Kwa kuwa mambo ya kufanya ni mengi na yanazidi kuongezeka kila siku, huku muda wa siku ukibaki kuwa ule ule, unahitaji kuwa na njia sahihi ya kuweka vipaumbele vyako ili uweze kutumia muda mfupi ulionao vizuri.
Watu wamekuwa wanakosea kwa kufikiri njia sahihi ni kukazana kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja na kuyafanya kwa haraka zaidi. Lakini hata wanapofanya hivyo, bado mambo ya kufanya yanaongezeka na yale wanayokuwa wamefanya hayaleti matokeo mazuri.

Ili kujiwekea vipaumbele sahihi na kutumia muda wako vizuri, kuna vigezo vitatu unavyopaswa kuvizingatia.
Kigezo cha kwanza ni umuhimu. Jambo lolote unalofanya linapaswa kuwa muhimu na lenye mchango kwako kupiga hatua zaidi. Kama siyo muhimu usijisumbue hata kulifanya, maana hata ukifanya kwa haraka, hailibadili. Kwa kigezo cha umuhimu tu unatosha kufuta mambo nane kati ya kumi yaliyo mbele yako unayotaka kufanya.
Kigezo cha pili ni usahihi. Ukishajua kile kilicho muhimu kufanya, kifanye kwa usahihi. Haina maana kuweka muda wako kwenye kufanya kitu kisha usikifanye kwa usahihi, hiyo kulazimika kurudia tena kukifanya. Ni bora utukie muda zaidi kufanya kitu kilicho sahihi, kuliko kuokoa muda na ufanye kisichokuwa sahihi.
Kigezo cha tatu ni ufanisi. Unapaswa kufanya kitu muhimu, kwa njia sahihi na namna ambayo ni bora. Kila wakati boresha zaidi unachofanya, usifanye kwa mazoea. Kila njia unayotumia kufanya angalia namna ya kuiboresha zaidi. Kwa kujisukuma kuwa bora kila unapofanya, unapunguza muda wa kufanya na hivyo kupata muda zaidi.
Vigezo ni hivyo vitatu, fanya yale tu yaliyo muhimu na yafanye kwa usahihi huku ukiboresha ufanisi wako. Usihangaike na mengi, usitake kufanya mengi kwa wakati mmoja au kwa haraka. Kama kitu siyo muhimu, haijalishi umekifanyaje, kinabaki kuwa siyo muhimu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kweli kabisa, ahsante kocha.
LikeLike
Karibu Tumaini.
LikeLike