Kwa zama tunazoishi sasa, wengi wanaona njia rahisi ya kufikia mafanikio makubwa ni umaarufu.
Kwamba kadiri watu wengi zaidi wanavyokujua ndivyo unavyopata mafanikio makubwa.
Ni rahisi kufikiria hivyo kabla mtu hujafika kwenye ngazi hiyo ya umaarufu. Lakini wale waliofika kwenye ngazi hiyo, hugundua haiwapi uhuru. Wakishakuwa maarufu maisha yanaacha kuwa yao na jukumu lao linakuwa kulinda umaarufu walionao.
Ipo njia nyingine ya uhakika ya kufikia mafanikio makubwa ambayo ni kinyume na umaarufu, njia hiyo ni uaminifu.
Mtu unapojenga uaminifu mkubwa, unawavutia kwako watu walio sahihi na hilo linakusaidia kufikia mafanikio makubwa. Japo mafanikio kwa njia hii huwa hayaji kwa haraka, lakini yanapokuja yanampa mtu uhuru mkubwa.
Mitandao ya kijamii inatupa njia rahisi ya kupata umaarufu, lakini kwa kuwa njia hiyo ipo wazi kwa kila mtu, umaarufu huo umekuwa haudumu. Na kwa sababu kila mtu anautafuta, basi wengine wapo tayari kufanya hata mambo ya kijinga kabisa ili kuupata umaarufu.
Kinachotokea ni watu kujikuta wapo kwenye mashindano ya kufanya ujinga, ili tu kuwa maarufu. Wenyewe wanaita kiki, lakini hazidumu, hivyo inabidi mtu aendelee kufanya ujinga zaidi na zaidi.
Lakini uaminifu haupatikani haraka, na haupatikani kwa kufanya mambo ya kijinga, bali uaminifu hupatikana kupitia kazi ambayo mtu anaifanya, kwa kujiwekea viwango ambavyo anavifikia na kuahidi vitu anavyotimiza.
Uaminifu hujengwa kidogo kidogo na ukilindwa, unadumu na kuwa na nguvu kubwa.
Njia mbili ziko mbele yako, unachukua ipi, umaarufu ambao utakuponyoka haraka au uaminifu ambao utadumu na wewe? Maisha ni yako, chaguo ni lako. Jua kila chagua lina majukumu ambayo lazima uyatimize.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,