza yeye mwenyewe kila siku, inatupa nguvu kubwa kwamba tunaweza kuyatengeneza maisha tunayoyataka sisi wenyewe.

Usiwasikilize wanaokuambia unapaswa hivi au unapaswa kuwa vile, wewe chagua ni maisha gani unayoyataka, kisha yaishi hao. Jifunze kwa wale walioishi maisha ya aina hiyo, fikiri muda wote kuhusu maisha ya aina hiyo na chukua hatua za kukuweka kwenye maisha ya aina hiyo.

Hakuna yeyote ambaye amepangiwa hatima yake tangu anazaliwa, bali kila mmoja wetu anaitengeneza hatima yake kwa kila anachofanya kwenye kila siku ya maisha yake. Hakikisha kila unachofanya kinatengeneza hatima nzuri kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha