Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu kinachoitwa “Surely You’re Joking, Mr. Feynman!”: Adventures of a Curious Character. Kitabu hiki kinaelezea maisha ya aliyekuwa mwanafizikia wa nchini Marekani Richard P. Feynman ambaye alikuwa mdadisi sana.
Yale yaliyo kwenye kitabu hiki ni aliyoyasimulia Feynman kwa rafiki yake wa karibu aliyeitwa Ralph Leighton. Ni mkusanyiko wa matukio mbalimbali ya maisha ya Feyman kama tutakavyokwenda kuyaona.
Kitabu hiki kimehaririwa na Edward Hutchings.

Utangulizi kutoka kitabuni.
Ralph Leighton anatuambia kwamba hadithi zilizopo kwenye kitabu hiki ni mkusanyiko wa yale aliyokuwa akiambiwa na Feynman kwa kipindi cha miaka 7 ambayo walikuwa wakishiriki pamoja kwenye kikundi cha kupiga ngoma.
Ndiyo, umesoma vizuri, mwanafizikia na aliyekuwa profesa wa chuo kikuu, pia alikuwa mpiga ngoma na mengine mengi ambayo tutajifunza kwenye uchambuzi huu.
Ralph anasema ni vigumu kuamini kama mtu mmoja anaweza kufanya mambo mengi na ya tofauti kama alivyokuwa anafanya Feynman.
Kupitia maisha ya Feynman, tunapata hamasa kubwa ya kuchagua kuyaishi maisha yetu kwa misingi sahihi, kuwa na udadisi, kujifunza na kujaribu vitu vipya.
Albert R. Hibbs ambaye alikuwa mwanafunzi wa Feynman anaeleza kwamba hadithi zilizopo kwenye kitabu hiki ni picha halisi ya tabia za Feynman ambazo zilikuwa udadisi, msukumo wa kutatua mafumbo, kujaribu vitu vipya, kuishi kwa misingi yake bila kujali wengine wanachukuliaje, utani, kuigiza, ubishi na kutokuvumilia kisicho sahihi. Kitabu kina mengi ambayo mtu akiyasoma atashtushwa, lakini anapata funzo kubwa.
Maisha ya Feynman yalijengwa kwenye msingi wa sayansi, hasa fizikia. Alipenda na kuamini sana kwenye sayansi. Aliumia pale alipoona wengine wanafanya makosa kwenye sayansi. Na mara zote alisimama upande wa sayansi, akifundisha kwa njia rahisi kueleweka na kuwafanya wanafunzi wake waipende sayansi.
Kwa wale ambao hatukupata bahati ya kuwa wanafunzi wa Feynman na kujifunza mengi kutoka kwake, kitabu hiki kinatupa nafasi ya kumjua na kujifunza kupitia maisha yake.
Kuhusu Feynman.
Richard Phillips Feynman alizaliwa mwaka 1918 kwenye mji mdogo unaoitwa Far Rockaway, ulioko New York nchini Marekani. Aliishi kwenye mji huo mpaka mwaka 1937, akiwa na miaka 17 ambapo alienda chuo kikuu cha MIT kwa miaka minne ambapo alipata shahada ya fizikia.
Mwaka 1939 alidahiliwa kwenye chuo kikuu cha Princeton ambapo alitunukiwa shahada uzamivu (PhD) kwenye fizikia mwaka 1942.
Akiwa Princeton alishiriki kwenye timu (Manhattan Project) iliyotengeneza bomu la nyuklia lililomaliza vita kuu ya pili ya dunia. Kati ya Aprili 1943 mpaka Novemba 1946 Feynman alikuwa kwenye timu ya ndani ya kutengeneza bomu hilo. Mchango wake kwenye utengenezaji wa bomu ulikuwa mkubwa kupitia ujuzi wake wa fizikia ya nadharia.
Baada ya kumalizika kwa mradi wa bomu, alienda kufundisha kwenye chuo cha Cornell mpaka mwaka 1951 ambapo alihamia chuo cha Caltech ambapo alikaa kipindi chake chote cha kazi.
Mwaka 1941 alioa mke wake wa kwanza ambaye alifariki kwa TB mwaka 1946. Mwaka 1951 alioa mke wa pili ambaye waliachana mwaka 1956. Na mwaka 1960 alioa mke wa tatu ambaye aliishi naye hadi kifo chake.
Feynman alifariki dunia Februari 15, 1988, akiwa na miaka 69.
Matukio mengi ya maisha yake tutakwenda kujifunza kwenye kitabu hiki.
Karibu kwenye uchambuzi.
Kitabu hiki kina sehemu tano;
Sehemu ya kwanza ni maisha ya awali ya Feynman mpaka anapokwenda chuo cha MIT. Kikubwa tunachojifunza kwenye sehemu hii ni udadisi wake tangu akiwa mtoto na maabara aliyoitengeneza nyumbani kwao huku akiwa fundi redio aliyetegemewa na wengi akiwa na miaka 11.
Sehemu ya pili ni miaka aliyokuwa kwenye chuo kikuu cha Princeton. Chuo cha Princeton kiliifungua dunia kwa Feynman, pamoja na kuwa mwanafunzi wa fizikia, alitumia muda wake kujifunza vitu vingine kama falsafa, baiolojia na aliweza kupiga hatua kubwa kwenye maeneo hayo. Pia akiwa Princeton aliona jinsi ambavyo watu hawajifunzi kwa kuelewa, bali kwa kukariri.
Sehemu ya tatu ni kipindi cha kutengenezwa kwa bomu la nyuklia. Feynman akiwa mwanafizikia mchanga, anakuwa mmoja wa timu iliyotengeneza bomu la nyuklia lililotumika kwenye vita kuu ya pili ya dunia. Wakati wa zoezi hilo, aliyekuwa mwanafizikia mkubwa kipindi hicho Niel Bohr alichagua kujadiliana nadharia mbalimbali na Feynman kwa sababu katika timu ya wanafizikia wote wakubwa, Feynman pekee ndiye ambaye hakuwa anamuogopa, alimbishia bila ya kujali ni mwanafizikia mkubwa.
Sehemu ya nne ni maisha yake akiwa chuo cha Cornell na baadaye Caltech. Sehemu hii pia ina safari yake aliyofanya nchini Brazil na kukaa mwaka mzima. Kwenye sehemu hii tunajifunza msimamo katika kuchagua, Feynman aliondoka chuo cha Cornell na kwenda Caltech na aliamua kubaki hapo licha ya kupata nafasi kwenye vyuo vingine ambapo angelipwa zaidi. Pia kwenye safari yake ya Brazil alijifunza jinsi ambavyo wanafunzi kwenye nchi hiyo walikuwa hawafundishwi sayansi, bali kukaririshwa ili wafaulu mtihani.
Sehemu ya tano ni maisha yake kama mwanafizikia na mambo mbalimbali aliyokuwa anakutana nayo kwenye maisha. Kwenye sehemu hii Feynman anatushirikisha mambo mbalimbali kwenye maisha yake kama mwanafizikia, moja kubwa ni pale alipotangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya Nobel kwenye fizikia. Awali alitaka kuikataa tuzo hiyo, lakini akashauriwa aipokee. Na hapo ndipo alipojifunza makosa mengi yaliyopo kwenye tuzo hiyo.
Tutakuwa na chambuzi tatu za kitabu hiki, uchambuzi wa kwanza utakuwa na sehemu ya kwanza na ya pili, uchambuzi wa pili sehemu ya tatu na ya nne na uchambuzi wa tatu utabeba sehemu ya tano.
Karibu kwenye uchambuzi huu tuweze kujifunza mengi kupitia Richard Feymnan aliyekuwa na maisha ya kipekee. Kuna mengi mno ya kujifunza kupitia misimamo yake, utani wake na mambo mengine aliyokuwa anayafanya nje ya fizikia.
Kupata uchambuzi wa kina wa kitabu hiki cha Surely You’re Joking, Mr. Feynman karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania
Kwenye channel hiyo utapata chambuzi za vitabu vingine vizuri pamoja na vitabu vyenyewe kwa nakala tete. Kama unapenda kupiga hatua kwenye maisha yako, sehemu sahihi kwako kupata maarifa ya vitabu ni kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA, fungua kiungo hiki na jiunge; www.t.me/somavitabutanzania
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.