Kama umewahi kulima hata bustani ya mboga au maua, unajua kwamba kuondoa magumu kwenye eneo unalolima ni zoezi lisilo na ukomo. Huondoi mara moja na shamba likawa safi milele. Kila wakati unapaswa kurudia zoezi la kuondoa magugu.

Kadhalika kwenye kusafisha miili yetu, mtu unaoga kila siku kwa sababu uchafu unajirudia mara kwa mara kwenye mwili.

Lakini kuna maeneo ya maisha yetu ambayo tumekuwa hatufanyi usafi huu endelevu.

Na eneo muhimu sana linalohitaji zoezi hili ni muda wetu. Unaweza kupanga kabisa ni vipaumbele vipi vitachukua muda wako. Lakini baada ya muda, ukajikuta unatumia muda wako kwenye vitu ambavyo siyo vipaumbele kabisa.

Vipaumbele ambavyo vinakufikisha kule unakotaka kufika ndiyo zao la shamba la maisha yako. Mambo mengine yote yanayowinda muda wako ni magugu.

Ili upate mafanikio makubwa, unapaswa kuondoa magugu hayo, na siyo kufanya hivyo mara moja, bali kufanya kwa kurudia.

Kila wakati fanya zoezi la kuondoa magugu kwenye muda wako, kila unapoianza siku yako panga yale unayokwenda kufanya na unapoimaliza fanya tathmini ya yale uliyofanya ukilinganisha na vipaumbele ulivyokuwa umejiwekea.

Kama utaona kuna mambo yamechukua muda wako ambayo hayapo kwenye vipaumbele vyako, yaweke kwenye orodha ya mambo ambayo hutayafanya na kila unapotaka kufanya jikumbushe kwamba mambo hayo umeshayafuta.

Kadhalika kila unapoanza kufanya kitu chochote, jiulize kama kipo kwenye vipaumbele vyako, kama hakipo, usifanye.

Maisha ni mafupi, muda una ukomo, ya kufanya ni mengi lakini yaliyo muhimu kwako kufika unakotaka kufika ni machache, yatambue hayo machache na yape kipaumbele kisha fanya zoezi la kuondoa magugu kila wakati.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha