Muda na pesa ni vitu viwili unavyoweza kutumia kupima vipaumbele vya mtu na hata kuweza kutabiri kwa uhakika mtu huyo ataishia wapi.

Tukianza kwenye vipaumbele, hata kama mtu hajakuambia chochote, ukiangalia jinsi anavyotumia muda na pesa zake, utajua wazi vipaumbele vyake ni nini.

Mtu anaposema kwamba hana muda wa kufanya kitu fulani, maana yake kitu hicho siyo kipaumbele kwake. Kwa sababu kila mtu ana masaa 24 kwenye siku yake, na katika masaa hayo kuna vitu anafanya, ili afanye kitu fulani, inabidi aache baadhi ya vile anavyofanya sasa. Na hapo ndipo kipaumbele kinapohusika, mtu hataacha kilicho muhimu kwake ili kufanya kisichokuwa muhimu.

Hivyo kama unajiambia huna muda wa kufanya vitu fulani, labda kujifunza, kusoma na mengine, jiambie tu ukweli, jiambie kwamba vitu hivyo siyo vipaumbele kwako, acha kujificha kwenye muda na kuwa mkweli kwako mwenyewe.

Kadhalika kwenye pesa, mtu anaposema hawezi kumudu kitu fulani, maana yake ni kwamba kitu hicho siyo kipaumbele kwake. Tunajua kitu kinapokuwa kipaumbele hasa, mtu atafanya kila namna aweze kukimudu. Hivyo kama huna pesa za vitu fulani, jua wazi hujavipa kipaumbele, hujavifanya kuwa vitu ambavyo uko tayari kufanya chochote ili kuvipata.

Kwa upande wa kutabiri, kama mtu atafanikiwa au la, wewe angalia tu jinsi anavyotumia muda na fedha zake. Mtu ambaye ana masaa 24 kwenye siku yake ambayo ameyajaza mambo mengi ya kufanya, lakini anakosa muda wa kujifunza, hawezi kufikia mafanikio makubwa.

Mtu ambaye kila kipato anachopata anatumia chote na anaenda mbele zaidi na kukopa kwa ajili ya matumizi, atabaki kwenye umasikini kwa kipindi chote atakachoishi kwa namna hiyo.

Usijisumbue kutabiri wengine wataishia wapi kwenye maisha yao,  badala yake jitabirie wewe mwenyewe. Jifanyie tathmini ya matumizi ya muda na fedha zako na jiulize kama ukienda hivyo utafika kule unakotaka kufika. Kama jibu ni hapana, anza kuchukua hatua sahihi sasa.

Kila siku fanya tathmini ya matumizi ya vitu hivi viwili, unapoimaliza siku yako angalia ulivyotumia muda wako na fedha zako kwa siku nzima, kisha jiulize kama ukienda hivyo kila siku utafika wapi. Tathmini za aina hii zitakuonesha mapema wapi unakosea na utaweza kuchukua hatua sahihi ili usipotee.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha