Kabla ya mapinduzi ya viwanda, watu wengi walikuwa wanafanya kazi zao binafsi na kila mtu alilenga aina fulani ya wateja ambao atawafanyia kazi. Hivyo mtu alipokuwa na uhitaji, alijua ni mtu gani anayemfaa kwa kazi aliyonayo.

Mapinduzi ya viwanda yalileta mabadiliko mengi, kubwa kabisa likawa kuzalisha bidhaa kwa wingi na kumlenga kila mtu. Hivyo bidhaa zilizozalishwa zilikuwa za kawaida ambazo zinaweza kumfaa kila mtu. Hilo linapunguza gharama za uzalishaji na kufanya bidhaa ziuzwe kwa bei ya chini ambapo wengi wanaweza kuzimudu.

Mtazamo huu wa viwanda umeharibu mpaka wale wanaofanya kazi zao binafsi, wanajikuta wakianza kulenga watu wengi kama viwanda vinavyolenga.

Kwa kufanya hivyo, wanakutana na upinzani mkubwa, kwa sababu watu wanaishia kuwafananisha na viwanda, wanawaambia mbona bei yako ni kubwa kuliko ya bidhaa nyingine zilizopo sokoni.

Mtu kwa kuambiwa hivyo, anaona suluhisho ni kupunguza bei ili iendane na ya bidhaa za viwanda. Lakini hata anapofanya hivyo, bado hapati wateja kama alivyofikiri awali.

Kama wewe ni mtu unayefanya kazi zako binafsi, iwe ni utoaji wa huduma au uzalishaji na uuzaji wa bidhaa, usijifananishe wala kujilinganisha na viwanda au taasisi kubwa zinazotoa huduma au bidhaa kama yako.

Badala yake wewe kuwa wa tofauti, kwanza kabisa chagua aina ya wateja ambao unawalenga, kisha waguse kwa utu wako. Wape kile ambacho hawawezi kukipata kwenye bidhaa za viwandani au huduma za taasisi kubwa.

Kitu cha kuanza nacho ni kujali utu wa mteja wako, kumthamini yeye kama mtu, tena wa tofauti kabisa na wengine. Kumjua kwa undani, kujua vitu anavyopendelea na kuona jinsi unavyoweza kumwandalia huduma au bidhaa ambayo itaendana na yeye na kumtofautisha na watu wengine.

Kwa kufanya hivi, utaweza kutoza gharama kubwa zaidi na bado watu wakaja kwako kwa sababu wanachokipata hawawezi kukipata sehemu nyingine yoyote.

Lakini pia kwa kufanya hivi, kuna watu watakupinga, kukukosoa na kukukataa. Watakuambia gharama zako ni kubwa, watakuambia wanaweza kupata pengine na wengine watakushauri uwe kama viwanda taasisi nyingine, usibabaishwe na watu wa aina hiyo. Jua siyo wateja wako, jua hawaelewi kile unachofanya na peleka nguvu zako kuwafikia wateja walio sahihi na kuwapa kile kilicho bora kabisa.

Kwa njia hii utaonekana kwenda taratibu, na kuonekana kuchelewa, lakini ukishaujenga msingi, matokeo yanakuwa makubwa baadaye.

Kama unafanya kazi zako binafsi, usijilinganishe na kiwanda au taasisi kubwa, weka utu wako kwenye kile unachofanya na gusa utu wa wengine, utaweza kuwahudumia wateja sahihi na kutoza kiasi kikubwa kuliko viwanda au taasisi zinavyotoza.

Msingi wa viwanda au taasisi ni kutoa bidhaa/huduma za kawaida kwa watu wa kawaida. Msingi unaupaswa kuwa nao wewe ni kutoa bidhaa/huduma za kipekee kwa watu wa kipekee.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha