Kwenye kitabu cha Thinking, Fast and Slow mwandishi ametushirikisha tafiti ambazo ukizitafakari kwa kina, utashangazwa sana na jinsi akili zetu zinavyofanya kazi.

Kwenye moja ya tafiti hizo ameonesha kwamba, tunachokumbuka kuhusu siku za nyuma siyo uhalisia wa tukio zima, bali jinsi tukio lilivyoisha. Kwa maana hii basi, sehemu kubwa ya kumbukumbu tulizonazo kuhusu siku zilizopita siyo sahihi. Na ni vigumu kujua hivyo kwa sababu akili yako inatoa upendeleo kwenye vitu fulani bila wewe kujua.

Tafiti nyingine ambazo mwandishi ameshirikisha ni kuhusu mipango mbalimbali ya makadirio, ambayo inawekwa na watu ambao ni wataalamu kabisa. Mara zote matokeo huwa tofauti na mipango ilivyowekwa. Makadirio kwenye muda na gharama, huwa hayawi kama mtu alivyopanga.

Kwa tafiti hizo mbalimbali na hata kwa uzoefu wetu, tunapata hitimisho moja; kwamba wakati uliopita na wakati ujao siyo sahihi, ni uongo. Huu ni ukweli unaoweza kutuumiza, lakini hatuna budi kukubaliana nao, maana kupingana na ukweli, hakuufanyi uondoke.

Swali unaloweza kujiuliza ni kama wakati uliopita na ujao ni uongo, je maisha yetu yote ni uongo? Jibu ni ndiyo na hapana.

Jibu ni ndiyo pale unapoweka muda wako kwenye kufikiria yaliyopita na kuhofia yajayo. Hapo unakuwa umechagua kuishi maisha ya uongo kwa sababu kumbukumbu ulizonazo siyo sahihi na makadirio unayojiwekea pia siyo sahihi.

Jibu ni hapana pale unapochagua kuishi kwenye wakati ulipo, kufikiria wakati wa sasa, pale ulipo kwa kile unachofanya. Sasa ndiyo wakati pekee wa ukweli kwenye maisha yako, unachokiona ndicho kilichopo kwa wakati huo na kile unachochagua kufanya sasa ndiyo unachoweza kukifanya kwa usahihi.

Lakini pia tunapaswa kuwa na tahadhari kwenye sasa, kuna wakati akili zetu zinatudanganya na sasa pia ikawa ya uongo. Kwenye kitabu hicho hicho, mwandishi ameshirikisha dhana anayoiita KILE UNACHOONA NDICHO PEKEE KILICHOPO (WHAT YOU SEE IS ALL THERE IS). Kwa tafsiri fupi, kuna wakati akili inachagua kuona kile unachotaka kuona, na siyo kile kilichopo. Hivyo unapaswa kuwa makini, kuhakikisha unaona kitu kama kilivyo na siyo kama unavyotaka kuona, kitu ambacho huendeshwa na hisia zako.

Wakati wa ukweli kwenye maisha yako ni wakati ulionao sasa, siyo wakati uliopita kwa sababu kumbukumbu ulizonazo siyo sahihi na wala siyo wakati ujao kwa sababu makadirio yoyote unayofanya siyo sahihi. Chagua kuishi sasa, chagua kukabiliana na kila kilicho mbele yako sasa kwa usahihi na utakuwa na maisha bora.

Muhimu zaidi ni kukumbuka kuona kitu kama kilivyo na siyo kama unavyotaka kukiona wewe.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha