Kila mmoja wetu ni kama amevaa miwani ya rangi ambayo anaitumia kuiangalia dunia.
Kama umewahi kuvaa miwani yenye rangi, unajua kila unachoangalia kitakuwa na rangi ya miwani hiyo. Hivyo siyo kwamba vitu hivyo vimebadilika rangi, bali miwani imekufanya uvione kwa rangi hiyo.
Kila mmoja wetu ana miwani anayoitumia kuiangalia dunia, miwani hiyo ni mtazamo ambao mtu anao. Mtazamo wako wa kiakili ndiyo unaochuja nini unaona na nini huoni na kwa kile unachoona, maana yake itatokana na mtazamo ulionao.
Hii ni kusema kwamba hatuioni dunia kama ilivyo, bali kama tulivyo sisi. Pia hatuwaoni watu kama walivyo, bali kama tulivyo sisi.
Kwa kujua hili, tunapata njia rahisi kabisa ya kuibadili dunia na hata kuwabadili watu wengine, ambayo ni kubadili mitazamo ambayo sisi wenyewe tunayo juu ya dunia na juu ya watu wengine.
Hatua ya kwanza unayoweza kuchukua na ikakunufaisha sana ni kuacha kuwa na maoni kwenye kila kitu. Huwa tunahangaika kuwa na maoni kuhusu kila kitu, hata vitu ambavyo hatuna uelewa navyo. Hali hiyo inatulazimisha kuhukumu vitu, kitu ambacho hakiwi sahihi kwani uelewa wetu una ukomo.
Ukishahukumu kitu, unabeba hukumu hiyo na kila wakati utakipokea kwa hukumu uliyotoa awali. Mfano kama umeshamhukumu mtu ana dharau, siku ukamsalimia na asiitike, moja kwa moja utajiambia ni dharau zake. Lakini huenda hakusikia, huenda yuko kwenye mawazo au amevurugwa kwa namna nyingine, yote hayo hutazingatia.
Unapoiangalia dunia, iangalie kwa mtazamo chanya, kwa kila linalotokea au kukutana nalo, liangalie kwa mtazamo chanya. Hata kwa watu pia, kuwa na mtazamo chanya wakati wote. Angalia kile chenye manufaa kwenye kila hali au kila mtu unayekutana naye. Kwa njia hiyo, utaona mambo mazuri na utaweza kuwa na maisha bora pia.
Na pale unapojikuta njia panda au kwa hali ya kukata tamaa, jikumbushe hili, kwamba unachoona sivyo kilivyo, bali wewe ulivyo. Hivyo ukibadilika wewe na kile unachoona kitabadilika pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,