Kila mtu huwa anapenda kuwa maarufu, lakini wengi huwa hawajui gharama kubwa ambayo umaarufu inakuja nayo.
Wengi hukazana kufikia umaarufu na wanapoufikia wanajuta kwa nini walikuwa wanautafuta.
Hasa pale wanapokuwa maarufu kwa sababu walikuwa wanatafuta umaarufu na siyo kwa sababu kuna kitu kikubwa wamefanya.
Gharama kubwa ya umaarufu ni kukosa uhuru wa kuyaishi maisha yako kwa namna unavyotaka wewe.
Ukishakuwa maarufu, wale wafuasi wako wanakuwa wamekuweka kwenye gereza, wanategemea ufanye na uwe kama umaarufu wako ulivyo.
Hivyo kila hatua ambayo unachukua, inaonekana na kila mtu. Maisha yanaacha kuwa yako na yanakuwa ya wafuasi wako.
Kila wakati lazima uwafurahishe, ili waendelee kukupa umaarufu, nje ya hapo umaarufu wako utaanguka.
Wengi waliofanikiwa na wanaopenda kubaki na uhuru wao, wamekuwa wanashauri sana mtu kuepuka kutafuta umaarufu wa lazima. Na hata umaarufu ukikufuata kwa sababu ya mambo makubwa uliyofanya, usiupe uzito sana. Usikubali kuingia kwenye gereza ambalo umaarufu unakutengenezea.
Mitandao ya kijamii imekuwa sehemu rahisi ya watu kutengeneza umaarufu hewa. Ndiyo maana utaona wengi wanafanya mambo ya hovyo mitandaoni, kama kuweka picha zao za uchi au kuwashambulia wengine, ili tu wapate wafuasi wengi.
Na kwa zama zetu, watu maarufu na mashujaa siyo tena wanasayansi wanaovumbua vitu au watu waliojitoa na kufanya makubwa kwenye jamii, bali wale wenye wafuasi wengi mitandaoni.
Na njia za kupata wafuasi hao ni rahisi, tukana watu, kuwa ‘mchambaji’ maarufu, washambulie wengine, iba maarifa ya wengine na yashirikishe kama yako, weka picha za uchi, wadhalilishe wengine au weka picha na habari za kuhamasisha hata kama siyo kweli.
Uzuri ni kwamba, umaarufu huo wa njia za mkato huwa haudumu, kwa sababu wafuasi ambao mtu anakuwa amewapata siyo makini, akija mwingine mwenye utayari wa kufanya ujinga zaidi, wataenda naye na kumwacha wa awali.
Lengo lako kubwa kwenye maisha ni wewe kufikia ndoto zako na kutoa thamani kubwa kwa wengine. Mara zote pambana na hilo na usiingie kwenye mtego wa umaarufu. Usishawishike na wale wanaokuambia ukiwa maarufu itakuwa rahisi kwako kufikia ndoto zako, ni waongo, itakuwa vigumu zaidi.
Kama umaarufu utakuja, acha uje kwa matokeo ambayo umezalisha, ambayo yameongeza thamani kwa wengine. Usilazimishe umaarufu kwa lengo tu la kuwa maarufu, utaishia kuwa na wakati mgumu zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ahsante sana kocha. Ubarikiwe.
LikeLike
Karibu Tumaini.
LikeLike
Nimejifunza kuepuka watu ambao wana mtazamo hasi wakati wote wanawaza wamezaliwa kwaajili kushindwa,
LikeLike
Vizuri Mary
LikeLike