“It seemed that one had little control over one’s own destiny. All one could do was to get on with the one job that nobody else could do, the job of being oneself.” — Monica Dickens, Mariana

Mafanikio makubwa kwenye maisha huja pale mtu anapofanya kitu cha kipekee, kitu ambacho hakuna mwingine anayeweza kukifanya.
Kwa kuwa dunia ina wengi wanaofanya vitu vya kawaida, kufanya wanachofanya wengine ni kujiingiza kwenye ushindani mkali ambao utapelekea ushindwe.

Kwa kuwa ni vigumu kujua kipi cha tofauti wewe kufanya,
Ipo njia moja ya uhakika ya kukuwezesha wewe kufanya kilicho tofauti kabisa na wanachofanya wengine.

Njia hiyo ni kuchagua kuwa wewe, kwa uhalisia wako bila kuiga wengine.
Iko hivi rafiki, hakuna mtu nwingine aliye kama wewe hapa duniani.
Na hakuna anayejua wewe ukoje, isipokuwa wewe mwenyewe.

Hivyo utakapochagua kuwa wewe, utakuwa umejitofautisha na wengine wote.
Na chochote unachofanya, ukikifanya kama wewe utaleta matokeo makubwa na ya tofauti kabisa.

Ifanye kazi yako kama wewe,
Ifanye biashara yako kama wewe,
Weka utu na upekee wako kwa kila unachofanya,
Jali zaidi kile unachofanya.
Kwa njia hiyo utaweza kufanya makubwa sana.

Zama tunazoishi sasa, kila mtu anakazana kuiga wengine,
Kitu ambacho kimepelekea watu kukosa msimamo kwenye maisha yao.
Hadithi za waliofanikiwa zimekuwa nyingi na kila mara mtu anapojifunza hadithi mpya, anabadilika na kuwa mtu mwingine, kwa kuiga yale ya aliyejifunza kwenye hadithi yake.

Haimaanishi usijifunze kwenye hadithi za waliofanikiwa,
Bali usijaribu kuwa kama wale unaojifunza kupitia hadithi zao.
Wao hawakufanikiwa kwa kuwa kama watu wengine, bali walifanikiwa kwa kuwa wao.

Hivyo chagua kuwa wewe na kila hadithi mpya unayojifunze, iweke mkazo na msimamo kwenye kuwa wewe.

Asubuhi ya leo tafakari kama bado unajikumbuka wewe mwenyewe.
Angalia ni vitu gani viko ndani yako na umekuwa unakazana kuvificha,
Angalia ni utu gani unaoweza kuweka kwenye kazi au biashara yako.
Kisha anza kuchukua hatua mara moja,
Anza kuishi wewe, kwa kutoa kila kilicho ndani yako.
Na kwa hakika, maisha yako yatabadilika na dunia itakupa heshima ya tofauti.
Usidharau upekee wowote ulio ndani yako, ukiutumia vizuri, utakusaidia sana.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu sharti na chaguo, soma zaidi hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/09/03/2073

Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.