Mtandao wa intaneti una nguvu ya kukupatia maarifa yanayofundishwa kwenye chuo chochote kile duniani bure kabisa. Lakini nguvu ya vyuo imebaki kwenye vyeti ambavyo vinatolewa kama ushahidi wa mtu kusoma kitu husika.

Hiyo ina maana kwamba, kama huna cheti cha kusomea kitu husika, haimaanishi huwezi kukijua na kukitumia kuyafanya maisha yako na ya wengine kuwa bora zaidi. Zipo njia mbalimbali za wewe kuweza kufundisha kitu ambacho wewe mwenyewe hujasomea na kupata cheti, lakini umejifunza kwa njia nyingine.

Kwenye makala ya leo ya ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu, tunakwenda kujifunza jinsi unavyoweza kufanyia kazi na kufundisha wengine kitu ambacho hujatunukiwa cheti cha kukisomea.

Kabla hatujajifunza hatua unazoweza kuchukua, tusome maoni ya msomaji mwenzetu aliyeandika kuomba ushauri kwenye eneo hili.

Hello! Kocha

Ahsante sana Kwa Kubadilisha Maisha Yangu Kupitia Maarifa Haya Ya Thamani kubwa Unayonipatia Kila siku .

Mimi Nina Maarifa Mengi Ya Afya, Nina uwezo Wa Kumfundisha mtu kujitibu maradhi Yasiyoambukiza kama vile Kupunguza uzito, kitambi, na nguvu za kiume. Natumia Account ya Instagram kutoa Maarifa na Watu Wamenufaika sana, Sijasoma Udaktari, Mimi nimesoma Ualimu Tena Wa Sanaa! Lakini Nimewapa watu Maarifa Ya Afya  Wameyatumia Wanapona kabisa. Na ni kazi ambayo situmii nguvu kabisa!

1. Sasa kinachonisumbua Sijasoma Udaktari nikijitokeza hadharani  hofu yangu watahoji kuwa mimi nimesoma wapi Udaktari?

2. Je Nitumie mbinu gani ili Watu Waendelea kuniamini ? Kwa sababu nataka kujibrand, nimeona maudhui yangu watu wengi wanakopi na kupest kwenye peji zao .

3. Malengo Yangu natakuwa na Clinic Ya kutibu magonjwa Yasiyoambukiza, changamoto sijasoma Udaktari.

Naomba Ushauri wako Kocha Nakuamini, hakika ushauri Wako nitaufanyia Kazi. Ahsante sana. – Moses N.

Msomaji mwenzetu Moses ameeleza vyema pale alipokwama, kwa upande wake ni eneo la afya ambalo ana maarifa ya kutosha lakini anakwama kuyatumia kwa sababu hajasomea afya na kutunukiwa cheti. Kwa mwingine unaweza kuwa umekwama eneo jingine, labda ni teknolojia, elimu, siasa, michezo na mengineyo. Ushauri tunaokwenda kupata hapa unaweza kuugeuza na ukakusaidia kwenye eneo jingine ulilokwama, siyo kwenye afya pekee.

Zifuatazo ni hatua za kuchukua ili uweze kufanyia kazi na kufundisha eneo ambalo hujasomea na kupata cheti.

Pata maarifa ambayo ni sahihi.

Hatua ya kwanza na muhimu ni kupata maarifa ambayo ni sahihi eneo hilo. Japokuwa tunaishi kwenye zama za maarifa, maarifa mengi tunayokutana nayo mitandaoni siyo sahihi. Hivyo usiwe mtu wa kuzoa zoa maarifa mtandaoni ambayo hujapima usahihi wake kisha ukawashirikisha wengine.

Katika kupata maarifa sahihi, anza kwa kuchagua vitabu sahihi ambavyo vinakupa msingi sahihi kwenye eneo hilo. Kwenye afya na tiba mbadala, chagua vitabu vya msingi kwenye eneo hilo visivyopungua vitano, kisha visome kwa kina na kuelewa eneo hilo kwa msingi kabisa.

Hatua ya pili ni kutafuta kozi zinazotolewa bure kupitia mtandao wa intaneti. Vyuo mbalimbali vimekuwa vinatoa kozi za kila aina bure au kwa gharama ndogo kabisa. Kwa kujua eneo lako na kutafuta kwa usahihi utaweza kupata kozi nzuri za kujifunza.

Katika kupata maarifa sahihi, epuka mitandao ya kijamii, makala za mtandaoni au video za kwenye mtandao wa youtube. Sisemi kwamba hizo hazifundishi, zinaweza kuwa zinafundisha vizuri sana, lakini kama unataka kujifunza na uweze kuwafundisha wengine basi anza na vitabu na kisha kozi, makala na video fupi fupi iwe ni ziada tu, lakini siyo hatua yako ya kwanza kujifunza.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Own The Day, Own Your Life (Imiliki Siku Uyamiliki Maisha Yako).

Tengeneza mfumo mzuri wa masomo na andaa masomo kwa usahihi.

Baada ya kuwa umejifunza na kuijua misingi ya eneo unalotaka kufundisha wengine, sasa andaa mfumo wako wa kutoa mafunzo. Usiwe mtu wa kukurupuka au kuandika vitu kwa lengo la kushika hisia za watu.

Badala yake tengeneza mafunzo ambayo utakuwa unayatoa. Kwa upande wa afya unaweza kuchagua magonjwa ambayo unaona yanawasumbua wengi kwenye jamii au ukachagua eneo la mwili ambalo utaandalia masomo.

Katika kuandaa masomo, weka rufaa ya vyanzo vyako vya maarifa. Kama ni kitabu kitaje. Pia pendelea kutumia tafiti mbalimbali zilizofanyika kwenye eneo husika.

Hapa unahitaji kutafuta tafiti zilizofanywa kwa usahihi kwenye eneo husika na zitumie katika kuandaa masomo yako. Kama kuna hoja unataka kuitetea, onesha ushahidi wa tafiti ambazo zinakubaliana na hoja hiyo.

Mambo mengi unayopendelea kufundisha unaweza kuwa na uzoefu nayo wewe binafsi kwa kuwa umekuwa unayatumia. Usitegemee uzoefu wako huo pekee kwenye kuandaa masomo yako. Badala yake changanya uzoefu wako na maarifa yaliyopo kwenye vitabu na tafiti mbalimbali.

Hapa pia epuka kutumia makala za mitandaoni kama ushahidi, huwezi kujua usahihi wake. Hivyo tumia vitabu na tafiti zilizofanywa kwa usahihi.

Kuwa mkweli na jua mipaka yako.

Unapoandaa na kutoa masomo yako, kuwa mkweli na mwaminifu. Usidanganye wala kuongeza chumvi. Epuka kuandaa masomo kwenye maeneo ambayo wengi wanasumbuka nayo huku wewe huna ujuzi sahihi au uzoefu kwa sababu tu kuna soko. Kwenye afya hapa wengi hukimbilia kwenye matatizo ya uzazi, ambayo yanawasumbua wengi, wanaona soko lipo, na watu ni rahisi kushawishika. Wewe epuka hilo, fundisha au shauri pale tu unapokuwa na uelewa wa kutosha ana ambao utamsaidia mtu.

Kitu kingine muhimu ni kujua mipaka ya elimu au ushauri wako na kipi ambacho kipo nje ya uwezo wako. Unapotoa mafunzo na ushauri wa afya kwa wengine, watakuletea matatizo ambayo unajua kabisa hayo ni nje ya kile unachoweza wewe. Usitake kuonekana unajua sana au kutaka kuwafanyia watu majaribio. Badala yake wape ushauri sahihi, kama ni jambo linalohitaji kwenda hospitali na kupata vipimo na matibabu zaidi basi mshauri mtu afanye hivyo. Hata kama kwa kufanya hivyo itakupunguzia wateja, jua itakujengea heshima kubwa na kuaminika na wale unaowalenga.

Kingine muhimu ni kuwa makini sana na shuhuda unazopokea kutoka kwa watu unaowashauri au kuwafundisha. Kwenye eneo la afya, ni vigumu sana kujua ni kitu gani kimemponya mtu. Hata dawa za hospitali tu zenyewe, zinaweza zisimponye mtu kabisa au mwingine akatumia na kupona, lakini kilichomponesha siyo dawa aliyopewa. (Kujua kwa undani hili, soma kitu kinaitwa Placebo Effect). Hivyo basi, unapopokea shuhuda za wale unaowashauri na kuwafundisha, zichuje kabla hujazitumia kwa wengine. Angalia kama kweli anachosema mtu kinatokana na tiba mbadala aliyotumia. Pia jipe muda na mfuatilie mtu kabla hujatumia ushuhuda wake.

Muhimu zaidi kwa kila ushuhuda wa tofauti unaoupata, angalia kwenye tafiti mbalimbali kama kuna wengine wamewahi kupata matokeo ya aina hiyo. Ukiweka umakini wako kwenye kuchuja shuhuda, utashirikisha shuhuda ambazo ni za kweli na hivyo watu kujenga uaminifu kwako.

SOMA; Tano Za Juma Kutoka Kitabu BULLETPROOF DIET (Mfumo Bora Wa Ulaji Utakaokuwezesha Kupunguza Uzito, Kuwa Na Nguvu Na Umakini Mkubwa Na Kuwa Na Afya Bora)

Zijue taratibu zote za kisheria kwenye eneo hilo.

Kila tasnia ina taratibu zake za kisheria, wale wanaosomea wanafundishwa hizo. Wewe kwa kuwa hukuenda shule kwenye eneo hilo, basi unapaswa kutafuta na kuzijua taratibu za kisheria kwenye eneo husika.

Eneo la afya lina taratibu nyingi za kisheria, hivyo unapaswa kuwa makini sana. Kwanza kabisa usijipe cheo cha kiafya ambacho huna, usijiite daktari au vyovyote vile, wale wenye vyeo hivyo wana leseni na wanajua namna gani wanabanwa. Pili usitangaze bidhaa yoyote ya kiafya, sheria hairuhusu bidhaa za afya kutangazwa kama vitu vingine. Hivyo wewe unapaswa kuegemea upande wa kutoa elimu na ushauri wa afya.

Kama kuna bidhaa au vitu unawashauri watu watumie, ambavyo siyo vya asili, basi jua uhakika wake na iwapo vimedhibitishwa na mamlaka mbalimbali.

Kuwa na blogu unayoweka maudhui yako.

Masomo unayoyaandaa usiyasambaze hovyo mitandaoni, wengi watayaiba na kuyafanya yao huku wewe ukiwa umeingia kazi kubwa kuyaandaa. Hivyo unapaswa kuwa na blogu ambayo unaweka mafunzo yako.

Kwenye mitandao ya kijamii unaweza kueleza kwa uchache, lakini ili mtu apate somo kamili basi anapaswa kuingia kwenye blog na maelekezo ya kufanya hivyo unayaweka.

Kwa kufanya hivi, utatengeneza wasomaji kwenye blog na hapo utaweza kuwapa huduma zako zaidi.

Tengeneza njia ya kuingiza kipato mapema.

Utakapoanza, kwa kiasi kikubwa utakuwa unatoa elimu na ushauri bure kwenye eneo ulilochagua. Lakini unapaswa kuwa tayari na mpango wa namna gani utaingiza kipato kwenye eneo hilo.

Unapaswa kuandaa mapema bidhaa au huduma utakazowauzia wale wanaokufuatilia ili uweze kuingiza kipato.

Kwa upande wa afya inaweza kuwa ni virutubisho ulivyoandaa wewe na unaviuza au virutubisho vya wengine unavyoviuza na kupata kamisheni. Inaweza pia kuwa ni huduma za mafunzo na ushauri zaidi, labda kuna kundi la mafunzo unalo au mtu kupata ushauri wako kwa kuonana ana kwa ana au kwa njia ya simu.

Unaweza pia kuandika kitabu chenye maarifa hayo ya msingi na mtu akakinunua ili kuendelea kujifunza mwenyewe.

Anza mapema na mpango wa kulipwa ili juhudi unazoweka kukuza hadhira yako zisipotee. Na watu wanapoanza kukufuatilia, tangu mapema wanajua wakitaka zaidi kwako wanapaswa kufanya nini.

Mfano mtu anaweza kusoma maarifa uliyoweka mtandaoni, akakupigia simu na kutaka umshauri zaidi. Kama hujapangilia huduma zako, utajikuta kila siku unatumia muda kuwashauri watu bure. Lakini ukiwa umepangilia huduma zako, utamweleza mapema kwamba utaratibu wa kupata ushauri ni huu, anaufuata na unampa ushauri.

SOMA; Imani Kumi (10) Potofu Kuhusu Ulaji Zinazowazuia Watu Kupunguza Uzito Na Kuwa Na Afya Bora.

Soma kozi fupi za tiba mbadala.

Kwenye kila tasnia, huwa kuna kozi fupi fupi zinatolewa na vyuo mbalimbali. Kwenye tiba mbadala pia kuna vyuo vinavyotoa kozi fupi fupi.

Tafuta vyuo hivyo na usome kozi hizo fupi, itakuongezea sifa zaidi na kukufanya ujiamini pia.

Ajiri mtu aliyesomea afya.

Kwenye mipango yako ya kukua zaidi na kufungua kliniki utahitaji kuajiri mtu aliyesomea mambo ya afya au afya mbadala.

Kufungua klinini ni tofauti kabisa na kuendesha mafunzo na ushauri mtandaoni. Utahitajika kuwa na leseni ambayo kuipata utapaswa kuwa na mtu aliyesomea na mwenye vyeti vyake.

Hivyo usione ni kikwazo kwako kushindwa kufungua kliniki, wapo wengi waliosomea maeneo hayo, unaweza kuwatumia kupata usajili na pia kuendesha kliniki yako.

Ushauri huu unakuonesha unapaswa kuweka kazi kweli kweli na siyo kuendesha kwa mazoea kama wengi wanavyofanya. Hivyo kama ni kitu kinachotoka ndani ya moyo wako kweli, ukifanyia kazi ushauri huu na ukajipa muda, utafanya makubwa sana kwenye eneo hilo. Kwa sababu wengi wa waliopo, hata wale waliosomea, hawafanyi kwa viwango nilivyoshauri hapa. Fanya kwa viwango hivi na utapiga hatua na kufanikiwa huku wengine nao wakinufaika.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania