Kitu pekee tunachojifunza kwenye historia ni kwamba hakuna tunachojifunza kwenye historia, hiyo ni kauli aliyowahi kuitoa mwanafalsafa Hegel.

Ni kauli nzito na inayopaswa kutufundisha mengi, lakini kama Hegel alivyoeleza, haitufundishi chochote.

Iko hivi rafiki, hakuna kitu kipya kinachotokea hapa duniani kwa sasa. Kila kinachotokea sasa kimewahi kutokea huko nyuma, kwa sasa kimetokea tu kwa namna tofauti, labda kutokana na teknolojia kuwa ya juu.

Kuanzia matatizo yanayoikumba dunia, nchi na hata mtu mmoja mmoja, yote yamewahi kutokea tena huko nyuma. Maisha tunayoishi sasa ni marudio tu.

Lakini cha kushangaza, tunarudia makosa yale yale ambayo waliotutangulia waliyafanya walipokuwa wanapitia hali kama tunazopitia sasa. Kama tungechukua muda kujifunza kupitia waliotutangulia, tungepunguza makosa ambayo tunafanya.

Lakini hatufanyi hivyo, kwa sababu ambazo nakwenda kukushirikisha hapa. Kwa kila sababu nitakushirikisha hatua ya kuchukua ili maisha yako yaweze kuwa bora na uweza kukabiliana na kila changamoto unayopitia sasa.

Watu kuacha kusoma vitabu.

Uandishi ndiyo uvumbuzi mkubwa kuwahi kutokea duniani, alinukuliwa Abraham Lincolin. Hebu fikiria, leo hii unaweza kusoma vitabu vilivyoandikwa zaidi ya miaka elfu 2 iliyopita. Ni kwa sababu uandishi umeruhusu maarifa hayo kuweza kutunzwa na kurithishwa vizazi na vizazi.

Uzuri ni kwamba, kila unachopitia sasa, kuna mtu alishapitia miaka mingi iliyopita na akaandika kitabu kuhusu uzoefu wake kwenye hilo alilopitia. Kama mtu alipambana na kitu kwa miaka kumi na kukiandika kitabu, unaweza kukisoma kwa siku chache na ukaokoa kupoteza miaka 10 kwa kurudia makosa waliyofanya wengine.

Lakini cha kusikitisha ni kwamba watu wameamua kuacha kusoma vitabu. Wana kila sababu kwa nini hawasomi vitabu, lakini hakuna sababu yenye mashiko. Ni sawa na kukutana na mtu ambaye yuko mbio na unajaribu kumsimamisha anakuambia anachelewa. Ukimuuliza kwani unawahi wapi, hajui, lakini yuko kasi.

Ondoka mara moja kwenye tabia hiyo ya kutokusoma vitabu, chagua eneo unalotaka kubobea, amua wapi unataka kufika, kisha tafuta vitabu bora kwenye hayo na visome.

Ukitenga saa moja kila siku ya kusoma, au ukaweka utaratibu wa kusoma kurasa 10 za kitabu kila siku, kila mwezi utamaliza angalau kitabu kimoja na kwa mwaka angalau vitabu kumi.

Kama utatafakari yale uliyojifunza kwa kina, kisha ukachukua hatua kwenye maisha yako, huwezi kubaki pale ulipo sasa. Lazima utapiga hatua kubwa, utaepuka kurudia makosa ya wengine na kujifunza njia bora zaidi za kufanya unachofanya.

Karibu kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA, upate vitabu bora kwa maisha ya mafanikio, fungua; www.t.me/somavitabutanzania

Watu kupenda kusoma vitu vifupi.

Vitabu ni njia moja ya kujifunza, lakini pia zipo njia nyingine za kujifunza, kama kupitia makala, tafiti, ripoti mbalimbali na hata insha.

Uzuri ni kwamba, tunaishi kwenye zama ambazo mtandao wa intaneti unarahisisha kusoma maarifa hayo mbalimbali, tena bure kabisa.

Lakini cha kushangaza, watu hawapendi kusoma vitu virefu. Makala kama hii, wengi walioanza kusoma wameishia aya ya tatu, na wengine wanapita wakiangalia vichwa au maneno yaliyokolezwa tu.

Watu hawana tena umakini na utulivu wa kuweza kutenda dakika kumi za kusoma kitu kwa kina na kuondoka na maarifa ya kwenda kufanya kazi.

Usumbufu ni mwingi, kila mtu anapitia vitu juu juu, kinachotokea ni maarifa mazuri yanaelea huko mtandaoni huku wanaoyahitaji wakiteseka. Ni sawa na mtu ambaye anaogelea kwenye ziwa, lakini anakufa kwa kiu.

Kuondokana na hili, kwenye siku yako tenga muda ambao utasoma vitu kwa kina, ni bora usome vitu vichache kwa kina kuliko usome vitu vingi kwa juu juu. Kwa kila unachosoma, usikiache mpaka umeorodhesha nini umejifunza na namna gani unaenda kuboresha maisha yako.

Chagua mitandao au waandishi ambao utakuwa unajifunza kwao na weka umakini wako wakati unasoma kitu chochote kile. Usiwe na haraka wala kukimbilia popote, hakuna mashindano wala tuzo za aliyesoma vitu vingi zaidi. Tuzo pekee ni maisha yako kuwa bora, hivyo kazana na hilo.

Kama unapenda kujifunza kwa kina, una muda wa kusoma makala ndefu na kushiriki mijadala yenye tija, karibu kwenye MWONGOZO WA MAFANIKIO, fungua hapa; https://mafanikio.substack.com

Watu kutumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii.

Mitandao ya kijamii imepata umaarufu mkubwa na karibu kila mtu anaitumia kwa sasa. Mitandao hii imetuhadaa kwamba inatupa nafasi ya kuwasiliana na wengine na kutengeneza marafiki wengi.

Lakini ukweli wa mitandao huu umekuwa unafichwa. Mitandao hii imetengeneza mabilioni ya pesa, kwa kukuuza wewe. Angalia, hii mitandao haina bidhaa yoyote inayouza, na wewe unaitumia bure. Unajua inapataje pesa? Kwa kuuza umakini wako kwa watu wanaotaka kutangaza biashara zao mbalimbali.

Mitandao hii pia imechangia watu kukosa muda na umakini wa kusoma vitabu na mafunzo mengine mazuri.

Mtandao wa instagram umepata umaarufu mkubwa kwa sababu huhitaji kufikiria chochote, wewe piga picha yako na weka, halafu subiri wa kukusifia na kukupa likes.

Mtandao wa twitter umepata umaarufu mkubwa kwa sababu ukomo wa unayoweza kuandika, ambao ni herufi 280 tu, huwezi kuandika zaidi ya hapo. Hivyo ni vitu vifupi vifupi tu vinaandikwa huko, na kwa sababu watu hawataki vitu virefu, wanafurahia sana mtandao huo.

Rafiki, kama hutumii mitandao hiyo ya kijamii kibiashara, yaani kama huingizi fedha moja kwa moja kutoka kwenye mitandao hiyo, basi acha kuitumia mara moja. Hakuna manufaa yoyote unayoyapata kwenye mitandao hiyo, zaidi ya usumbufu, msongo na kupunguza umakini wako.

Jitoe kabisa kwenye mitandao yote ya kijamii, na ghafla utaona jinsi ulivyo na muda mwingi wa kufanya yale muhimu kwako. Nilichukua hatua hii mwaka 2018 baada ya kukaa kwenye mitandao hiyo kwa miaka 9 na sijawahi kujutia maamuzi hayo.

Kama unataka njia rahisi ya kujiondoa kwenye mitandao yote ambayo upo, fungua hapa; https://www.deseat.me

Watu kuishi kwa mazoea na kufuata mkumbo.

Hivi umewahi kukaa chini na kujiuliza kwa nini unafanya kila unalofanya? Umefanya kazi au biashara uliyonayo sasa kwa muda, lakini je unajua kwa nini uliingia kwenye kazi au biashara hiyo? Unajua wapi unapotaka kufika?

Hata mengine unayofanya kwenye maisha, labda umechukua mkopo, umejenga nyumba, umeoa au kuolewa, umewahi kujiuliza kwa nini ulifanya maamuzi hayo?

Kwa bahati mbaya sana, maamuzi mengi ambayo watu wanafanya ni kwa mazoea au kufuata mkumbo. Mtu anaambiwa wenzako wameshaoa au kuolewa, na yeye anafanya hivyo. Mtu anaona wenzake wanachukua mkopo na yeye anachukua.

Maisha ya aina hii yamekuwa hayakosi changamoto, kwa sababu mtu anahangaika na mengi lakini hayana maana kwake. Hivyo mwisho wa siku anayaona maisha yake yakiwa tupu, anaweza kuwa na kila anachoambiwa anapaswa kuwa nacho, lakini hana furaha.

Huwezi kuwa na furaha kwenye maisha kama hujayaishi maisha yako, kama hujajijua wewe mwenyewe na kuishi kwa uhalisia wako. Unaweza kupata kila ambacho wengine wanacho, tena wengine wakakuonea wivu kwa nafasi uliyonayo, lakini ndani yako ukajiona ni mtupu.

Acha sasa kuishi maisha ya mazoea au kufuata mkumbo, kwa kila jambo unalofanya, jua kwa nini unafanya. Kwanza kabisa jitambue wewe mwenyewe, jua uimara na udhaifu wako, jua wapi unataka kufika na maisha yako. Kisha hoji kila unalotaka kufanya linaendanaje na wewe na linakufikishaje kule unakotaka kufika.

Usiogope kufanya kitu peke yako, usiogope kupingwa, kukosolewa na kuchukiwa na wengine. Wewe pekee ndiye unayejijua kuliko wengine wanavyokujua, chagua kuyaishi maisha yako na siyo kuwafurahisha wengine.

Kutegemea furaha kutoka kwenye vitu vya nje.

Kama unajiambia ukishafika hatua fulani au kuwa na kitu fulani ndiyo utakuwa na furaha basi jua unatembea na laana. Hiyo ni kwa sababu hakuna furaha ya kudumu utakayoipata kwa kitu chochote cha nje yako. Unaweza kupata raha ya muda mfupi, lakini siyo furaha ya kudumu.

Kutegemea furaha kutoka kwenye vitu vya nje imekuwa ndiyo chanzo cha matatizo ambayo wengi wanakutana nayo kwenye maisha. Ulevi ambao wengi wanaangukia ni kutafuta furaha za nje na za haraka, kitu ambacho kimekuwa hakidumu.

Tambua kwamba furaha ya kweli na idumuyo inaanzia ndani yako, inaanza na wewe mwenyewe na haitegemei chochote cha nje. Kama huna furaha kabla hujapata unachotaka, hata ukikipata huwezi kuwa na furaha.

Mafanikio hayaleti furaha, bali furaha ndiyo inaleta mafanikio. Hivyo anza na furaha, jitambue, jua wapi unakwenda, jipende, penda unachofanya na kila siku piga hatua kuwa bora zaidi. Kwa njia hizi, utakuwa na furaha bila kujali uko kwenye ngazi ipi.

Rafiki yangu mpendwa, hizo ndizo sababu kubwa tano za changamoto nyingi tunazopitia kwenye maisha ya zama hizi. Tukiweza kutatua hizi kwa kuzingatia yale tuliyojifunza, hakuna kitakachokukwamisha, utakuwa na maisha tulivu, yenye furaha na mafanikio makubwa.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail  

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania