Kuna vitu ambavyo huwa vinakaribiana sana, ambapo mstari wa kuvitofautisha ni mwembamba sana kiasi kwamba usipokuwa makini unaweza kwenda upande usio sahihi.
Tukianza na kujikweza na kujiamini, hivi ni vitu vinavyokaribiana sana. Kujiamini ni kuzuri, kunakusaidia kufanya makubwa kwenye maisha yako. Lakini pale kujiamini huko kunapozidi na ukaona hakuna aliye kama wewe, basi hapo kunakuwa ni kujikweza. Pale ambapo unataka kila mtu akubaliane na wewe na kukusifu wewe, hapo ni kujikweza. Na kwa namna hiyo utaharibu mahusiano yako mengi. Jiamini, lakini usione wewe ni bora kuliko wengine, usidharau wengine na siyo lazima kila wakati utangaze mambo yako kwa wengine.
Ushahidi na kuamini, ni eneo jingine ambalo ni rahisi kuchanganya. Kuamini ni rahisi, jamii zetu zimejengwa kwenye kuamini, hata kama kitu hujawahi kukiona, kama wengine wanakiamini, basi na wewe unaamini. Lakini kuna wakati ushahidi unakuwa wazi kabisa, ambao unakwenda kinyume na kile unachoamini, wengi hukataa ushahidi huo na kushikilia kile wanachoamini. Usiwe mtu wa aina hiyo, hata kama ushahidi unapingana na imani yako, upe ushahidi uzito kuliko imani yako. Tambua imani nyingi ulizonazo siyo sahihi, hivyo unapopata ushahidi, ufuatilie kweli na utumie kwenye yale unayofanya.
Ukweli na maoni ni eneo ambalo linawachanganya wengi zaidi. Watu wamekuwa wanabeba kila wanachosoma au kusikia kutoka kwa wengine na kufanyia kazi. Kinachotokea ni hawapati matokeo sahihi, kwa sababu sehemu kubwa wanachokuwa wamechukua siyo ukweli bali ni maoni. Unapaswa kujua kutofautisha ukweli na maoni, ukweli ni kile kilicho sahihi kwa wengi na kwa kila hali, maoni yanaweza kuwa sahihi kwa watu fulani au katika hali fulani. Maoni pia ni kitu ambacho watu wanatengeneza, kutokana na mtazamo walionao juu ya kitu. Kwa kuwa tunaishi kwenye zama za mafuriko ya taarifa na maarifa, puuza maoni na tafuta ukweli. Ukweli utakusaidia kufanya maamuzi yaliyo sahihi.
Tambua upande ulio sahihi, ujue mstari mwembamba wa upande ulio sahihi na usio sahihi kisha jichunge usivuke mstari huo. Hiyo ndiyo njia ya kuwa na maisha rahisi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,