Kinachowafanya wasanii au watu wengine maarufu kuingia kwenye madawa ya kulevya ni hiki.

Kazi zao zinahusisha kutoa burudani au huduma kwa watu wengi kwa wakati mmoja. Pale wanapokuwa wanafanya kazi yao, wanakuwa kwenye furaha ya hali ya juu sana.

Fikiria msanii anafanya tamasha linalohudhuriwa na watu zaidi ya elfu 10 au mtu anahutubia watu wengi kwa wakati mmoja. Kitendo hicho kinamfanya ajione yuko juu na kinampa furaha  kubwa sana.

Sasa mtego uko hapa, hilo haliwezi kutokea kila siku. Msanii hawezi kufanya matamasha ya aina hiyo kila siku au hata kila wiki. Kuna kipindi ambacho anakuwa hana matamasha ya kufanya yanayomweka kwenye hali ya furaha.

Lakini yeye anataka kupata furaha kama ambayo huwa anaipata akiwa jukwaani na hapo ndipo anapojikuta akijaribu kutumia madawa ya kulevya kitu kinachompa furaha hiyo kweli. Lakini pia haidumu, anajikuta akihitaji kutumia mara kwa mara na hilo kupelekea awe na uraibu wa madawa hayo.

Huo ni mfano mmoja kwa wasanii, lakini hivyo ndivyo wengi wanavyonasa kwenye mtego wa furaha. Kutaka kuwa na furaha kila wakati. Kitu ambacho hakiwezekani.

Hakiwezekani kwa sababu furaha ni matokeo ya kemikali zinazofanya kazi kwenye ubongo wako, kemikali hizo huwa zinazalishwa kwa vichocheo mbalimbali na kiwango chake cha kuzalishwa kinatofautiana.

Kuna kemikali ya dopamini inayozalishwa kwa kukamilisha lengo, endofini inayozalishwa unapofanya zoezi, serotonini inayozalishwa unapojiona uko juu ya wengine na oksyitosini inayozalishwa unapojumuika na wengine.

Ni vigumu kwenye kila dakika ya siku yako ukawa kwenye hali zinazozalisha kemikali hizo, tena kwa viwango ambavyo ni vikubwa. Hivyo badala ya kukimbizana na kutaka kuwa na furaha muda wote, itakuwa na manufaa kama utaelewa jinsi mwili na akili zako zinafanya kazi.

Mfano kila siku kujiwekea malengo ambayo kuyakamilisha kunaachilia kemikali ya dopamini. Kufanya mazoezi ambayo yatazalisha kemikali ya endofini. Na kushirikiana na wengine, kitu kitakachozalisha kemikali ya serotonini na okysitosini.

Kutokuwa na furaha kwenye siku yako haimaanishi kwamba kuna kitu ambacho hakipo sahihi, bali inamaanisha mwili na akili yako havijawa kwenye mazingira sahihi ya kuzalisha kiwango cha kutosha cha kemikali hizo za furaha.

Usikimbilie njia za mkato za kuzalisha kemikali hizo, kama pombe, madawa ya kulevya au mitandao ya kijamii, badala yake fanya kile kitakachozalisha kemikali hizo na utakuwa kwenye hali nzuri.

Jambo muhimu kabisa la kuondoka nalo hapa ni kujua furaha siyo kitu unapaswa kuwa nacho masaa 24 kwa siku, siku zote saba za wiki. Kuna mengi unakutana nayo kwenye siku yako yanayokukwamisha au kukukwaza, yanapelekea kuzalishwa kwa kemikali nyingine ya msongo inayoitwa kortisol.

Kupitia hali ya kutuwa na furaha ni jambo la kawaida, muhimu ni kujua nini kinasababisha, kisha kukirekebisha na kurudi kwenye kiwango chako cha furaha. Usikimbilie njia za mkato, huwa zinafanya kazi haraka, lakini huwa zinatengeneza uraibu ambapo huwezi tena kutengeneza furaha bila ya njia hizo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha