Hapa nakwenda kukushirikisha sura moja kutoka kwenye kitabu cha aliyekuwa mwanafizikia Richard P Feynman. Sura hii inatufundisha kuhusu kufanya maamuzi na kuyaishi hayo badala ya kuhangaika na kurudia kufanya maamuzi hayo kila mara.

Kwenye kitabu chake kinachoitwa Surely You’re Joking Mr. Feynman ameshirikisha matukio mbalimbali kwenye safari ya maisha yake ya kisayansi na kawaida. Feynman alikuwa mtu anayependa utani, kudadisi, kuhoji na kujaribu vitu vipya kila wakati.
SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Surely You’re Joking, Mr. Feynman! (Maisha Na Matukio Ya Mtu Mwenye Udadisi)
Feynman natushirikisha kwamba alifanya kazi ya uprofesa wa fizikia kwenye chuo cha Cornell kwa muda. Lakini mazingira na idara nyingine zilizokuwepo kwenye chuo hicho havikumfurahisha. Hivyo hakuvutiwa kuendelea kufanya kazi kwenye chuo hicho. Akiwa Cornell aliona hapati watu wa kutosha wa kujadiliana nao kitu kitakachomsaidia kukua kitaaluma. Pia hakukuwa na ugunduzi mwingi unaofanyika.
Hali ya hewa ndiyo ilimpa hasira zaidi, mara kwa mara kulikuwa na baridi kali inayopelekea kuwepo kwa barafu njiani na hivyo kuwa vigumu kwenda kazini kwa gari. Siku moja akiwa anaenda kazini kwa gari, barafu ilikuwa kali kiasi cha gari kuteleza. Ilibidi ashuke ili kufunga minyororo kwenye tairi, zoezi ambalo ni gumu na kwa baridi iliyokuwepo, aliteseka sana. Hapo alifanya maamuzi kwamba hawezi kuendelea na maisha ya aina hiyo, lazima kutakuwa na sehemu nyingine isiyo na shida za aina hiyo.
Alikumbuka miaka ya nyuma aliwahi kutembelea chuo cha Caltech na alikumbuka jinsi mazingira yalivyokuwa mazuri na maprofesa wengine walivyo vizuri pia. Basi Feynman aliomba nafasi ya kufundisha kwenye chuo hicho, ambayo aliipata haraka.
Lakini chuo cha Cornell kiliposikia anataka kuondoka, nao hawakutaka kumpoteza, hivyo walimwahidi kumpa maslahi mazuri. Kila Ofa ambayo Caltech walimpa Feynman, Cornell walimpa zaidi ili tu abaki. Kila mara alijikuta njia panda, asijue achague upande gani. Mwisho kikaja kigezo cha likizo, Feynman alitaka kupata likizo ya mapumziko ya mwaka mzima (sabbatical). Caltech walikubali kumwajiri na mwaka wa kwanza kumpa likizo, yaani anaajiriwa na kuanza likizo ya mwaka hapo hapo. Hivyo alikubali ofa ya Caltech.
Feynman alikaa kwenye chuo hicho cha Caltech maisha yake yote ya kazi mpaka anafariki. Anakiri alipenda sana mazingira ya California na mahusiano yake na maprofesa wengine.
Lakini siku za mwanzo wakati ndiyo anahamia Caltech, hali ya hewa ilibadilika ghafla, kukawa na ukungu mkali kiasi cha kushindwa kuona mbele. Hali ilikuwa mbaya kiasi cha kumkasirisha Feynman na kuona ni bora angebaki Cornell, maana japo hali ya hewa ilikuwa mbaya, haijawahi kuwa mbaya kiasi hicho.
Alipiga simu kwenye chuo cha Cornell kuulizia kama nafasi yake bado ipo aweze kurudi. Aliambiwa nafasi ipo na atapigiwa simu kesho yake kupewa uthibitisho.
Siku iliyofuata, akiwa Calthech alikutana na profesa mwenzake aliyemwambia kuna mwenzao amefanya ugunduzi mpya kwenye nyota. Kulikuwa na tatizo ambalo Feynman alilijua na halikuwa limetatuliwa, ugunduzi huo ulikuwa umetatua tatizo hilo. Siku hiyo hiyo akapata taarifa kwamba profesa mwingine wa baiolojia amefanya ugunduzi kwenye vipimo uliosaidia kufuatilia uzalianaji wa bakteria.
Kwa taarifa hizo mbili za ugunduzi mkubwa na wenye manufaa, Feynman aliona Caltech ndiyo sehemu sahihi kwake. Baadaye Cornell walimpigia simu na kumwambia wanamalizia mipango ili arudi, akawajibu hawezi kurudi tena, amebadili tena mawazo.
Hapo alijipa msimamo kwamba ameamua kukaa Caltech na hakuna kitu kingine chochote kitakachobadili mawazo yake au kumfanya aamue tena tofauti.
Feynman anasema unapokuwa kijana na fursa nyingi kuwa mbele yako, huwa unasumbuka sana kuchagua. Unahitaji ufike mahali ufanye maamuzi ambayo hutarudi tena nyuma. Anatoa mfano akiwa mwanafunzi wa chuo cha MIT alikuwa njia panda kila anapoenda mgahawani, hivyo siku moja alichagua aina ya chakula atakachokuwa anatumia na tangu hapo hakusumbuka tena.
Miaka mingi baadaye, akiwa ameshafanya maamuzi ya kubaki Caltech, alipata ofa kutoka chuo cha Chicago. Wawakilishi wawili kutoka chuo hicho walimtembelea kumshawishi ajiunge na chuo hicho. Walimweleza jinsi chuo hicho kilivyo na fursa nyingi nzuri kwake kufanya makubwa.
Feynman aliwajibu kwamba alishaamua kubaki Caltech na hakuna cha kubadili maamuzi yake. Walimwambia hata mshahara atakaolipwa kwenye chuo cha Chicago ni mkubwa zaidi. Walimuuliza iwapo angependa kujua ni kiasi gani cha mshahara atapewa.
Feynman aliwaomba wasimtajie kiasi hicho cha mshahara, kwa sababu mke wake ambaye alikuwa chumba cha pili akisikia kiasi cha mshahara anaokataa, wataanza kubishana.
Mwezi mmoja baadaye alikutana na mtu mwingine kutoka Chicago aliyemwambia walisikitishwa sana na kitendo cha yeye kukataa ofa nzuri waliyompa. Alimwambia hawaelewi aliwezaje kukataa ofa kama hiyo. Feynman alimjibu ilikuwa rahisi, sikuruhusu wanitajie kiwango cha mshahara.
Wiki moja baadaye alipokea barua kutoka Chicago ikitaja kiwango cha mshahara ambacho angepewa kama angekubali, kiasi hicho kilikuwa mara 4 ya anachopata Caltech. Barua iliendelea kueleza kwamba nafasi bado ipo na wangependa sana kiwa naye.
Feynman aliandika barua kuwajibu ambapo alieleza haya; “Kwa kiwango hiki cha mshahara nimeamua kukataa zaidi nafasi mliyonipa. Hiyo ni kwa sababu kwa pesa nyingi hivyo, nitakuwa na uhuru wa kufanya kila aina ya starehe na hilo litakuwa kikwazo kwenye kazi zangu za kitaaluma.”
Hivyo Feynman alikataa nafasi hiyo na kubaki kwenye maamuzi yake ya mwanzo.
Hapa tunajifunza mtu kujua kile hasa unachofanya kisha kufanya maamuzi na kuyasimamia badala ya kuhangaika na maamuzi mapya kila wakati. Pia tunapaswa kuepuka tamaa ya fedha zaidi isiwe sababu ya kufanya maamuzi ambayo baadaye tutayajutia. Ni rahisi kuona fedha zaidi zitayaboresha maisha yako, lakini huenda zikayafanya maisha yako kuwa hovyo zaidi.
Fanya maamuzi ukizingatia ukuaji wako binafsi, kufurahia unachofanya na kuzungukwa na watu sahihi. Ukipata mazingira ya aina hiyo, yashikilie na nenda kaweke kazi, utazalisha matokeo bora yatakayokupa mafanikio makubwa kuliko kuchagua kitu kwa kuangalia kipato pekee.
Kupata uchambuzi kamili wa kitabu hiki ambacho kina visa vingi vya kujifunza, karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kwa kufungua www.t.me/somavitabutanzania
Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania