Ukitaka kuvua samaki, unakuwa na ndoano ambayo unaiwekea chambo na kisha kuweka kwenye maji yenye samaki.

Samaki akiwa kwenye pita pita zake za kutafuta chakula, anaona chakula kizuri, anakifuata, anakula na kujikuta amenasa kwenye ndoano na hapo anavuliwa.

Ni kwa njia hiyo pia umakini wa watu umekuwa unashikwa, hasa mtandaoni.

Unaingia mtandaoni, lengo ni kutafuta kitu fulani, ukiamini baada ya muda mfupi utakuwa umetoka na kuendelea na kazi zako nyingine. Lakini unajikuta umetumia muda mwingi kwenye mtandao na hakuna cha muhimu ulichopata.

Kinachotokea ni unakuwa umenasa kwenye ndoano ambazo ziko mtandaoni na umakini wako umetekwa na kupelekwa kwenye maeneo yasiyo na tija kwako.

Uliingia mtandaoni ukiwa na lengo moja, mara ghafla unakutana na habari ya kusisimua, au picha inayokuvutia au kukushawishi utake kujua zaidi. Au umekutana na majibishano fulani yanayoendelea. Unaingia kujua zaidi na hapo unakuwa umenasa kwenye ndoani, unapoteza muda wako mwingi na umakini wako unahama kabisa.

Ubaya ni kwamba tumetegwa kila mahali sasa, kila eneo lina ndoano mbalimbali za kukamata umakini wetu. Matangazo mbalimbali yametengenezwa kwa namna ambayo yatanasa umakini wetu.

Wajibu wetu mkubwa kwenye zama tunazoishi sasa, ni kuepuka kunasa kwenye ndoano hizo zinazovua umakini wa watu. Tunaweza kufanya hivyo kwa njia tatu;

Njia ya kwanza ni kujua ndoano hizo, hapa ni kuwa na utambuzi wa vitu vyenye lengo la kunasa umakini wako. Habari nyingi mpasuko na zinazoshika hisia, hizo zina lengo moja, kunasa umakini wako. Ziepuke kama ukoma, pia epuka mitandao wakati unahitaji kufanya kazi muhimu.

Njia ya pili ni kuacha kunasa kwenye ndoano hizo, hapa ni kama huwezi kuondoka kwenye mazingira yenye ndoano, basi acha kunasa kwenye ndoano hizo. Kazana kupeleka umakini wako kwenye yale maeneo muhimu na epuka yale yasiyokuwa muhimu.

Njia ya tatu ni kuchomoka kwenye ndoano baada ya kunasa. Pamoja na kuepuka kunasa, kuna wakati utateleza na kujikuta umeshanasa kwenye ndoano bila kutegemea. Labda ulihadaika kitakuwa kitu muhimu, umefungua na kuingia na kukuta siyo muhimu, tambua hapo umeteleza na mara moja ondoka kwenye mtego huo ulionasa. Kibaya ni kwamba wengi wakishanasa kwenye ndoano, hawajitambui wamenasa, hivyo umakini wao unaburuzwa kwa muda mrefu. Wewe kwa kuwa makini na kujua wakati ambao umenasa, unaweza kuchomoka na kurudi kwenye umakini wako.

Tambua kwamba kila mtu anawinda umakini wako, kila mtu mtandaoni, kwenye vyombo vya habari na kwenye biashara mbalimbali anawinda umakini wako. Hiyo ni kwa sababu umakini wako ndiyo utajiri wao. Sasa hebu fikiria kama utaweza kutunza umakini wako na kuupeleka kwenye yale maeneo muhimu kwako, ni makubwa kiasi gani utafanya?

Linda umakini wako sana, ndiyo hazina yako pekee, usikubali wengine waiibe na kuitumia kujinufaisha wao wenyewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha